Tuesday, December 5

Mhasibu wa Takukuru akwama mahakamani


Dar es Salaam. Mahakama imegoma kumfutia shtaka la utakatishaji fedha mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai.
Gugai anayedaiwa kuwa na utajiri wa kutisha usiolingana na kipato chake, aliiomba mahakama kumfutia shtaka hilo na kujikuta likitupiliwa mbali.
Gugai na wenzake watatu, George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera wanakabiliwa na mashtaka hayo ambayo hayana dhamana pamoja na mengine ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Novemba 16, na kusomewa mashtaka 43 yakiwamo 20 ya kutakatisha fedha.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, kupitia kwa jopo la mawakili wao lilioongozwa na Alex Mgongolwa waliiomba mahakama kuwafutia mashtaka ya utakatishaji fedha, pamoja na mambo mengine wakidai hayajakidhi vigezo vya kisheria.
Maombi na hoja za mawakili wa washtakiwa hao, zilipingwa vikali na upande wa mashtaka ulioongozwa na Simon Wankyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliiahirisha hadi jana kwa uamuzi wa ama kuyafuta mashtaka hayo au la.
Hata hivyo, hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba anayesikiliza kesi hiyo katika uamuzi wake alitupilia mbali maombi na hoja za mawakili wa washtakiwa hao.
Akisoma uamuzi wake, Simba alitupilia mbali maombi na hoja hizo akisema hazina msingi wa kisheria na hati ya mashtaka ipo sawa haina kasoro za kisheria.
Baada ya kusoma uamuzi huo, wakili wa Serikali mkuu, Vitalis Peter aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Simba aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 18, litakapotajwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kueleza hatua ya upelelezi ulipofikia.
Awali, akiwasilisha maombi ya kufutwa kwa mashtaka hayo, Mgongolwa alidai mashtaka hayo hayakidhi vigezo vya kisheria vilivyotajwa katika sheria ya utakatishaji fedha.
Alidai maelezo ya makosa hayo hayaelezi kosa la utakatishaji fedha na kwamba, lazima makosa hayo yaonyeshe uhalisia ili kumwezesha mshtakiwa kutengeneza utetezi wake.
Aliendelea kuwa msingi wa mashtaka ya utakatishaji wa fedha ni fedha, lakini katika mashtaka yote hayo ya utakatishaji hakuna sehemu iliyotajwa fedha na kwamba kinachoonekana ni udanganyifu wa kiwango cha mali anazomiliki mshtakiwa.
Maombi hayo yalipingwa na upande wa mashtaka ambao waliiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo, kwa kuwa hayana msingi kisheria.
Gugai kwa upande wake anakabiliwa na shtaka la kumiliki mali ambazo hazina maelezo.
Anadaiwa kuwa kati ya Januari 2005 na Desemba 2015, katika mkoa wa Dar es Salaam, akiwa ofisa wa umma aliyeajiriwa na Takukuru, alikutwa anamiliki mali zenye thamani ya Sh. 3,634,961,105.02 ambazo haziendani na kipato chake cha sasa wala cha nyuma. 

No comments:

Post a Comment