Wednesday, March 14

Yanayotajwa Ni maandamano ya kimwili ama ni ya kiroho

Mkuu wa Mwanza, John Mongella (katikati),
Mkuu wa Mwanza, John Mongella (katikati), akiongoza maandamano ya kupinga uwindaji haramu wa tembo na faru yaliyofanyika jijini Mwanza hivi karibuni, maandamano hayo hayakuwa ya kisiasa. Picha ya Maktaba 

Wahaya wana msemo wao usemao “Kyakutinisa kitakulye”, ni sawa na kitendawili. Jibu lake ni “mwilima”. Tasfiri yake inaondoa utamu wake. Kwa kujaribu; “Kinatisha lakini hakina madhara” na jibu lake ni “ giza”. Enzi zile kule vijijini hatukuwa na umeme, hivyo giza lilikuwa tishio kweli, lakini halikuwa na madhara.
Tumesikia kuna maandamano yanakuja mwezi wa nne. Mitandao ya kijamii inaandika kila siku juu ya maandamano haya na vyombo vya habari vimeanza kudakia baada ya viongozi kuyazungumzia.
Je, maandamano haya ni sawa na “Kyakutinisa Kitakulye”? Na tunaweza kujibu bila kusita kwamba ni “giza lisilo na madhara”? Tumesikia jeshi la polisi likisema kwamba atakayefanya maandamano atakipata cha moto. Na Rais John Magufuli akiwa Chato amesema kwa ukali kwamba atakayefanya maandamano atasimulia! Rais wa nchi ambaye ndiye amiri jeshi mkuu na mlinzi wa amani akitamka hivyo ni hatari sana.
Hata Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ameweka msisitizo kuwa hata wakiandamana nyumbani kwao kuzunguka kitanda watachukuliwa hatua.
Bahati mbaya kabisa, hatujasikia anayeuliza chanzo cha maandamano haya. Hakuna anayejadili namna ya kutafuta majibu ya maswali magumu yanayozunguka maandamano haya.
Hatujasikia mwenye kupendekeza njia za kuzigusa roho za wale wanaotaka kuandamana. Tunasikia mipango ya kuishughulikia miili ya watakaoandamana. Hatuwezi kujadiliana, hatuwezi kuzungumza, hatuwezi kubungua bongo na kuzama kwenye tafakuri, bali kupigana? Tunafikiri tutapata jawabu chanya kwa kupigana na pengine kupoteza maisha?
Hili ni swali langu kwa pande zote, wale wanaoandaa maandamano na wale wanaojiandaa kuyazuia. Haya ni maandamano ya kimwili au ni ya kiroho? Yawezekana pia wale wanaoandaa hawajatafakari juu ya hili. Ni muhimu kabisa kujua ni kitu gani kinalengwa hapa.
Maana kama ni maandamano ya kiroho, hakuna haja kubwa ya kuingia barabarani. Mtu anaweza kuyafanya akiwa nyumbani kwake. Maandamano ya kiroho ni hatari zaidi ya yale ya kimwili. Ni rahisi kupambana na maandamano ya kimwili kuliko ya kiroho. Ingawa kupambana na maandamano ya kimwili kunasababisha kupoteza maisha, maumivu na wakati mwingine ulemavu, ni mapambano ambayo mara nyingi yanaiacha roho salama.
Ninajua kabisa kwamba Rais Magufuli ana washauri wake, hivyo sina haja ya kusema ninamshauri; inawezekana wanamshauri na si lazima yeye kufuata kila unachoshauriwa, iwe ni ushauri mzuri, mbaya kwa nia mbaya au kwa bahati mbaya. Lakini hali inapoelekea kubaya hatuwezi kukaa pembeni na kuangalia yanayotokea kana kwamba tunaishi nchi ya jirani; sote tuna wajibu, vinginevyo historia itatuhukumu wakati ukifika na tuna la kusema mbele za Mungu; kwa vile mimi ni Mtanzania na nina uchungu na taifa langu, nashindwa kujizuia kutoa ushauri wa bure kwa Serikali inayoongozwa na CCM: Kabla ya kupambana kwa silaha na kuumizana, jiulize kwanza, maandamano haya ni “Kyakutinisa kitakulye” au ni ya kweli? Je, chanzo chake nini? Je, kuna la kujadili? Na swali kubwa kabisa ni: Haya yatakuwa ya kimwili au ya kiroho?
