Tuesday, December 5

Mtoto aliyezaliwa ubongo ukiwa nje afanyiwa upasuaji


Dar es Salaam. Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) imefanya upasuaji mkubwa wa kurudisha ubongo wa mtoto mwenye umri wa miezi minne aliyezaliwa ukiwa kwenye mfuko nje ya kichwa.
Upasuaji huo uliofanyika kwa mafanikio ni wa kwanza nchini wa kurudisha ubongo uliokuwa kwenye mfuko nje ya kichwa (occipital encephalocele).
Imeelezwa upasuaji huo uliwahusisha madaktari bingwa kutoka nchini kwa gharama ya Sh4 milioni badala ya kati ya Sh25 milioni na Sh30 milioni kama ungefanika nje ya nchi.
Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo wa Moi, Nicephorus Rutasibwa amesema leo Jumanne Desemba 5,2017 kuwa upasuaji huo umefanywa kwa zaidi ya saa nne.
Dk Rutasibwa amesema upasuaji umefanyika baada ya utafiti wa miezi miwili kujua namna bora ya kumsaidia mtoto huyo ili kuokoa maisha yake.
“Tathmini ya uchunguzi ilionyesha uvimbe au mfuko ulikuwa umefunika sehemu kubwa ya ubongo na mishipa ya damu inayolisha ubongo, hivyo kuhatarisha maisha yake. Upasuaji ulihitaji umakini wa hali ya juu na vifaa vya kisasa,” amesema.
Dk Rutasibwa amesema upasuaji huo ulifanywa bila kuathiri utendaji kazi wa ubongo ambao wakati wote wa upasuaji ulikuwa unafanya kazi.
Hata hivyo, amesema walikabiliana na changamoto wakati wa maandalizi ya upasuaji ya upatikanaji wa mishipa ya damu ya mtoto kwa kuwa ilikuwa midogo.
“Baada ya upasuaji mtoto aliendelea vizuri na aliweza kunyonya, tangu alipozaliwa ilikuwa vigumu kumbeba lakini sasa mama anaweza kumbeba mwanaye. Mtoto amepata nafasi ya kuendelea na maisha,” amesema.
Mama wa mtoto huyo ambaye hakupenda kutajwa jina amesema awali alikata tamaa ya mwanaye kupona kutokana na uvimbe uliokuwa ukimuelemea.
“Nawashukuru madaktari bingwa kwa kufanikishwa upasuaji huu, nilishakata tamaa na sikujua kama leo ningeweza kumnyonyesha mwanangu akiwa mzima,” amesema.

No comments:

Post a Comment