Tuesday, December 5

Kabudi ataka kutumiwa wasaidizi wa kisheria

       Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa
       Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi       
Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ametoa wito kwa jamii kuwatumia wasaidizi wa sheria ili kupata ushauri kwa kuwa hivi sasa wanatambulika kisheria.
Akifungua maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jana, Profesa Kabudi alisema kuwatumia wasaidizi wa sheria kutapunguza muda unaotumika mahakamani.
“Nitoe rai kwa wananchi kutumia fursa hii mliyopewa na sheria kupata msaada wa kisheria kupitia wananchi wenzenu waliojitolea kwa moyo kutoa ushauri,” alisema katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.
Alisema kutokana na kada hiyo kuwa ngeni nchini, watu wengi hasa wanasheria na mawakili wamekuwa na mtizamo hasi na hata kufikia kuwapiga vita.
Profesa Kabudi alisema kwa kutambua umuhimu wa kusogeza huduma karibu na wananchi, sheria imeweka wasajili wasaidizi katika ngazi za halmashauri ambao watakuwa wakishirikiana na wasaidizi wa kisheria maeneo hayo.
Naye mwakilishi wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), John Seka alisema jukumu la chama hicho ni kutoa msaada wa kisheria kwa jamii.
Aliwataka wananchi kuzitumia ofisi za chama hicho zilizopo mikoa mbalimbali nchini kupata msaada wa kisheria. “Tumekuwa tukitoa msaada wa kisheria ikiwamo kutoa mawakili ili kuwasaidia wananchi wasio na uwezo,” alisema.     

No comments:

Post a Comment