Tuesday, December 5

WAZIRI AAGIZA SONGAS KUWASHA UMEME LEO

WAZIRI wa Nishati, Dk.Medard Kalemani ameuagiza uongozi wa kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Songas kuhakikisha kuanzia leo wanawasha umeme   kumaliza tatizo lililopo.
Aliyasema hayo jana alipokutana na viongozi wa kampuni hiyo   Dar es Salaam, baada ya kutokea hitilafu katika mitambo yao iliyosababisha watumiaji waliounganishwa na gridi ya taifa kukosa umeme.
Alihoji sababu za kampuni hiyo kuchukua muda mrefu kufanya marekebisho katika mitambo ya kuzalisha umeme  hitilafu inapotokea,ikilinganishwa na kampuni nyingine.
Akijibu swali hilo, Meneja wa Uzalishaji wa Kampuni hiyo, Tvsk Kao alisema kwa kawaida muda wa kurejesha   uzalishaji wa umeme ni saa nane, lakini kutokana itilafu isiyo ya kawaidia iliwachukua muda mrefu kufanya matengenezo hayo.
“Tatizo lililojitokeza halijawahi kutokea, ilikuwa changamoto kubwa, tunaamini ifikapo saa 11 jioni (leo), tatizo litakuwa limetatuliwa na kurudisha upatikanaji wa umeme katika hali ya kawaida.
Alisema kampuni hiyo  inaelewa umuhimu wa nishati katika kukuza uchumi hivyo ingependa mitambo yote ya kuzalisha umeme ifanye kazi.
“Tutahakikisha  kuwa na vifaa  vya ziada vya kufunga katika mitambo   tatizo linapotokea,” alisema Tvsk.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,Dk. Hamisi Mwinyimvua, aliwataka wataalamu hao kuhakikisha tatizo linatafutiwa suluhisho mapema na ahadi walizotoa zinatekelezwa kwa wakati.

No comments:

Post a Comment