Monday, June 5

Wafanyakazi wa Manji walipa faini kuikwepa jela



Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana iliwahukumu wafanyakazi 16 wa Kampuni ya Quality Group Ltd, inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Yusuph Manji kulipa faini ya Shilingi laki tano katika kila kosa linalowakabili ama kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha alisema mshtakiwa wa kwanza hadi wa 14 wanakabiliwa na mashtaka matatu hivyo katika kila kosa, kila mmoja atatoa jumla ya faini ya Sh1.5 milioni.
Iwapo wangeshindwa, kila mshtakiwa angetumikia kifungo cha miaka mitatu jela katika kila kosa hivyo kufanya watumikie kifungo cha miaka tisa jela.
Kwa upande wa washtakiwa 15 na 16 ambao ni Meneja mradi Jose Kiran na Katibu wake, Prakash Bhatt walihukumiwa kulipa faini ya Shilingi laki tano au kwenda jela miaka mitatu.
Kiran na Bhatt, wao walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za kukiuka amri ya Ofisa Uhamiaji na kujaribu kutoroka. Hata hivyo, washtakiwa hao wamekwepa kifungo kwa kulipa faini hiyo.
Kiran na Bhatt wanadaiwa kuwa Februari 20, 2017, wakiwa ni waajiriwa wa Quality Group Ltd, walimzuia Ofisa wa Uhamiaji kufanya kazi zake na kwamba, walikataa kuripoti katika ofisi za Uhamiaji zilizopo jijini Dar es Salaam kwa kujaribu kutoroka nchini kwa kupitia mpaka wa Horohoro.
Washtakiwa 14 ambao ni washauri, Jagadish Mamidu (29), Niladri Maiti (41), Divakar Rajasekaran (37), Mhasibu, Mohammad Taher Shaikh (44), mshauri Bijenda Kumar (43) na mshauri Prasoon Kumar Mallik(46).
Wengine ni mshauri Nipun Dinbadhu Bhatt (32), Meneja Msaidizi, Pintu Kumar (28), mshauri Anuj Agarwal (46), mshauri Varun Boloor (34), mshauri Arun Kumar Kateel (46), mshauri Avinash Chandratiwari (33) na mshauri Vikram Sankhala (50), wamefanikiwa kulipa faini na kukwepa vifungo hivyo na waliambiwa ili waweze kuendelea kuishi Tanzania lazima wafuate sheria za nchi.
Wakili wa Serikali wa washtakiwa hao, Hudson Ndusyepo kabla ya hukumu kutolewa, aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa wa kwanza hadi wa 14 hawakuwa na nia mbaya ya kutenda makosa hayo.
Alidai kuwa walikutana na Ofisa wa Uhamiaji wakamwambia wanahitaji kuongeza muda wa viza za kufanya kazi na wakamkabidhi hati zao za kusafiria na baadae aliwarejeshea zikiwa na viza ndani.
Aliendelea kudai kuwa, wao waliamini viza hizo zilipatikana kwa halali na malipo yalifanyika na fedha kuingia serikalini kupitia mpaka wa Tunduma na risiti walipata.
Alidai baada ya kukamatwa iligundulika zilipatikana kinyume cha sheria.
Alikiri hilo ni kosa lao la kwanza na akaomba Mahakama iwasamehe, wapewe adhabu ndogo na nafasi nyingine ya kuwapo nchini.
Mwendesha Mashtaka wa Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma alidai washtakiwa waliingia nchini mwishoni mwa 2016 na wakapewa viza za miezi mitatu za kufanya kazi. 


No comments:

Post a Comment