Friday, October 9

‘Obama siyo rais mweusi kamili Marekani’



Washington, Marekani. Mmoja ya watu wanajulikana kwa utajiri mkubwa wa vyombo vya habari duniani amesema kuwa Marekani haijapata rais anayewakilisha uhalisia wa kweli juu ya jamii ya watu weusi.
Tajiri huyo Rupert Murdoch aliandika ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema kuwa Rais Barack Obama siyo ‘rais mweusi kamili’.
Tajiri huyo hakuishia hapo bali alikwenda mbali zaidi kumsifia mmoja wa wanaotaka kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi ujao kupitia chama cha Republican.
Alimmwagia sifa mgombea Ben Carson akisema kuwa :”Ben na Candy Carson wazuri sana. Itakuwaje tukiwa na rais mweusi kamili atakayeangazia kikamilifu masuala ya rangi? Na mengine mengi”.
Alipendekeza pia watu wasome makala iliyo kwenye jarida la New York Magazine inayozungumzia “kutamanishwa kwa makundi ya wachache” na uongozi wa Rais Obama.
Murdoch mwenye umri wa miaka 84, ndiye mwanzilishi wa himaya ya mashirika ya habari ya News Corporation iliyokita mizizi maeneo mengi duniani.
Kampuni yake inamiliki Fox News Channel, The New York Post na The Wall Street Journal nchini Marekani na magazeti ya Times nchini Uingereza.
Hivyo ni baadhi tu ya vyombo vya habari anavyomiliki tajiri huyo mkubwa duniani.
Yeye ameorodheshwa kuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi zaidi duniani.
Mgombea huyo wa urais mwenye umri wa miaka 63 ni mtaalamu wa upasuaji wa mfumo wa neva na mmoja wa wagombea 15 wanaopigania tiketi ya chama cha Republican kuwana urais wa Marekani 2016.
Siku chache zilizopita, aliandika kwenye Twitter: “Kotekote, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanamtambua Ben Carson. Lakini umma unafahamu na kupendezwa na upole na unyenyekevu.”
Hata hivyo, Rais Obama, katika uongozi wake, amekuwa mwangalifu kuhusu masuala ya ubaguzi wa rangi na asili.
Carson aliibua utata mwezi uliopita baada ya kusema kuwa Mwislamu hafai kuwania urais Marekani kwa vile Uislamu unakinzana na katiba ya Marekani.

No comments:

Post a Comment