‘Mahakama ya Kangaroo’ ni msamiati wenye maana ya mabaraza ya uamuzi au mikutano yenye kutoa hukumu kwenye mashauri mbalimbali pasipo kuheshimu misingi ya sheria na haki. Kwamba watu wanakaa kikao na kutoa hukumu kwa mtu au watu bila kutimiza viwango vya kisheria katika utoaji haki.
Msamiati huo pia hubeba tafsiri ya uwepo wa mahakama halali kisheria yenye mamlaka kwenye nchi, lakini hakimu au jaji kwa makusudi anaamua kuendesha kesi nje ya sheria na maadili ya mahakama. Pia, huonekana kupitia hukumu zenye kukandamiza haki kwa makusudi.
Kauli kali zenye kuhukumu kabla ya kufika mahakamani ambazo hutamkwa na watawala au amri za kisiasa zenye kutolewa na viongozi wa nchi ni miongoni mwa masuala yenye kuelezwa kama Mahakama ya Kangaroo. Matamshi yenye kumtia mtu hatiani kwanza kisha vyombo vya sheria ndiyo vianze kuchukua hatua, ni kipimo chenye kuthibitisha hali hiyo.
Mfano wa Mahakama ya Kangaroo ni kama Baraza la Mapinduzi ya watu wa Cambodia, lililoketi Agosti 19, 1979 na kumhukumu kifungo cha maisha jela aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Pol Pot na ndugu yake, Leng San. Umoja wa Mataifa ulikataa hukumu hiyo kwa sababu baraza husika halikutimiza vigezo vya kimahakama, yaani hakukuwa na mchakato kabla ya hukumu.
Katika mahakama za kawaida ukweli wa pande mbili unasikilizwa kwa uhuru usio na vipengele. Ushahidi unatolewa na shahidi anavumiliwa wakati akieleza kile alichonacho kuhusiana na shauri husika. Mawakili wanaachiwa uga mpana wa kuhoji ili kurahisisha haki ionekane inatendeka. Mwisho jaji au hakimu anahukumu baada ya vipimo vya kisheria.
Mchakato wa mahakama umewekwa kwenye nchi ili kulinda haki za watu dhidi ya haki za kisheria. Kwamba mtu hata aonekane mkosefu kiasi gani kwenye macho ya wengine, hususan watawala, ahukumiwi kwa matakwa ya watu, bali anapimwa dhidi ya haki za kisheria. Huo ndiyo utaratibu wa nchi kama ulivyowekewa mwongozo na Katiba ya nchi.
Kwa kurejea tafsiri ya Mahakama ya Kangaroo ni kuwa maoni yoyote yenye kuhukumu watu wengine ni kosa, maana ni uthibitisho wa uwepo mahakama hiyo. Na kwa vile kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na maoni mengi yenye kuhukumu wengine, ni wazi kuwa mitandaoni kuna mahakimu na majaji wengi siku hizi.
Viongozi wengi wa kisiasa wamekuwa wakitoa amri na matamshi yenye kuhukumu. Huo ni uthibitisho kwamba mahakama hii inapatikana sana kwenye majukwaa ya kisiasa. Inapaswa kufahamika kwamba Mahakama ya Kangaroo ni kielelezo cha nchi kuwa na watu wasioheshimu haki za kisheria ambazo zimewekwa mahsusi ili kulinda haki za watu.
Kadhalika ni kipimo kuwa watu wengi hupenda watendewe haki lakini wao wenyewe hawaheshimu haki za wengine. Vilevile viongozi ni wepesi kusisitiza kuchukuliwa kwa hatua za kisheria, lakini katika nafasi zao hawaziheshimu. Mahakama za Kangaroo hazipaswi kuwepo. Kila mtu ni vizuri akajisikia kutendewa haki mbele ya sheria za nchi.
Nondo na Mahakama ya Kangaroo
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo ambaye ni mwenyekiti wa Mtandao wa Haki za Wanafunzi Tanzania (TSNP), alidaiwa kutoweka usiku wa Machi 6, mwaka huu, kabla ya kupatikana jioni Machi 7. Inaelezwa kuwa Nondo alipokuwa kwenye mazingira aliyohisi ni yenye hatari, alituma ujumbe kwa rafiki yake.
Nondo anadaiwa kutuma ujumbe “Nipo katikati ya hatari”. Baada ya hapo hakupatikana tena. Jioni ya Machi 7, Nondo alipatikana au alijikuta yupo Mufindi, Iringa. Mtu aliyetoa taarifa za Nondo kupatikana Mufindi, alidai alimkuta akiwa haelewi alipo, ndipo alimsaidia pesa ya kukodi taksi aende Kituo cha Polisi Wilaya ya Mufindi kuripoti apate msaada zaidi.
Habari za awali ni kwamba Nondo alikuwa Dar es Salaam. Ujumbe kwamba alikuwa kwenye hatari, aliutuma akiwa Dar es Salaam. Siku iliyofuata ndipo alijikuta Mufindi. Taarifa za kupotea Nondo zilisababisha mwamko mkubwa wa kuhoji hasa kwenye mitandao ya kijamii. Nondo alipatwa na madhila hayo kipindi akiwa ameahidi kuongoza wanafunzi kuandamana kushinikiza Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ajiuzulu.
Nondo alisema, wangeandamana kwa sababu ya kuwapo kwa matukio mengi ya uvunjifu wa haki za binadamu. Watu wengi wakikutwa wameuawa nchini na kukosekana majibu ya kina kuhusiana na vifo hivyo. Zaidi ni tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye daladala Februari 16, mwaka huu, wakati polisi wakizuia maandamano ya viongozi na wafuasi wa Chadema, waliokuwa wanakwenda ofisi za msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni, kushinikiza mawakala wao wapewa hati za viapo na barua za utambulisho.
