Thursday, November 23

Rais Magufuli kubariki ufunguzi wa hospitali Mloganzila


Dar es Salaam. Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 23,2017 Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema hospitali hiyo itakayofunguliwa Jumamosi Novemba 25,2017 imepewa hadhi ya kuwa hospitali ya rufaa ya Taifa.
Amesema hilo linatokana na kutoa huduma za kitabibu zinazohitaji madaktari bingwa na madaktari bingwa wabobezi, huku ikiwa imesheheni vifaa vya kisasa.
Profesa Kamuhabwa amesema uwepo wa vifaa vya kisasa na madaktari wa kutosha utasaidia hospitali kupunguza kwa kiasi kikubwa wagonjwa kwenda nje ya nchi kupata tiba.
"Hospitali hii itasaidia kuongeza idadi ya madaktari bingwa kwa kuwa imewekewa mazingira rafiki kwa ajili ya kufanya uchunguzi na utafiti ili kuboresha huduma na matibabu," amesema.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo ni mwendelezo wa Kampasi ya Mloganzila ikiwa ni jitihada za Serikali katika kuboresha chuo hicho.
Naibu makamu mkuu wa chuo na mwangalizi wa huduma za hospitali, Profesa Said Abood amesema hospitali hiyo ina mfumo wa Tehama katika kutuma na kupokea sampuli hivyo kurahisisha kasi ya majibu na huduma.
Amesema huduma zote za hospitali zipo katika jengo moja, hivyo hakutakuwa na usumbufu wa mgonjwa kuzunguka kufuata utaratibu ili kupata matibabu.
"Tuna vifaa vya kisasa ambavyo ni vichache nchini au havipo kabisa, mfano kifaa cha kuvunja mawe kwenye figo bila upasuaji," amesema.

No comments:

Post a Comment