Monday, July 20

Kambi ya Lowassa sasa rasmi Chadema

Sasa ni rasmi kwamba kambi ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Edward Lowassa imeamua kuachana na chama hicho baada ya madiwani 18 kutangaza kuhamia Chadema, huku mratibu wa wanachama wanaomuunga mkono kada huyo wa CCM kuamua kujiunga na vyama vinavyounda Ukawa.
Matukio hayo yametokea ikiwa ni mwendelezo wa wimbi la wanachama wa CCM kutangaza kuhamia vyama vya upinzani, hasa Chadema baada ya madiwani tisa pamoja na wanafunzi 28 wa vyuo vikuu kutangaza kuhamia Chadema ambayo ni chama kikuu cha upinzani.
Wote wameeleza sababu ya kuhama CCM ni kutokubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu wa kukata jina la Lowassa wakati wa mchujo wa wagombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala mwishoni mwa wiki iliyoishia Julai 12.
Akizungumzia kuhama kwa madiwani hao, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hawezi kujibu lolote kwa madai kuwa hana taarifa rasmi na kutaka waulizwe viongozi wa chama wa mkoa.
“Madiwani hao siwajui na sina taarifa rasmi ninaweza kutoa maoni yangu, lakini kesho ikabainika kuwa hazikuwa taarifa rasmi juu ya kuhama kwao?” alihoji.
Nape alisisitiza kuwa hakuna kanuni zilizokiukwa wakati wa kumsaka mgombea urais kama wanachama hao wanavyodai.
Nape pia alizungumzia kitendo cha mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru cha kuilaumu Kamati ya Maadili na Kamati Kuu akisema kinaweza kukigawa chama hicho.
“Kama wakiendelea CCM kitaitisha mkutano na kuwajibu. Lakini kwa sasa tunawataka tu wawasilishe malalamiko yao sehemu husika maana huo utaratibu wanaujua,” alisema
Jana, mkoani Arusha, madiwani hao, walioongozwa na viongozi wa kijadi wa jamii ya Kimasai wanaofahamika kwa jina la Malaigwanan, walipokewa jana na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema kwenye hafla fupi iliyofanyika mjini Monduli.
Mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Onesmo ole Nangole alisema chama chake hakina uwezo wa kuzuia mtu kuondoka CCM.
“Tumepata taarifa za kuondoka madiwani na viongozi wetu na kuchomwa kadi lakini hatuwezi kuzuia uamuzi wa watu kufanya wanachotaka,” alisema.
Alisema tayari wameanza kufuatilia kinachoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali mkoani Arusha ili kujua athari za matukio hayo kwa CCM.
Viongozi hao waliohamia Chadema ni 10 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ina kata 20. Awali, halmashauri hiyo ilikuwa na kata 15 kabla nyingine tano kuongezwa mwaka huu.
Akisoma tamko la kujiengua CCM na kuhamia Chadema, mwenyekiti wa madiwani hao, Julius Kalanga ambaye ni diwani wa Kata ya Lepurko, alisema hatua hiyo imetokana na kuchoshwa na vitendo alivyoviita vya hila, uonevu, ubaguzi na unyanyasaji vinavyofanywa ndani ya chama hicho tawala.
“Tumetafakari usalama wetu ndani ya CCM kwa umoja wetu tumeshindwa kuuona… CCM iliyokuwa ikiongozwa kwa Katiba, kanuni na miongozo hivi sasa inaongozwa kwa matakwa ya familia chache kwa jinsi watakavyoona inawapendeza wao,” alisema Kalanga.
Alisema mchakato wa CCM wa kumpata mgombea urais uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma ni miongoni mwa ishara za wazi za chama hicho kukosa maadili kuanzia kwenye vikao vya Kamati ya Maadili alichodai kilikosa maadili hadi kukatwa kwa majina ya wagombea akiwemo Lowassa.
Kalanga, mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Lowassa katika shughuli zake za kisiasa, alisema wana-CCM wamepoteza haki na uwezo wa kuchagua viongozi wanaowataka kutokana na kunyimwa uwezo wa kufikiri kwa sababu uamuzi hauzingatii utaratibu wa vikao.
“Tunakataa kuwa watumwa katika misingi hii na ndiyo maana leo tunaondoka sisi viongozi wote na kuamua kujiunga Chadema,” alisema Kalanga.
“Tunamwomba Mheshimiwa Lowassa aungane nasi katika safari yetu hii inayoendelea. Awe na moyo wa ujasiri na kufanya uamuzi mgumu maana hakuna busara nyingine inayoweza kutumika zaidi ya kuondoka CCM,” alisisitiza Kalanga.
