Wednesday, March 14

Karume: Kuheshimu haki zawengine chanzo cha amani

Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume 

“Kuheshimu haki za wengine ni amani.” Ndivyo anavyosema Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume wakati akihutubia mkutano amani katika mji wa Belfast nchini Ireland hivi karibuni.
Karume ni rais wa sita wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ni mtoto wa rais wa kwanza visiwani humo, Abeid Amani Karume.
Karume ambaye ana historia ya kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kufanya mabadiliko ya kikatiba na kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), alizungumzia umuhimu wa amani kwa kumnukuu Rais wa zamani wa Mexico, Benito Juarez aliyewahi kusema palipo na heshima pana amani. Na kuwa kuheshimu haki za wengine maana yake ni amani.
Suluhu ya kisiasa ya Zanzibar kati ya vyama vya CUF na CCM wakati wa utawala wake pengine ndiyo iliyowafanya waandaaji wa mkutano wa amani kutoka Taasisi ya Amani Duniani (GBF), kumwalika Karume kuhutubia mkutano huo unaofanyika Belfast.
Karume anabebwa na mwafaka wa tatu baada ya kufanya mazungumzo na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CUF na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad na kuunda SUK. Hapo ni baada ya mwafaka wa kwanza wa 1996 uliosimamiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyaoku na mwafaka wa pili uliokuwa kati ya Katibu Mkuu wa CCM kwa wakati huo, Philip Mangula na Maalim Seif.
Mbali na kunukuu kauli ya Benito, kwamba penye heshima ndipo ilipo amani, Karume pia amewaambia washiriki wa mkutano huo wa Belfast kwamba kiongozi mwenye maadili lazima awe mpole, anayeweza kujieleza vizuri, anayeongozwa kwa haki na usawa, kuwajibika kwa kasi inayotakiwa, kukiri makosa na kuheshimu haki za kila raia.
Hotuba ya Karume kwa washiriki wa mkutano huo ililenga umuhimu wa uadilifu na ubunifu wa viongozi kwa amani barani Afrika ambapo GPF tangu kuanzishwa kwake imejikita katika kuinua ubunifu na msingi bora kuendeleza ujenzi wa amani duniani.
Karume aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kwamba hivi karibuni alikuwa Kampala nchini Uganda ambako alikutana na Rais Yoweri Museveni na mazungumzo yao yalijielekeza kwenye hoja mbili za kujenga amani na maisha bora kwa wananchi.
Akizungumzia hoja ya msingi ya uongozi wenye misingi ya uadilifu na ubunifu, Karume anasema hoja zote mbili ni muhimu katika kuendeleza amani na kuboresha maisha ya watu.
“Kwa ushahidi, si mimi tu ninayethamini uongozi wa uadilifu na ubunifu ikiwamo umuhimu wa kuijenga amani, mahudhurio yenu kwenye mkutano huu yanaonyesha namna mnavyothamini ujenzi wa amani. Tumekutana wote hapa kubadilishana mawazo ambayo ni muhimu sana yanayohusu maadili ya uongozi katika kujenga amani endelevu miongoni mwetu, hasa katika uongozi wenye uadilifu na ubunifu,” anasema Karume.
Karume aliweka historia ambapo uhasama wa CCM na CUF uliwekwa
pembeni Novemba 3, 2010 alipoapishwa rasmi kushika uongozi wa nchi kwa awamu ya kwanza Dk Ali Mohamed Shein. Sare za CCM, CUF na vyama vingine zilivaliwa bila kujali itikadi. Mfuasi wa CCM alivaa sare ya CUF na wa CUF alivaa ya CCM au NCCR-Mageuzi.
Historia hiyo ya uvumilivu wa kisiasa ilijitokeza pia kwenye hotuba ya Karume kwa kusema kiongozi mwenye maadili anatawala maeneo yote katika jamii kama ilivyokuwa kwa kiongozi wa kisiasa na wa kijeshi wa Roma ya kale, Julius Caesar.
Caesar au Gaius Julius Caesar anakumbukwa hasa kwa mafanikio mbalimbali yanayoonekana kuathiri dunia hadi leo. Baadhi ya mafanikio hayo ikiwamo kuheshimika na jina lake kuwa neno kwa ajili ya cheo cha watawala wa Kiroma waliomfuata. Kutokana na badiliko hilo la jina “Caesar” kuwa cheo, lugha mbalimbali zilipokea cheo hicho kama vile Kijerumani (“Kaiser”), Kirusi (“Tsar”) na Kiswahili (“Kaisari” - kutokana na neno la Kijerumani).
Pia, aliunda kalenda ambayo imekuwa msingi wa kalenda ya kimataifa leo (Kalenda ya Juliasi). Kwa heshima yake, mwezi wa saba unaitwa Julai.
