Tuesday, December 5

Tani tatu za sangara zanaswa zikisafirishwa kwa magendo


Ngara: Tani tatu za samaki aina ya sangara zenye thamani ya Sh20.8 milioni zimekamatwa zikisafirishwa kwa magendo wilayani Ngara mkoani Kagera.
Samaki hao waliovuliwa katika Ziwa Victoria wilayani Muleba wamekamatwa jana Jumatatu Desemba 4,2017 jioni katika Kijiji cha Murusagamba wilayani Ngara wakisafirishwa kwa gari kwenda nchini Burundi.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Michael Mntenjele amesema leo Jumanne Desemba 5,2017 kuwa samaki hao walivuliwa kinyume cha sheria na walikuwa wakiwasafirisha bila vibali.
Mntenjele amesema samaki hao walikuwa kwenye gari aina ya Mitsubishi likiendeshwa na Ayubu Sanga mkazi wa Dar es Salaam    anayefanya shughuli zake Kata ya Izigo wilayani Muleba.
Amesema dereva huyo akiwa na bosi wake walikatwa wakisafirisha mzigo huo kwa magendo. Alisema bosi huyo alitoroshwa wakati wakihojiwa na polisi kwa msaada wa baadhi ya maofisa uvuvi.
Mkuu wa wilaya amesema dereva na ofisa uvuvi wa kata ya Murusagamba wanashikiliwa na vyombo vya dola kwa mahojiano.
Ofisa Uvuvi Mkoa wa Kagera, Efraz Mkama amesema samaki hao wana uzito wa kuanzia nusu kilo hadi kilo 30 na urefu wa kati ya sentimita 25 na sentimita 90 .
Amesema watuhumiwa wametenda kosa la kusafirisha samaki ambao hawajachakatwa kwa mujibu wa sheria ya uvuvi.
“Mzigo haukuwa na nyaraka, ulisafirishwa usiku na kukiuka utaratibu kuanzia maeneo ya mwaloni katika kata na vijiji mbalimbali wilayani Muleba. Tutafuatilia huko alikotokea,” amesema Mkama.

No comments:

Post a Comment