Wednesday, March 7

MKURUGENZI WA UNIDO AWASILI TANZANIA KUUNGA MKONO MAENDELEO YA VIWANDA

Serikali imesema kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) limekubali kushirikiana na serikali ya Tanzania katika ukuzaji na uendelezwaji wa viwanda nchini.

Hayo ameyasema Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akimpokea Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), LI Yong.

Mwijage amesema kwamba katika muda mfupi aliozungumza na Mkurugenzi huyo amesema kwamba yuko tayari kushirikiana na Tanzania katika ukuaji wa viwanda nchini na kuitangaza nchi yetu kimataifa ili kuvutia wawekezaji.

Mwijage amesema kuwa UNIDO imefanya vizuri katika nchi mbalimbali hivyo alichokifanya katika nchi zingine ndicho atakachokifanya Tanzania katika maendeleo ya viwanda vya kuzalisha bidhaa bora na sio mali ghafi.

Amesema kuwa ujio wa bosi wa UNIDO ni sehemu ya kutangaza bidhaa kuweza kupata masoko nje ya nchi na sio wakati wa sasa kupeleka mali ghafi.

Mwijage amesema katika kipaumbele kilichopo ni kuweka viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula pamoja na viwanda vya nguo ambapo mali ghafi zote zinapatikana nchini.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, LI Yong amesema kuwa katika ziara hiyo kuna vitu vingi atajifunza kwa nchi ya Tanzania kwa hatua iliyofikiwa katika uendelezwaji Viwanda.

Katika ziara hiyo atafanya mazungumzo na Viongozi wakuu wa Serikali kwa Tanzania bara na Zanzibar pia kufanya mazungumzo na Sekta binafsi nchini ikiwa ni sehemu ya kusukuma maendeleo ya viwanda kwa kasi.
 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akizungumza na waandishi habari kuhusiana na ujio wa Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, leo tarehe 7 Machi, 2018 jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya watendaji wa UNIDO pamoja na watendaji wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya nje, ushirikiano wa kikanda na kimataifa wakimpokea Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, LI Yong(kushoto) mara baada ya kuwasili.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage(kushoto)  akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, LI Yong(kulia) mara baada ya kuwasili nchini leo.

No comments:

Post a Comment