Karume anasema historia ya Caesar ambayo inaendelea kugonga vichwa vya habari, kutawala mijadala ya wasomi na maeneo mbalimbali ina muhimu wake hata katika dunia ya sasa ambayo imeendelea kuwa na siasa zinazoyumba, misuguano ya kimaadili, migogoro ya uongozi wa kisiasa, rushwa na uroho wa madaraka.
Anasema kama inavyofahamika siasa ni moja ya shughuli muhimu za kibinadamu inayoongozwa na kanuni, sheria na usawa katika kuvumiliana. Karume anaendelea kusema siasa inahitaji uwajibikaji wa hali ya juu kutoka kwa wananchi, vyama vya siasa, wabunge, watendaji wa Serikali, mahakama, vyombo vya habari, jumuiya za wafanyabiashara, taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za dini na taasisi za elimu.
Karume ambaye wakati akigombea urais wa Zanzibar kwa mara ya kwanza alitambulishwa kama ‘mtoto wa simba’ kwa maana baba yake alikuwa na msimamo mkali katika uongozi wake na yeye (Karume) alitabiriwa kuwa vivyo hivyo, anasema uaminifu ni heshima katika siasa na vyombo vya umma ni muhimu kwa amani, maendeleo kwa jamii, hasa katika kuinua demokrasia.
Anasema kupitia uaminifu, viongozi wanatakiwa wawe imara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kimaadili katika kukabiliana na changamoto za kisiasa na jamii iliyogawanyika kwa kuweka taratibu za kuaminia na zenye maadili, ikijumuisha uaminifu, ukweli na haki.
Karume anasema viongozi wa kisiasa wanatakiwa kuwa mfano kwa wanaowaongoza, wananchi wao waone uaminifu wao, ukweli na ujasiri huku akisema Afrika ina bahati ya kuwa na viongozi wengi ambao wameonyesha viwango vikubwa vya uongozi wa uadilifu na ubunifu kama vile Samora Machel (marehemu) wa Msumbiji, Kenneth Kaunda wa Zambia, Nelson Mandela (marehemu) wa Afrika Kusini na hakumsahau baba yake Abeid Amani Karume (marehemu) kwamba katika uongozi wake alibadili Zanzibar kiuchumi na kijamii.
Mwasisi huyo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 kwa kuondoa utawala wa kisultani wa Waarabu, Abeid Amani Karume alishika uongozi wa visiwa hivyo vya Unguja na Pemba na kuamuru mwingiliano wa kijamii kwa kuruhusu ndoa kati ya Waafrika na raia wa kigeni. Pia, ujenzi wa majumba ya Michenzani na mambo mengine ya kiuchumi kama ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya Bwawani na uanzishwaji wa kituo cha kwanza Televisheni ya rangi kwa Afrika.
Anasema Afrika ni bara lililo kwenye mabadiliko lina utajiri wa asili na rasilimali watu, lakini bado linaendelea kuogelea kwenye dimbwi la umaskini, njaa, kipato kisichowiana na usalama mdogo kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe, ugaidi na vurugu zinatokana na migogoro kadhaa.
Karume anasema kwa sasa uongozi wenye maadili ndiyo unaohitajika zaidi kuliko huko nyuma, hasa changamoto za kisiasa, kiuchumi na maendeleo ya kijamii. Mbali na kuzungumzia mkutano wa ‘kuendeleza amani, usalama na maendeleo endelevu kwa Afrika Mashariki’ uliofanyika Zanzibar 2015 ambao ulisisitiza umuhimu wa uaminifu na heshima kwa kila mmoja, pia alizungumzia uzoefu wake kuhusu Zanzibar ilivyogawanyika kutokana na migogoro ya kisiasa na kwamba ni namna gani uongozi wa uaminifu na ubunifu ulivyoleta amani Zanzibar.
Anasema uzoefu wake alipokuwa Rais wa Zanzibar mgawanyiko wa kisiasa uliwanya wabuni utamaduni wa maelewano kupitia ushirikishwaji wa pamoja kwa njia ya kidemokrasia, ilikuwa ni suluhisho pekee la kisiasa katika visiwani hivyo.
Karume anasema kama kiongozi, alitumia haki na uwakilishi wa wananchi wote kupitia vyombo vyao vya uwakilishi ikiwamo chama chake cha siasa, ilikuwa ni wakati wa kuwa mbunifu, mwenye msimamo, kufikiria malengo ya muda mrefu na kuweka pembeni hisia zake za kisiasa.
“Nina hakika hiyo ilikuwa ni uamuzi sahihi wa kisiasa kwa maslahi ya wananchi.” Anasema Karume huku akimnukuu mshindi wa tuzo ya amani duniani, Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini alisema; “Tunataka watu ambao wapo kwa masilahi ya watu na si kwa masilahi binafsi.”

No comments:

Post a Comment