Sunday, December 3

Wapangaji wadai fedha zao kwa wenye nyumba zinazobomolewa Dar


Wamiliki wa nyumba zilizowekwa alama ya X kutoka Kimara hadi Ubungo wamegoma kurudisha pesa kwa wapangaji wao walioanza kuondoka kwenye nyumba hizo.
Nyumba hizo zilizowekwa alama ya X Novemba 20 mwaka huu kupisha ujenzi wa barabara ya Morogoro zitaanza kubomolewa siku nne kabla ya sikukuu ya Krismasi.
Wapangaji hao wamelalamikia gharama za usafiri huku wengine wakiwataka wenye nyumba kuwarudishia japo gharama hizo za usafiri.
Wakizungumza na Mwananchi baadhi yao walisema walilipa kodi ya miezi sita na wengine miezi 12, hivyo wanastahili kurudishiwa fedha za miezi iliyobaki.
Mkazi wa Kimara Baruti, Victoria Charles alisema ameishi katika nyumba aliyopanga kwa mwezi mmoja tu.
“Nilikuja hapa mwishoni mwa Oktoba na wakati nakuja nililipia miezi sita, haya leo nyumba inawekwa alama X najuta kwa nini nililipa kiasi hicho cha pesa nilicholipa,” alilalamika Victoria.
Alisema alijaribu kumuomba mwenye nyumba amrudishie kodi iliyobaki lakini alimwambia kuwa hali ni ngumu kwa sasa.
“Tulijaribu kumueleza kuhusu kodi zetu alisema hana, yaani hapa usafiri tu natakiwa nitoe laki na nusu,” aliongeza.
Mkazi wa Ubungo, Abbas Mustafa alisema ameamua kuhama mapema ili kuondoa usumbufu na kuepusha vitu vyake kuharibika ubomoaji utakapoanza.
“Nakumbuka wenzetu Kimara waliathirika, vitu vyao vilivunjwavunjwa na kusababisha hasara, hivyo mimi naondoka mapema,” alisema Mustafa.
Alisema muda uliopo ni mdogo kwa wao kupata vyumba hata hivyo aliongeza kuwa hali ni ngumu kifedha na mwenye nyumba hakuwaeleza chochote juu ya malipo yao.
“Hii ni kama taarifa ya kushtukiza kwetu, ukizingatia hatujamaliza hata miezi mitatu tangu tumekuja kupanga hapa, lakini hatuna jinsi tutaenda kujisitiri kwa ndugu hadi hapo tutakapo pata pesa kwa ajili ya kupanga sehemu nyingine,” aliongeza.
Pascal Lameck aliyepangisha wapangaji tisa alisema wote wamehama na kila mpangaji alihitaji kurudishiwa pesa.
Alisema wakati anapokea pesa zao hakujua kama nyumba yake ingewekwa alama ya X jambo alilodai ni uonevu.
“Kinachonikosesha raha ni wapangaji kutaka niwarudishie pesa zao, hivi kwa maisha haya ndugu mwandishi naipata wapi pesa hiyo,” alisema.
Alisema mara kadhaa alipelekwa katika ofisi za kata ili alipe kodi alizochukua pamoja na kupewa muda wa kurudisha lakini alidai hana uwezo wa kulipa.
“Hata mimi roho inaniuma sana, sipendezwi na tuhuma hizi, lakini sina jinsi kwani hapa nilipo ninakosa raha maana nilikuwa nategemea wapangaji kuendesha maisha yangu,” alisema.
“Mimi kwa kweli uwezo wa kulipa sina na ili kunusuru maisha yao waondoke tu ili mwezi ujao Tanroads wasije kuharibu mali zao,”aliongeza.
Diwani wa Kata ya Kimara, Pascal Manota alisema amekuwa akipokea kesi mbalimbali za wapangaji kudai kutapeliwa na wenye nyumba.
“Unakuta mtu anakuja hapa anasema anataka kurejeshewa pesa yake kwa kuwa nyumba aliyopanga imewekwa alama ya X,” alisema Manota.
Alisema katika vikao vyao na wananchi waliwaambia wasilipe pesa nyingi kutokana na bomoabomoa hiyo.
“Baadhi ya wenye nyumba bado wanaendelea kuchukua kodi za wapangaji ila kwa sasa tumetoa agizo kwa viongozi wa serikali za mitaa kuwa mikataba yote ya upangishaji vyumba au nyumba ipitie huko ili tuwaonyeshe wananchi maeneo sahihi ya kupanga,” aliongeza.
Bomoabomoa yazua taharuki Dodoma
Mjini Dodoma, Kampuni ya Miliki ya Raslimali za Reli (Rahco) imezua taharuki baada ya kutangaza bomoabomoa kwa wafanyabiashara zaidi ya 1,000 waliojenga majengo na vibanda vya biashara katika hifadhi ya reli.
Juzi jioni, gari la matangazo lilipita likiwatangazia wafanyabiashara hao kuwa Rahco ingeendesha bomoabomoa kuanzia saa 12:00 jana asubuhi.
Wafanyabiashara wanaotakiwa kubomoa majengo yao ni wale waliojenga kandokando ya stendi ya daladala ya Jamatini, soko la Sarafina, kituo cha mafuta, mama lishe na vibanda vya kukatia tiketi za mabasi yaendayo mikoani.
“Waliojenga eneo la hifadhi ya reli, wanaofanya biashara eneo la hifadhi ya reli waondoke kabla ya kesho (jana) sasa 12.00 asubuhi. Ikifika asubuhi hujaondoka hutaruhusiwa kuchukua kitu chochote ndani,” alisema.
Hata hivyo, baada ya matangazo hayo wafanyabiashara walijikusanya na kuwaita viongozi mbalimbali wa mkoa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge.
Wakizungumza katika mkutano huo, wafanyabiashara hao walisema wako tayari kuondoka kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kupisha ujenzi huo, lakini wakaomba kupatiwa maeneo mbadala na muda wa kuondoka katika hilo.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Sakina Said alisema hawapingani na kauli ya Serikali juu ya kupisha maeneo hayo kwa ajili ya maendeleo ya Taifa bali wanaomba kupatiwa eneo jingine na muda wa kujiandaa kuondoka.
“Mkuu wa mkoa tunaiheshimu na kuitii Serikali yetu tukufu chini ya uongozi wa jemedari mkuu Rais Dk John Magufuli, tunachokuuomba tupatiwe muda na tuonyeshwe maeneo ambayo tutafanyia biashara zetu,” alisema.
Mfanyabiashara mwingine Jonath Jonathan alisema wengi wa wafanyabiashara wamechukua mikopo benki ambayo wanatakiwa kurejesha kwa wakati na kuomba Serikali kuwafikiria kuwapa muda na kuwatafutia eneo mbadala.
Akizungumza katika hadhara hiyo, Dk Mahenge aliwataka wafanyabiashara hao kutii amri ya kuondoka kwenye maeneo hayo ili kupisha ujenzi wa reli mpya ya kisasa.
Alisema mkandarasi ameshawekeana mkataba na Serikali na kwamba kazi ya ujenzi wa reli hiyo inatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

No comments:

Post a Comment