Akwilina hakuwa katika sehemu ya maandamano. Vilevile kuna wengine walikuwa kwenye maandamano na walipigwa risasi, lakini wakawekwa mahabusu bila kutibiwa wala kupewa dhamana. Kwa matukio hayo, Nondo aliona ni wakati mwafaka Mwigulu kung’oka Wizara ya Mambo ya Ndani.
Sasa basi, baada ya Nondo kuwa amepatikana na kwenda Kituo cha Polisi Mufindi, taarifa ya awali kabisa ya Kamanda wa Polisi Iringa, Juma Bwire ilieleza watamshughulikia kama taarifa alizotoa zilikuwa za uongo. Kwa hisia za Kamanda Bwire ni kwamba huenda Nondo alitoa taarifa za kutekwa ili kuhamasisha wanafunzi wenzake kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Izingatiwe kuwa Nondo ndiye mlalamikaji. Aliripoti polisi ili kueleza yaliyomsibu kuanzia kutekwa Dar es Salaam mpaka kujikuta Mufindi. Polisi wanaopaswa kushughulikia tukio hilo, kabla hata ya kufanya uchunguzi, wanaanza kutoa vitisho.
Ukiisoma kauli ya Kamanda Bwire, unaona kuwa polisi wanamtuhumu Nondo kwa nafasi ya kwanza kwamba ‘alijiteka’ kwa nia ovu, halafu wanazichukua tuhuma zake za kutekwa kwa nafasi ya pili.
Mpaka hapo inatia shaka ikiwa kweli Nondo alitekwa, kama utafanyika uchunguzi makini, wakati wachunguzi wenyewe wanamtuhumu anayetakiwa kusaidiwa kiuchunguzi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar wa Salaam, Paul Makonda, yeye ameagiza polisi Iringa wakishamalizana na Nondo, wampeleke Dar es Salaam wamshughulikie kwa sababu hawezi kuuchafua ‘mkoa wake’ halafu aachwe. Hakuna namna nyingine ya kuitafsiri kauli hiyo zaidi ya kuusema ukweli kwamba Nondo ameshahukumiwa kuwa hakutekwa.
Katika mitandao ya kijamii hali ndiyo mbaya kabisa. Watoa maoni wengi wanamtuhumu Nondo kuwa alisafiri kwa basi mwenyewe kwenda Mufindi, kwa hiyo alitangaza kuwa ametekwa ili kusababisha taharuki kwa nchi, vilevile kujitafutia umaarufu kwa njia za kihalifu. Tayari Nondo ameshahukumiwa mitandaoni.
Haki batili
Viongozi na watumia mitandao ya kijamii wanatakiwa kuheshimu haki za kisheria. Waache kujigeuza Mahakama za Kangaroo. Hukumu kwa watenda makosa haitolewi mitandaoni wala kwenye majukwaa ya viongozi wa kisiasa. Misimamo ya kisiasa isiwe sababu ya kuwazodoa au kuwapuuza wenye kustahili haki.
Inatakiwa kwanza Nondo asikilizwe. Alichokisema kifanyiwe uchunguzi. Ikiwa maelezo yake yatakosa nguvu ya kiupelelezi, ndipo tuhuma zihame, kutoka kutuhumu kutekwa hadi yeye kutuhumiwa kujipoteza kwa nia ovu. Siyo kumshambulia na kuanza kutoa ahadi za kumshughulikia.
Tafakari iwapo Nondo kweli alitekwa. Maumivu aliyonayo kutokana na tukio hilo. Wakati akitegemea polisi na viongozi wa nchi wamsikilize, wamtendee haki na ikibidi waliomfanyia uhalifu wakamatwe, anajikuta akituhumiwa kutaka kusababisha taharuki kwa nchi kwa kutangaza alitekwa wakati haikuwa hivyo.
Wengine wanasema si kweli kwamba Nondo alitekwa, maana asingeachiwa nafasi ya kutuma ujumbe wa simu kwa rafiki yake. Wanasema kama alitekwa mbona hakuguswa hata kidogo? Watu hao wanajipa uchambuzi wa watu kutekwa. Utafikiri ipo kanuni kwamba kila mwenye kutekwa lazima anyang’anywe simu na apigwe mpaka aumizwe.
Aliyesema Nondo anauchafua mkoa wa Dar es Salaam kwa kutangaza alitekwa, maswali kwake ni je, anayechafua ni anayeteka au anayetekwa? Kwa nini watu wawe wakali kwa aliyetangaza kutekwa kuliko kusaidia kuwapata watekaji? Je, imesahaulika kuwa mwanamuziki Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’ alitekwa wapi?
Roma akiwa na wenzake watatu, walitekwa Oysterbay, Dar es Salaam kwenye studio ya muziki ya Tongwe Records na walishikiliwa kwa siku tatu kabla kuachiwa na kujikuta wapo Ununio, Dar. Kada wa Chadema, Ben Saanane, alitoweka Dar es Salaam tangu Novemba 2016 na mpaka leo hajaonekana.
Wapo watu walituhumu kuwa Ben alijipoteza mwenyewe kutafuta umaarufu. Miaka inapita, hali ni kimya, Ben haonekani. Hata Roma na wenzake pamoja na kutokeza wakiwa wamejeruhiwa, bado walisemwa walijiumiza makusudi ili kuhalalisha kwamba walitekwa. Leo Nondo anaulizwa eti mbona hakuumia hata kidogo. Mahakama za Kangaroo ni hatari sana.
No comments:
Post a Comment