Thursday, November 23

Yono yajipanga upya mnada nyumba za Lugumi




Dar es Salaam. Mnada wa majumba ya kifahari ya mfanyabiashara maarufu, Said Lugumi utarudiwa kesho, huku kampuni ya udalali ya Yono, ikitoa masharti mapya kwa washiriki ikiwemo kutoa Sh2 milioni kama gharama ya ushiriki.
Mnada huo wa tatu utafanyika kesho Ijumaa Novemba 24,2017 baada ya wa Septemba 7,2017 kukosa mshindi na wa Novemba 9,2017 kudaiwa kuvurugwa na ‘bilionea’ Dk Louis Shika aliyefika bei kwa nyumba zote tatu lakini alishindwa kutimiza masharti ya kulipa asilimia 25.
Katika mnada huo, majumba mawili ya Lugumi moja la Mbweni JKT na la Upanga yatauzwa kufidia Sh14 bilioni anazodaiwa zikiwa ni kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 23,2017 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Yono, Scholastika Kevela amesema wamejizatiti kuhakikisha hakuna mtu atakayeharibu mnada huo kama inavyodaiwa kufanywa na Dk Shika.
“Mchezo ule ambao tulichezewa mara ya mwisho hautarudiwa, kwa sasa tumekuja na masharti magumu kwamba, washiriki wote watakaoingia katika minada uwe mshangiliaji au mtazamaji lazima utajiandikisha katika kitabu maalumu cha washiriki wa mnada,” amesema Kevela.
Amesema, “Baada ya kujiandikisha, tutakujazia fomu maalumu ya kushiriki mnada, tutakuchua taarifa mbalimbali kutoka katika vitambulisho vyako vya Taifa, leseni ya udereva au pasi ya kusafiria.”
“Kama kweli wewe ni mshiriki halali tutakutaka utoe Sh2 milioni kupitia akaunti ya Yono kama dhamana ya ushiriki kuwa unataka kununua nyumba, ukishinda mnada hiyo Sh2 milioni ni sehemu ya malipo na kama ukishindwa kupata mali au bidhaa tunakurudishia mara moja,” amesema.
Amesema kwa atakayeshindwa kupata mali na Sh2 milioni ametoa na kisha akaharibu mnada, hatarudishiwa fedha na hatua za kisheria zitachukuliwa. Amesema mshindi wa mnada atatakiwa kulipa papo hapo malipo ya awali ya asilimia 25.
“Kama utasema ziko Kenya ziko wapi, tutakuchukua chini ya ulinzi kwenda benki mama, baba umeshinda nyumba lipa. Mnada tutaurudia palepale na asilimia 75 ya yule mshindi atatakiwa kulipa la sivyo fedha aliyotoa awali ya asilimia 25 haitarudishwa,” amesema Kevela.

No comments:

Post a Comment