Tuesday, December 5

Lukuvi amesema kodi inapaswa kulipwa kila mwezi


Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewaonya wamiliki wa nyumba wanaopangisha na kudai kodi ya mwaka mzima.
Akizungumza leo Jumanne Desemba 5,2017 akifungua jengo la makao makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam na sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere, amesema kodi ya nyumba inatakiwa kutozwa kila mwezi.
"Mpangaji anatakiwa kulipa kodi kila mwezi labda atake mwenyewe kulipa kwa miezi zaidi ya mmoja," amesema.
Lukuvi amesema hata NHC inatoza kodi kwa wateja wake kwa mwezi. "Acheni tamaa wenye nyumba chukueni kodi kila mwezi," amesema.
Amesema kuna vijana wanaoajiriwa wanashindwa kukaa jirani na mjini kutokana na kutozwa kodi ya nyumba kwa mwaka.
Mbali ya kauli hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula Novemba 17,2017 akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Halima Bulembo bungeni alisema Serikali iko katika mchakato wa maandalizi ya muswada wa sheria ambayo itasimamia sekta ya nyumba, hivyo kuondoa changamoto ya wamiliki kudai kodi ya pango ya zaidi ya mwezi mmoja.
Halima katika swali lake alisema vijana ambao ni kati ya asilimia 56 na 60 nchini, wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya kodi ambayo hutakiwa kulipa kwa kipindi cha mwaka mmoja au miezi sita.
Akijibu swali hilo, Mabula alisema Serikali imeliona tatizo hilo na ipo katika mchakato wa kuandaa muswada wa sheria utakaosimamia sekta hiyo.
Mabula alisema baada ya kukamilika kwa sheria ambayo itaunda chombo cha kusimamia sekta hiyo, wapangaji hawatalipa kodi ya mwaka wala miezi sita tena bali watalipa kwa mwezi na kuweka amana ya miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment