Sunday, December 3

Nassari aeleza uvamizi ulivyofanyika kwake


Joshua Nassari, mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chadema, amesema watu wasiojulikana wamevamia nyumbani kwake na kufyatua risasi moja iliyomuua mbwa wake katika tukio ambalo amelihusisha na upinzani wa kisiasa uliotokana na uchaguzi mdogo wa madiwani.
Nassari amefafanua kuwa aliwajibu watu hao kwa kupiga risasi tano hewani, huku wenyewe wakipiga risasi kama 12 hivi, huku moja ikimpata mbwa wake.
Tukio hilo limetokea takriban miezi miwili baada ya mbunge mwingine wa Chadema, Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari lililoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma.
Nassari, ambaye chama chake kinaongoza kwa idadi ya madiwani jimboni mwake, amesema anahisi shambulio hilo lilifanywa na watu ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu.
“Kwa sababu kwa muda wa zaidi ya siku nne sikuwepo nyumbani na baada ya kurejea ndipo tukio hilo likatokea,” alisema Nassari.
Alisema, juzi alifika nyumbani kwake majira ya saa 5:00 usiku akitokea katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya vijana wa nchi za Afrika Mashariki zililofanyika kwenye taasisi ya MS TCDC iliyopo Usa River. “Nataka niamini taarifa nilizopewa kuwa nimekuwa nikifuatiliwa hata kabla ya uchaguzi mdogo kwa lengo la kunidhuru,” alisema Nassari.
“Kwa sababu mimi si mfanyabiashara (hivyo) hawana cha kuiba, zaidi ni sababu za kisiasa tu na Mungu amenisaidia sana.”
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema waliona kwenye mtandao wakawa wanamtafuta Nassari kwa kuwa baada ya tukio alitakiwa kwenda kuripoti polisi na ameshafanya hivyo.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo. Polisi walifika nyumbani kwa Nassari jana baada ya kuripoti tukio hilo akiwa na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Nassari hakueleza sababu za watu hao kumfuatilia na kutaka kumdhuru kutokana na uchaguzi mdogo wa madiwani ambao chama chake kilijitoa.
Hata hivyo, mbunge huyo alitoa tuhuma za madiwani waliokuwa wa Chadema kuhongwa fedha na kuahidiwa mafao yao iwapo wangehamia CCM.
Baada ya madiwani hao kuhamia CCM, Nassari aliwaonyesha waandishi wa habari video za jinsi kiongozi wa wilaya alivyowashawishi na kuwaahidi fedha. Tayari Nassari amewasilisha video hizo Takukuru.
Nassari alisema jana kuwa tangu awasilishe vielelezo vya ushahidi Takukuru, maisha yake yamekuwa hatarini.
Akizungumzia tukio la juzi usiku, Nassari alisema baada ya kufika nyumbani, takriban nusu saa baadaye alisikia hali isiyo ya kawaida ndani ya uzio wa nyumba yake na baadaye kusikia milio ya risasi kisha mbwa wake kunyamaza, hali iliyomfanya achukue silaha yake kujihami.
“Baada ya kusikia milio ya risasi, nikajua niko kwenye hatari nikafungua mlango wa nyuma nikaanza kurusha risasi kuelekea walipo,” alisema.
“Nilipiga risasi tano, wenyewe nadhani zimefika 12 kisha kukawa kimya nikaenda kuwaamsha vijana wanaonisaidia hapa nyumbani kuwaeleza tukio lililotokea kisha nikaondoka.”
Alisema alitaka kutoa taarifa polisi usiku huo, lakini baadaye akasita kutokana na kuwa na wasiwasi wa usalama wake kwa kuhofia wangemvamia akiwa njiani.
Alisema waliotekeleza tukio hilo hawakujua kama ana silaha kwa sababu mwaka 2014 wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa silaha yake aina ya bastola ilichukuliwa na polisi na hadi leo hajarudishiwa, hivyo kuwa na silaha nyingine kulimsaidia kujibu mapigo.
Mfanyakazi wake, Geofrey Joshua alisema alisikia milio ya risasi, lakini hawakuweza kutoka kwa sababu hakuwa na silaha na baada ya muda Nassari alitoka na kuwaelezea tukio zima kisha wakamuona mbwa mmoja kati ya wawili akiwa amekufa kwa kupigwa risasi.
Kaimu katibu wa Chadema wa mkoa, Elisa Mungure alisema tukio la kuvamiwa nyumbani kwa Nassari ni mwendelezo wa vitisho kabla na baada ya uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika jumapili iliyopita.
Mkazi wa eneo hilo, Dominick Mungure alisema tangu Novemba 25 mwaka huu siku moja kabla ya uchaguzi wa marudio hali ya usalama imekuwa tete huku baadhi ya watu wakishambuliwa na hakuna hatua zilizochukuliwa licha ya taarifa kutolewa na wahusika kutajwa.
“Hatujui hatma yetu kwa ujumla, hofu imetanda kwa kila mwananchi fikiria kama mbunge anaweza kuvamiwa hivi sisi wananchi itakuaje,” alisema Mungure.

No comments:

Post a Comment