Kama ni maandamano ya kimwili inawezekana kuyazuia kwa njia zozote zile ikiwemo kutumia silaha za moto. Lakini kama ni ya kiroho kuna kazi, ni muhimu kutafuta njia nyingine ya kuzituliza roho.
Historia inatuonyesha kwamba kupambana na mwili hakujaleta mafanikio popote duniani. Tuna mfano wa Soweto na mifano mingine mingi ambapo maandamano yalizimwa kwa nguvu za silaha za moto, lakini hakukuwa na mafanikio. Mwili ni mapambo tu kwenye uhai wa mwanadamu. Mwili unakufa na kuzikwa; Kwa nini kupoteza muda na nguvu kushughulikia kitu kinachopita na kukiacha kile cha kudumu kama vile roho?
Mtu anayefikiri vizuri hawezi kumpiga binadamu mwenzake kwa nia yoyote ile; ukimpiga unaumiza mwili wake na roho yake inabaki salama, ukimpiga risasi akafa, unakufa mwili, roho yake inabaki salama. Hadi leo hii tuna roho za watu waliokufa, wako kaburini lakini roho zao ziko salama na zinaishi miongoni mwetu.
Roho ya Baba wa Taifa bado tunaishi nayo; roho ya Mkwawa bado tunaishi nayo, roho za mashujaa wote waliokufa wakitetea heshima na maisha ya Watanzania bado tunaishi nazo; wao walikufa ili sisi tuweze kuishi kwa uhuru na salama.
Sitaki kuamini kwamba Watanzania tumesahau historia. Hakuna popote duniani ambao risasi iliweza kupambana na wananchi. Watawala wote walioshughulika kuitesa miili ya wapinzani wao na wakati mwingine kuwaua, mwisho wao ulikuwa mbaya. Sitopenda kuingilia hili kwa undani, maana linaeleweka vizuri labda mtu kujifanya anaanzisha historia yake.
Hoja yake
Hoja yangu katika makala hii, ni kutaka tujiulize juu ya maandamano haya, ni ya kimwili au ni kiroho? Hili ni muhimu sana. Kama maandamano haya ni ya kiroho, kuna kazi ya ziada ya kufanya. Tanzania ni yetu sote – ni muhimu kabisa kutafuta chanzo na mzizi wa maandamano haya. Kuyazima kwa nguvu ni kufunika kitu kitakachochipuka kesho.
Viongozi wote waliofanikiwa kuongoza vizuri na kukumbukwa milele yote, ni wale waliofanikiwa kuzikamata na kuzifunga roho za wananchi wao, wale waliofanikiwa kutafuta majibu ya matatizo yanayogusa roho za watu wao. Mfano mzuri ni wa Mahatma Gandhi. Huyu hakuwa na Serikali, hakuwa na jeshi, hakuwa na polisi; lakini kwa vile alifanikiwa kuzishika na kuzifunga roho za Wahindi, alifanikiwa kutafuta majibu ya maswali yaliyokuwa yakigusa roho za Wahindi, walimsikiliza na kumfuata na kuungana kupambana na mkoloni bila kumwaga damu.
Hawakushika silaha kupambana, walifanya maandamano, waliendesha migomo na kususia bidhaa za Wazungu kama vile nguo na chumvi. Wafuasi wa Mahatma Gandhi, walipigwa na kuumizwa na polisi wa wakoloni, lakini walisonga mbele. Walifungwa na kuwekwa gerezani, lakini walisonga mbele. Yeye Mahatma Gandhi, alikuwa akifungwa usiku na mchana, lakini alisonga mbele kutetea haki na kuleta uhuru wa watu wa India.