Diwani wa Kata ya Mererani, Edward Lenana ambaye ni mmoja wa waliotimkia Chadema alisema yeye na wenzake watazunguka kwenye majimbo yote ya jamii ya Wamaasai kuhamasisha jamii hiyo kutochagua wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
Akizungumza baada ya kuwakabidhi viongozi hao kadi za Chadema, Lema aliwataka kuingia kazini kukijenga chama chao kipya ili kufanikisha ushindi katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 25.
“Ndani ya Chadema hakuna mheshimiwa, kiongozi wala mwanachama mdogo. Wote ni makamanda wanaopaswa kupambana dhidi ya uovu na ukandamizaji. Kuanzia leo ninyi nyote ni makamanda. Hakuna kamanda mgeni wala mwenyeji, bali sote ni wapiganaji wenye lengo moja la ushindi mwezi Oktoba,” alisema Lema.
Mwenyekiti wa Chadema wa mkoa, Amani Golugwa aliwataka wanachama hao wapya kujifunza na kuishi katika misingi ya uadilifu, unyenyekevu na utumishi kwa umma aliosema ndiyo miongoni mwa imani kuu ya Chadema.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na wa viti maalumu, Joyce Mukya waliwahakikishia viongozi hao fursa ya kuendelea kuwatumikia wananchi katika kata zao wakiwa Chadema kwa sababu wapigakura ni wale wale, bali kilichobadilika na jukwaa la kusimamia kuwatumikia.
Wengine Dar wajiengua
Jijini Dar es Salaam, wanachama waliokuwa kundi la 4U Movement linalomuunga mkono Lowassa, walitangaza kuihama CCM chama hicho na kujiunga na Ukawa, kutokana na kile walichodai kuchukizwa na mchakato wa kumpata mgombea urais.
Mratibu wa wanachama hao, Hemed Ally alisema wamefikia uamuzi wa kujiunga na Ukawa inayoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF, kwa ajili ya “kutafuta mabadiliko nje ya CCM”, kutokana na kushindwa kuyapata wakiwa ndani ya chama hicho tawala.
Wadai njama zimewatoa
Wanachama hao wanaodai wana wafuasi wapatao milioni 10 ambao wengi ni vijana, walitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, huku wakisisitiza kuwa kulikuwa na njama za kuhakikisha kuwa Lowassa anaenguliwa huku wakinukuu maneno yaliyosemwa na kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye naye alikilalamikia chama hicho kutomtendea haki Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli.
Makada wa CCM waliopitishwa kuwania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 walikuwa 38, huku Dk John Magufuli akiibuka kidedea.
Waliongia tano bora walikuwa Dk Magufuli, Bernard Membe, Balozi Amina Salum Ali, Asha-Rose Migiro na January Makamba.
Wanachama hao walisema kwa pamoja wamekubaliana kutumia kura zao kuking’oa CCM madarakani katika uchaguzi wa mwaka huu.
Ally alisema kulikuwepo na ukiukwaji mkubwa wa kanuni katika uteuzi, jambo linalowafanya waamini kuwa Kamati ya Maadili ilikosa maadili.
“Tunaomba ieleweke wazi hatuna nia ya kumpinga Magufuli ila upatikanaji wake ulijaa maovu hivyo tumeamua hatutaiunga mkono CCM na kura zetu tutazipeleka upinzani.
“Lowassa hakutendewa haki na kila mmoja anatambua hilo, sisi tumeamua kutoka kwa sababu tulikuwa tunamuunga mkono yeye tukiamini atatuletea mabadiliko lakini kwa mtindo huu tunaona kiu yetu haiwezi kutimizwa ndani ya CCM,” alisema Ally.
Alivitaka vyama vya upinzani kuunganisha nguvu kwa pamoja na kushirikiana nao kuindoa CCM kwa demokrasia ya upigaji kura. Kwa mujibu wa Ally, wafuasi hao wamegawanyika katika makundi kadhaa ambayo ni 4 U Movement, Lowassa for Presidency, Team Lowassa, Umoja wa Waendesha Bodaboda na Shirikisho la Walimu.
“Upinzani ukijipanga vizuri tunaweza kuindoa CCM madarakani ikizingatiwa kura zetu zote tutazielekeza upande huo kumuunga mkono mgombea yoyote watakayemsimamisha,” alisema.
Katibu wa Shirikisho la Walimu Wafuasi wa Lowassa, Maulid Nkungu alisema kama vijana hawana sababu ya kukubaliana na utaratibu ambao hata wakongwe wa chama hicho hawajaridhishwa nao.
“Tuliipenda sana CCM, lakini imeonyesha kutopenda mabadiliko hilo ndilo linalotuondoa tumechoka kuonewa tunataka kulinda heshima na kuwakomboa wanaonyanyaswa,” alisema.

No comments:

Post a Comment