Anthony Petro (10) amezuia kuuzwa shamba hilo akidai kuona baba yake akisaini barua ya mauzo na hivyo kutoa taarifa polisi.
Akizungumza na mwandishi wetu juzi katika kituo kidogo cha polisi Kabanga, Anthony alisema alizuia shamba hilo lisiuzwe ili yeye na ndugu zake wawili wa kike wasikose sehemu ya kuishi.
Alisema wanaishi maisha ya dhiki wakimtegemea baba yao anayejishughulisha na kilimo na kuokota chupa za plastiki mtaani ili kupata chakula.
“Alitaka kuuza shamba ili sisi tukaishi wapi na tukalime wapi au tutatunzwa na nini? Niliamua kwenda polisi,” alisema mtoto huyo ambaye alisema ili kumsaidia mzazi wake huyo amekuwa akienda kutafuta misaada anapotoka shuleni.
Alisema amekuwa akienda kuomba msaada mji wa Kobero ulioko nchini Burundi umbali wa takriban kilomita nane kutoka wanapoishi na hufika huko kwa kuomba lifti kwenye magari.
Familia ya mtoto huyo iko eneo lililojitenga na makazi ya watu katika shamba lenye miti ya parachichi wakiishi kwenye nyumba chakavu iliyojengwa kwa miti na udongo.
Mkuu wa kituo kidogo cha polisi Kabanga, Bernard Masakia alithibitisha mtoto huyo kutoa taarifa kuzuia baba yake kuuza shamba.
Kutokana na uthubutu wake huo, Masakia kwa kushirikiana na askari wa polisi jamii waliamua kumsaidia baba wa mtoto huyo Sh35,000 kwa ajili ya kununua chakula na mahitaji mengine.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Mukitama, Kijiji cha Ngundusi, Joel Mwasi alisema Petro Magogwa (67) ambaye ni baba wa Anthony alitaka kuuza shamba kutokana na maisha kuwa magumu baada ya kufiwa na wake zake wawili .
Mwasi alisema tayari alishauza sehemu ya shamba hilo na kwamba mama wa mtoto huyo alifariki kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba.
Alisema familia hiyo inaishi mwisho wa kijiji ikipakana na kingine cha Kobero mkoani Muyinga nchini Burundi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngundusi, Josia Cleophace alisema Anthony hafanyi vizuri kitaaluma kutokana na mahudhurio yake darasani kuwa ya wastani.
Alisema mwanafunzi huyo amekuwa akienda kwenye vibanda vya wafanyabiashara kuomba misaada ili kupata chakula cha familia.
Wakazi wa Ngundusi, Medard Bilula, Edward Shungu na Generoza Chechelo kwa nyakati tofauti walisema mzazi wa mwanafunzi huyo anaishi kwa shida na watoto wanakosa mapenzi na malezi ya mama baada kufariki wakiwa wadogo.
Michael Nazali ambaye alinunua sehemu ya shamba alisema baba wa mtoto huyo alikuwa akihitaji fedha za matibabu na mahitaji mengineyo ya watoto hao ndipo alipomuuzia eneo mwaka 2000.
Alisema katika siku za hivi karibuni, amekuwa akimpatia msaada mzee huyo kutokana na sadaka zinazokusanywa na waumini kwa watu wasiojiweza na hakuwa na makubaliano ya kununua shamba kama inavyodaiwa na mtoto Anthony.
Mbali ya Anthony, watoto wengine wa Magogwa ni Eliza (9) na Editha (13) ambao wanasoma darasa la pili.
Magogwa alisema alioa jumla ya wake wanne na kuzaa watoto kadhaa huku wengine wakipoteza maisha kwa nyakati tofauti.
Alisema maisha yake yamekuwa duni baada ya kufiwa na wake zake wawili na wengine wawili waliachika na kati yao watatu walikuwa ni kutoka Burundi. Alisema wake wawili walio hai waliondoka na watoto watano.
Alisema wanawe watatu wa kike wameolewa lakini hawana uwezo kiuchumi hivyo anapougua au kuuguza msaada wake ni kukata sehemu ya shamba na kuuza.
“Nikiuza chupa 24 tupu za soda kwa wanaotengeneza pombe wananipatia Sh500 wakati mwingine napata Sh2,000 nanunua unga ili wanangu wasilale njaa,” alisema huku akibubujikwa machozi.
Alisema mara ya mwisho aliuza ardhi kwa Sh120,000 miaka mitatu iliyopita baada ya kuugua muda mrefu pamoja na wanawe.
Magogwa alisema, mkewe wa kwanza walizaa watoto wanane lakini watano wote wa kiume walifariki na kubaki watatu wa kike walioolewa.
Mke wa pili ambaye ni Mtanzania walizaa watoto wanane pia lakini kati yao, saba walifariki na aliyebaki ni msichana anayeishi wilayani Kahama.
Alisema mke wa watatu, raia wa Burundi walizaa watoto watano na wawili wa kiume walifariki na kubaki watatu wa kike ambao baada ya mama yao kufariki dunia, walichukuliwa na mama zao wadogo na wajomba ambao wanaishi Burundi.
Alisema mke wa nne walizaa naye watoto wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike. Alisema mama huyo alifariki kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba huku mwanaye mwingine wa kiume akifariki dunia baada ya miezi minane na kubakiwa na watatu akiwamo Anthony.
Alisema eneo la ardhi alilobakiwa nalo lenye miti ya parachichi na mikaratusi ameligawa kwa wanawe chini ya uongozi wa kitongoji ili hata akifa asiwepo wa kuwanyanyasa.
No comments:
Post a Comment