Kundi la Islamic State (IS) limeripoti katika mtandao wake wa propaganda wa Amaq kwamba linahusika na shambulio jijini Las Vegas, Marekani lililogharimu maisha ya watu 59 na wengine 527 kujeruhiwa.
Hata hivyo makachero wa Marekani wametupilia mbali madai hayo na wanaendelea na uchunguzi kubaini lengo la shambulio hilo lililofanywa dhidi ya watu waliokuwa wakishiriki tamasha la muziki kwenye eneo la wazi.
Maofisa waandamizi wa serikali ya Marekani wamesema hakukuwa na kitu chochote chenye uhusiano kati ya mshambuliaji wa Las Vegas na kundi lolote la kigaidi. Vilevile shirika la upelelezi la FBI limethibitisha kwa upande wake kwamba hakuna ‘mpaka sasa’ uhusiano na kundi la kijihadi
Pamoja na FBI kukanusha, mtandao huo wa IS umesema mshambuliaji huyo ni mfuasi wao ambaye ‘abadili dini kuwa mwislamu miezi michache iliyopita’. Amaq limemtaja Paddock kuwa mpiganaji wake mpya aliyepewa jina la kivita la ‘Abu Abd el-Bir al-Amriki’.
Polisi wamethibitisha kwamba baada ya Paddock kutekeleza shambulizi hilo alijiua kabla ya polisi kumkaribia.
Polisi walipofanya ukaguzi wa kina nyumbani kwake karibu na Mesquite, Nevada walikuta bunduki 19, vilipuzi, maelfu ya risasi na vifaa vya kielektroniki.
Pia, katika chumba cha hoteli ya Mandalay Bay Resort and Casino ambamo Paddock alikuwa anaishi, polisi walikuta silaha 23, zikiwemo ‘handgun’ moja na ‘rifles’. Polisi walikuta ndani ya gari lake kilo kadhaa za ‘ammonium nitrate’ dawa inayotumika kutengenezea milipuko.
No comments:
Post a Comment