Daima aliwaambia wafuasi wake, kwamba polisi wa wakoloni watapiga miili yao, lakini hawatazigusa roho zao. Filamu inayoonyesha maisha ya Mahatma Gandhi, inaonyesha vizuri kitu ninachojitahidi kuelezea kwenye makala hii. Nina imani viongozi walishaiona filamu hii. Kama ndio wanaisikia, basi waitafute waiangalie na kuona kama kuna la kujifunza.
Mfano mwingine ni wa Yesu wa Nazareti. Huyu hakuwa na mali, hakuwa na nyumba, hakuwa na Serikali, hakuwa na majeshi; lakini kwa vile alifanikiwa kuishika mioyo ya wafuasi wake na kuifunga, alitoa majibu ya maswali yaliyozigusa roho zao, walimfuata kila alipokuwa akienda na kuwa tayari kupoteza maisha yao kwa kufanya kazi yake.
Ukiondoa ujambazi ulioingizwa kanisani na Mfalme Constantine, watu waliingia kwenye imani ya Ukristo kwa mvuto; si risasi wala upanga, bali kwa kuvutwa; kwa mtindo wa kuzishika roho na kuzifunga, ni mfumo wa kutoa majibu ya maswali yanayogusa roho za watu. Bahati mbaya viongozi wa kanisa waliofuata baadaye hadi leo hii, wengi walishindwa kutengeneza mfumo mzuri wa kulifanya kanisa liwavutie waumini. Dini ya Ukristo ilienezwa kwa upanga na kumwaga damu kinyume kabisa na mafundisho ya Yesu.
Ingawa mfano wa magaidi si mzuri kuutumia katika makala hii, lakini kwa vile ni kitu kinachotokea kila wakati na sasa hivi nchi zote zimekuwa na mifumo ya kujikinga na magaidi, si vibaya kuutaja hapa. Nina imani wale wanaowaandaa magaidi si kwamba wanawafunga na kuwatesa ili kuwashawishi kukubali kujilipua, kinachofanyika ni kushika roho zao na kuzifunga.
Ni mfumo wa kuishughulikia roho zaidi ya mwili. Siungi mkono ugaidi, lakini huu ni mfano wa kuonyesha mafanikio ya kushughulikia roho badala ya mwili. Hata hivyo, dunia nzima imekataa kukaa chini na magaidi hawa kuongea na hao na kusikiliza matatizo yao. Kufikia hatua ya kujilipua, si kitu cha kudharau, wakisikilizwa mtu atashangaa kugundua kwamba hata hawa watu wazuri wanaopigana kwa njia hiyo kutetea uhai wao na uhai wa vizazi vijavyo.
Hata hivyo, ni muhimu nikaliweka jambo hili sawa hapa, ili nisieleweke vibaya. Ni haki kabisa kila mtu kutetea uhai wake, uhai wa ndugu zake na vizazi vyake, lakini ni dhambi ya mauti isiyokubalika, kutetea uhai kwa kuondoa uhai wa mwingine. Kutetea uhai, ni kuulinda uhai wa kila mtu na viumbe vyote.
Hivyo, kwa kiongozi anayetaka kuiongoza Tanzania, afahamu kwamba kuwapiga watu, kuwakamata na kuwafunga au kuwaua si msaada wa kumsaidia kuwaongoza vizuri. Njia hii imetumiwa na wengi na wameshindwa.
Makaburu wa Afrika Kusini walimkamata Mandela na kumfunga na kumtesa miaka 27, lakini kwa vile hawakufanikiwa kuigusa roho yake, wafuasi wake waliendeleza mapambano hadi alipofunguliwa. Makaburu walifikiri kumfunga Mandela ni kumaliza tatizo, kumbe ilikuwa imepandwa roho na inakua kwa kasi ya kutisha. Ingawa vyote vinategemeana, mwili na roho, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba roho ina nguvu lakini mwili ni dhaifu. Basi sisi kama taifa tujishughulishe kutafuta dawa ya kutufanya tuwe na roho yenye nguvu.

No comments:

Post a Comment