Thursday, November 23

Kutoeleweka tozo bandarini maduka yafungwa Kariakoo


Wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa la Kariakoo wamelalamikia gharama za uondoshaji mzigo bandarini kudumaza ufanisi wa shughuli zao.
Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Abdallah Mwinyi amesema soko hilo liko mbioni kupotea endapo jitihada za kulinusuru hazitafanyika.
Alisema hilo linatokana na changamoto wanazokutana nazo Bandari ya Dar es Salaam ambako kuna mlolongo mrefu wa kukamilisha taratibu za kuondosha mzigo unaoingizwa na kuwapo kwa makadirio makubwa ya tozo zinazotakiwa kulipwa jambo linalowakatisha tamaa.
“Mtu unaambiwa utoe Sh60 milioni kutoa kontena moja la bidhaa. Fikiria ukiwa na makontena saba utayatoa kwa kiasi gani na bei uliyoambiwa sasa haitakuwa sawa na utakapoingiza mgizo mwingine hapo baadaye,” alisema Mwinyi.
Mwinyi alisema mzigo wa aina moja unaoingizwa na watu wawili tofauti bandarini hapo hutozwa kiasi kisicholingana. Wapo wanaopata unafuu wakati wengine wanaumia.
Kuepuka ubaguzi huo wa tozo kwa mizigo inayoingi, alisema walipendekeza kuwapo kwa bei elekezi ya utoaji makontena kulingana na bidhaa kurahisisha tathmini lakini utaratibu huo ulitumika kwa muda mfupi kabla ya kuondolewa na mambo yakaendelea kuendeshwa kwa mazoea.
“Ilitolewa kwa sababu hakuna pesa iliyokuwa inaenda mfukoni kwa mtu bali serikalini na kukosekana kwa bei elekezi ni kuruhusu mianya ya rushwa,” alisema Mwinyi.
Kutokana na utaratibu huo usiotenda haki kwa walipakodi hao, alisema biashara imepungua kwa kiasi kikubwa sokoni hapo kwani wafanyabiashara wengi wmeshindwa kuendelea na shughuli zao hivyo kurudisha fremu walizopanga na kuwalazimu wamiliki kubadilisha matumizi ya nyumba zao kuendelea kujiingizia kipato cha kujikimu.
Hali hiyo, alisema inasababisha baadhi ya wafanyabiashara kutoka nchi jirani kuanza kulikimbia soko hilo kutokana na kupungukiwa bidhaa tofauti na ilivyokuwa zamani.
“Wateja waliokuwa wanakuja kutoka nje siku hizi wamepungua, wananunua bidhaa zao Kenya na Uganda ambako bei ni nafuu kuliko sisi,” alisema Mwinyi.
Alisema hali Kufa kwa soko hili hakutawaathiri wafanyabiashara peke yake lakini pia mapato ya Tanzania kwa sababu karibu robo tatu ya mapato yote kila mwezi yanatoka hapa,” alisema Mwinyi.
Alisema madhara ya kudhorota kwa mwenendo wa biashara katika soko hilo ambako kumesababisha maduka kadhaa kufungwa kutokana na uchumi wa wafanyabiashara wengi kuyumba yataenda mbali zaidi ya jamii hiyo.
“Zamani mtu alikuwa anaweza kutafuta fremu ya biashara hata mwaka mzima na asipate, kuna watu walikuwa na stoo mpaka sita lakini hivi sasa wamezirudisha na kubaki na moja. Wenye fremu moja wanahifadhi na mzigo humohumo dukani,” alisema Mwinyi.
Kudhihirisha mabadiliko yaliyopo, alisema kwa sasa mtu anayehitaji hata fremu 15 kwa ajili ya kufungua maduka 15 au stoo 30 anazipata bila hata kutumia dalali. “Nyumba zipo tu. Madalali wa vyumba hawana kazi sasa hivi. Wenye nyumba wenyewe ndio wanapangisha sasa,” alisema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Johnson Minja alisema malalamiko ya wafanyabiashara wanaoingiza mzigo kupitia Bandara ya Dar es Salaam ni ya nchi nzima na kwamba juhudi za kuzishawishi mamlaka husika kuondoa kero hiyo ni endelevu.
“Wengi wanalalamika. Tunaendelea kupiga kelele ili uwepo mfumo wa wazi kwa wote utakaomruhusu mfanyabiashara kufahamu kiasi atakacholipa mzigo wake ukiwasili,” alisema.

No comments:

Post a Comment