Tuesday, October 3

Mwalimu Nyerere watafuta mgeni rasmi mwingine

Mkuu wa chuo cha MNMA, Profesa Shadrack
Mkuu wa chuo cha MNMA, Profesa Shadrack Mwalalila 
Dar es Salaam. Baada ya Rais John Magufuli kueleza hatahudhuria kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, uongozi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) unatafuta mgeni rasmi mwingine atakayelifungua.
Chuo hicho ambacho kimeandaa kongamano hilo kimekuwa kikitangaza kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii kwamba kongamano hilo litafunguliwa na Rais Magufuli Oktoba 11.
Hata hivyo, Oktoba Mosi, Ikulu ilitoa taarifa kwamba Rais Magufuli hatahudhuria kongamano hilo kwa sababu ana majukumu mengine kulingana na ratiba yake ya kazi.
Ikulu ilielekeza taasisi za umma na zisizo za umma zinazomualika Rais katika shughuli zao kutotangaza ushiriki wake hadi zipate uthibitisho kuwa atahudhuria.
Akizungumza leo Jumanne, Mkuu wa chuo cha MNMA, Profesa Shadrack Mwalalila amesema bado hawajapata mgeni rasmi atakayefungua kongamano hilo.
“Bado hatujapata mgeni rasmi lakini kesho  tunaweza kumpata na tutawatangazia,” amesema.
Kwa mujibu wa tangazo la chuo hicho, mada kuu ya kongamano hilo ni mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika uchumi wa viwanda na maendeleo ya jamii.
Watoa mada ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku ambaye atatoa mada kuhusu uongozi bora katika ustawi wa uchumi wa viwanda.
Mada nyingine itatolewa na Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano kuhusu fursa na changamoto katika ustawi wa uchumi wa viwanda.
Nyingine itatolewa na Samuel Kisori kuhusu uadilifu na utaifa katika ustawi wa uchumi wa viwanda.
Kongamano hilo litafanyika ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Nyerere ambayo kitaifa huadhimishwa Oktoba 14 ya kila mwaka.

No comments:

Post a Comment