TIMU ya Taifa Tanzania Taifa Stars wameingia kambini jana kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi kuanzia saa 10 alasiri katika dimba la Uhuru.
Stars inakutana na Malawi ikiwa ni mara ya pili kwa mwaka baada ya kuvaana nao June 25 mwaka huu katika michuano ya COSAFA yaliyofanyika nchini Afrika Kusini na kufanikiwa kupata wa ushindi wa goli 2-0.
Timu hiyo chini ya Salum Mayanga inafanya mazoezi katika Uwanja wa Boko Veterani nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na tayari Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta tayari ametua nchini kuungana na nyota wengine wa Tanzania katika mazoezi ya pamoja.
Kocha Mayanga mapema wiki iliyoisha aliita kikosi kitakachounda Taifa Stars kwa ajili ya kuvaana na Malawi siku ya Jumamosi na akiwajumuisha nyota mbalimbali na akimrudisha Ibrahim Ajib baada ya kutokumuita kwa muda mrefu sambamba na golikipa Peter Manyika.
Mayanga aliteuliwa Januari 4, mwaka huu ameita nyota watano wanacheza soka nje ya mipaka ya Tanzania akiwamo nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Ally Samatta.
Kikosi hicho kina makipa Aishi Manula (Simba SC), Ramadhani Kabwili (Yanga) na Peter Manyika (Singida United).Mabekii ni Gardiel Michael (Yanga), Boniphace Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Yanga), Salim Mbonde (Simba SC), Erasto Nyoni (Simba SC) na Adeyum Ahmed (Kagera Sugar).
Viungo ni Himid Mao ambaye pia ni Nahodha Msaidizi (Azam FC), Hamisi Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Muzamil Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Yanga), Simon Msuva (Difaa El Jadidah/Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Morel Orgenes (FC Famalicao/Ureno).
Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Ibrahim Hajib (Yanga) na Mbaraka Yussuph (Azam FC).
Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Ame Ninje (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
Shirkisho la mpira wa miguu nchini wamewataka watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kuja kuishangilia timu ya Taifa kwa kujenga dhana ya mchezaji wa 12 uwanjani wakati wale 11 akiwamo Msuva, Ajib, Mbaraka wakileta faraja ya mabao.
No comments:
Post a Comment