Wednesday, March 14

Wapandishwa kizimbani kwa kusafirisha magunia 400 ya mkaa


Dar es Salaam. Nahodha wa meli ya MV Kops, Buruhani Haji (25) na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili  likiwamo la kusafirisha magunia 400 ya mkaa ndani ya boti.
Washtakiwa wengine ni Juma Mcha (24), Ally Salum(22), Salum Zuberi (25), Mahazi Kombo (22) na Omari Ahmad(23), wote ni mabaharia na wakazi wa Zanzibar.
Wakili wa Serikali, Mosii  Kaima amedai leo Machi 14, 2018 mbele hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba  kuwa washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Machi 2, 2018 kati ya ufukwe wa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam  na Unguja.
Kaima amedai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha magunia 400 ya mkaa yenye thamani ya Sh30 mil, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa wanadaiwa kusafirisha mkaa huyo kwa kutumia boti ya MV Kops yenye usajili wa namba  Z.931, bila kuwa na kibali cha usafirishaji kinachotolewa na mamlaka husika, huku wakijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Wakili Kaima alidai kuwa katika shtaka la pili, washtakiwa walikutwa na mazao ya misitu katika boti hiyo, bila kuwa na leseni  inayotolewa na Mkurugenzi wa mamlaka ya misitu nchini.
Washtakiwa hawakutakiwa kusema chochote mahakamani hapo kutokana kesi inayowakabili kuwa ya uhujumu uchumi.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo, hadi Machi 19, itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

No comments:

Post a Comment