Tuesday, October 3

Mbunge ataka mahakama imzuie Raila kususia uchaguzi


Nairobi, Kenya. Mbunge wa Jimbo la Pokot Kusini David Pkosing amefungua kesi Mahakama Kuu akitaka itoa amri ya kumshinikiza mgombea urais kupitia muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga kushiriki uchaguzi wa marudioOktoba 26 bila kukosa.
Katika kesi hiyo Pkosing anamtaka Raila atekeleze uamuzi wa Mahakama ya Juu iliyoamuru uchaguzi wa marudio na kwamba vitisho vya kutaka kususia uchaguzi huo ikiwa masharti kadhaa hayajatimizwa ni ukiukwaji wa sheria.
Kupitia kwa wakili wake Kibe Mungai, mbunge huyo amesema ikiwa Raila na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka watajitoa utatokea mgogoro wa kikatiba ambao unaweza kuitumbukiza nchi katika sintofahamu.
Mbunge huyo anataka mahakama itoe amri kwamba hatua ya Odinga, Musyoka au kiongozi yeyote wa Nasa kutoshiriki uchaguzi wa marudio ni kitendo cha uhaini na lazima wawajibike.
Katika hatua nyingine, Nasa wamemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) katika muda was aa 72 kumfungulia mashtaka wakala wa chama cha Jubilee Davies Chirchir baada ya kumtuhumu kwa makossa kadhaa yanayohusiana na uchaguzi.
Kupitia kwa mwanasheria wake Anthony Oluoch, Nasa imemlalamikia kwa makossa manne Chirchir, ambaye alikuwa wakala mkuu wa Uhuru Kenyatta katika kituo cha kujumlishia matokeo ya Bomas of Kenya.
Vilevile, Muungano huo wa Nasa unataka wafanyakazi sita wa kampuni ya Safaricom wanaodaiwa kuwa waliingilia uchaguzi wa rais wa Agosti 8 washtakiwe.
Muungano huo umesema kwamba ikiwa DPP Keriako Tobiko atashindwa kuchukua hatua katika muda wa saa 72, wataandaa mashtaka kivyao dhidi ya Chirchir kwa kuzingatia kifungu cha 28 cha Sheria ya Ofisi ya DPP ambayo inaruhusu watu binafsi kuendesha mashtaka.
Alipoulizwa Chirchir kuhusu tuhuma anazorushiwa na Nasa alisema hakutenda kosa lolote kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) ilimpa haki ya uwakala kama mawakala wengine. “Ikiwa wanataka kumshtaki basi wafanye hivyo hata kwa mawakala wao,” amesema Chirchir.
Hii itakuwa mara ya pili Nasa wanampa DPP sharti la kuwafungulia mashtaka watu binafsi inaodai waliingilia uchaguzi wa Agosti 8 ambao ulifutwa na Mahakama ya Juu. Mara ya kwanza ilikuwa Septemba 22 Nasa walimpompa Tobiko saa 72 kuwashtaki maofisa wa IEBC iliodai walivuruga uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment