Wednesday, March 14

ZFDA yateketeza nyama kutoka Afrika Kusini

Mkuu wa Jiko la kuteketezea bidhaa mbovu,
Mkuu wa Jiko la kuteketezea bidhaa mbovu, Khamis Khamis Mkanga akiingiza nyama katika jiko hilo lililopo Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ajili ya kuteketezwa baada ya kuingizwa nchini kinyume na sheria zikitokea nchini Afrika ya Kusini. Picha na Abdallah Omar    
Zanzibar. Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA), imeteketeza  kilo 48 za nyama kutoka Afrika Kusini baada ya Serikali kusitisha uingizaji nyama kutoka nchini humo kutokana na mlipuko wa bakteria wa listeria.
Ilibainika kuwa nyama hizo ziliingizwa nchini kinyume cha sheria.
Nyama hizo ni mali ya kampuni ya Qamar ya Vingunguti jijini Dar es Salaam, ilikamatwa Uwanja wa wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza leo Machi 14 wakati wa zoezi hilo, mkuu wa kitengo cha uchambuzi wa hatari zinazotokana na chakula wa ZFDA, Aisha Suleiman amesema kilichosababisha kuteketezwa kwa nyama hiyo ni katazo lililotolewa na ZFDA baada ya kutokea mlipuko wa ugonjwa wa listeriosis.
Amesema ZFDA ndiyo yenye majukumu ya kuhakikisha wananchi wanapata chakula salama.
Aisha amesema uamuzi ya katazo hilo umetokana na uwapo wa maradhi ya Listeriosis nchini Afrika Kusini, hivyo ofisi yao imepiga marufuku uingizwaji nyama, maziwa na samaki kutoka nchi hiyo.
 Bakteria wa listeria, wanaosababisha maradhi ya listeriosis, wamesababisha vifo vya watu zaidi ya 180 Afrika Kusini.
Amesema katazo hilo si kwa Zanzibar pekee bali na Tanzania bara na nchi nyingine kutokana na utaratibu wa biashara kimataifa.
“Hili katazo siyo sisi tu, ni utaratibu wa kimataifa kwamba kutokana na maradhi ya listeriosis bidhaa za nyama, samaki, maziwa ni marufuku kuingizwa nchini sasa hii kampuni ya Qamar LTD ya Dar es Salaam wao waliamua kuingiza nyama hiyo, tumeikamata na kuiangamiza.” amesema Aisha.

No comments:

Post a Comment