Dar es Salaam. Kamati ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi katika mchanga wenye madini unaosafirishwa nje imetoa mapendekezo 21 kwa Serikali, ikiwamo kuichukulia hatua za kisheria kampuni ya Acacia ambayo imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini kinyume na matakwa ya sheria.
Mapendekezo hayo yote yamekubaliwa na Rais Magufuli na ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuanza mara moja kuwachunguza wote waliohusika katika kulitia Taifa kwenye hasara kubwa kutokana na upotevu wa rasilimali ya madini na kuwachukulia hatua za kisheria.
Hata hivyo, Acacia imeeleza kusikitishwa na matokeo ya ripoti ya pili ya kuchunguza makinikia iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli.
Katika maelezo yaliyotolewa jana na kampuni hiyo, ilieleza kusikitishwa na matokeo yaliyotolewa na kamati ya pili na kudai ilijikita katika yaliyobainika kwenye ripoti ya kwanza iliyowasilishwa Mei 24 ambayo waliyakanusha.
“Kamati ilijikita katika kuchunguza sampuli kutoka makontena 44. Katika miaka 20 na takwimu tulizonazo ni vigumu kubainisha uchunguzi huo na iko wazi wameongeza thamani ya makinikia kwa zaidi ya mara 10,” ilieleza taarifa ya Acacia.
Kamati ya pili imeonyesha jinsi Acacia imekuwa haiweki bayana malipo ya kodi na mapato kwa miaka kadhaa ambayo ni mabilioni ya dola za Marekani.
Hata hivyo, kampuni hiyo imekanusha kwa kile ilichoeleza ni tuhuma mpya zilizotolewa.
“Tumekuwa tukifanya biashara zetu kwa kiwango cha juu na kuendesha shughuli zetu kwa kufuata sheria za Tanzania,” ilieleza taarifa yao.
Kamati hiyo iliyoundwa Aprili 10 ilitoa mapendekezo hayo ikiwa ni wiki tatu tangu kamati ya kwanza ilipowasilisha taarifa yake kwa Rais Magufuli, naye akaamua kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wake, Profesa Nehemiah Osoro alibainisha mapendekezo mengine kuwa ni Serikali kudai kodi na mrabaha kutoka kwa kampuni zote za madini ambayo yamekwepwa kulipwa na mrabaha stahiki kwa mujibu wa sheria.
Profesa Osoro alisema kampuni nyingi za madini zimekuwa zikiliibia Taifa kutokana na mikataba mibovu wanayoingia na pia kuendesha shughuli zao kwa kukwepa kodi na kutofuata sheria na taratibu nyingine za madini.
“Kuna tatizo kubwa katika mikataba yetu, lakini pia watendaji wetu wamekuwa hawasimamii masilahi ya Taifa. Naweza kusema wanaangalia masilahi binafsi katika kusimamia madini yanayozalishwa nchini,” alifafanua Profesa Osoro.
Mwenyekiti huyo aliishauri Serikali kuendelea kuzuia usafirishaji wa mchanga wenye madini kwenda nje ya nchi mpaka pale kampuni zinazodaiwa zitakapolipa kodi, mrabaha na tozo stahiki kwa mujibu wa sheria.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na kamati ni Serikali kuanzisha utaratibu utakaowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia (smelter) ili kuondoa upotevu wa mapato na kutengeneza ajira kwa Watanzania.
Kamati hiyo imependekeza Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa mawaziri, wanasheria wakuu wa Serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba na makamishna wa madini pamoja na wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini.
Pia, kamati imependekeza kuwa watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini, kampuni zilizohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia na kampuni za upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.
Profesa Osoro alitaja mapendekezo mengine ya kamati kuwa ni Serikali kufanya uchunguzi kuhusu mwenendo wa watumishi wa idara ya walipakodi wakubwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenye kushughulikia madai ya kodi ambayo mabaraza ya rufani ya kodi na mahakama zimekwishayatolea uamuzi.
Mapendekezo mengine ni Serikali kufuta utaratibu wa kupokea malipo ya mrahaba ya asilimia 90 na kusubiri malipo ya asilimia 10 kulipwa baadaye wakati kampuni za madini zinauza madini na kupewa fedha taslimu kwa mkupuo.
Kamati hiyo imependekeza pia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ifuatilie malipo ya fedha za kigeni yanayotokana na mrahaba kwa mauzo ya madini, jambo ambalo lilikuwa halifanyiki kwenye sekta ya madini kwa muda mrefu.
Profesa Osoro aliongeza kuwa Serikali ianzishe utaratibu wa kulinda maeneo ya migodi na viwanja ndege vilivyopo migodini ili kudhibiti vitendo vya hujuma vinavyoweza kufanywa na kampuni za migodi ikiwamo utoroshaji wa madini.
Kamati hiyo iliyotumia miezi miwili kukamilisha ripoti yake, imependekeza Serikali kupitia wataalamu wabobezi katika majadiliano na mikataba wapitie mikataba yote mikubwa ya uchimbaji madini na kufanya majadiliano na kampuni za madini ili kuondoa misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija kwa Taifa na badala yake kuweka masharti yenye tija kwa pande zote mbili kwa kuzingatia masilahi ya nchi.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na kamati yalitaka mabadiliko ya sheria ya madini ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha adhabu kwa makosa ya ukiukwaji wa sheria ya madini na sheria ya kodi.
Mabadiliko mengine ni sheria kuweka kiwango cha asilimia za hisa ambazo zitamilikiwa na Serikali; kutamka bayana kuwa madini ni mali asili ya Watanzania na iwekwe chini ya udhamini wa Rais na mikataba yote ya uchimbaji wa madini isiwe ya siri na iridhiwe na Bunge.
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema sheria pia iondoe mamlaka ya waziri wa Nishati na Madini, kamishna wa madini na maofisa wa madini na iweke masharti kwa waombaji leseni ya uchimbaji kuonyesha mchanganuo wa mafunzo kwa wazawa.
Mabadiliko mengine yaliyopendekezwa na kamati ni sheria ielekeze kampuni za madini kuweka fedha zinazotokana na mauzo ya madini katika benki zilizopo nchini.
“Serikali iunde chombo cha kusimamia biashara ya usafirishaji bidhaa nje ya nchi kupitia bandari kama lilivyokuwa shirika la Nasaco ili kudhibiti biashara haramu na kuondoa mianya ya ukwepaji kodi,” alibainisha Profesa Osoro.
Pia, kamati imependekeza kuwa Serikali ipitie na kufanya marekebisho au kufuta na kubadili kabisa sheria ya madini na sheria za kodi ili kuondoa pamoja mambo mengine masharti yote yasikuwa na manufaa kwa Taifa ikiwa ni pamoja na yaliyomo kwenye kifungu thabiti.
Vilevile kamati hiyo imemtaka kamishna wa madini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kampuni za madini ili kuhakikisha uzingatiaji wa ukiukwaji wa sheria na kuchukua hatua.
No comments:
Post a Comment