Dodoma. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeomba kuidhinishiwa Sh33.2 bilioni katika bajeti ya mwaka 2018/19, huku ikieleza mambo 10 itakayoyatekeleza kupitia taasisi zilizo chini ya wizara hiyo katika mwaka huo wa fedha unaoanza Julai mosi.
Miongoni mwa mambo hayo ni kuendelea kutoa elimu juu ya kanuni mpya za maudhui kwenye redio na televisheni zilizotungwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010, inayowabana wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni mjini Dodoma jana, waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe alisema katika mwaka huo wizara hiyo kupitia Idara ya Habari (Maelezo) pamoja na mambo mengine itaratibu kuanzishwa kwa vyombo vipya vya usimamizi wa masuala ya habari kama dawati la matangazo ya Serikali. “Pia Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Habari vilivyoanzishwa chini ya sheria namba 12 ya Huduma za Habari ya mwaka 2016,” alisema.
Kuhusu Shirika la Utangazaji (TBC), alisema litaanzisha chaneli ya utalii itakayorusha na kutangaza vipindi vinavyohusiana na maliasili zilipo nchini na kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumzia kanuni mpya za maudhui ambazo zinasimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Dk Mwakyembe alisema msingi wake ni kuhakikisha teknolojia inatumika badala ya kututumikisha na kuvuruga mustakabali wa maadili ya Taifa.
Alisema moja ya malengo ya kanuni hizo ni wahusika kuingia katika mfumo rasmi wa kutambulika kisheria na kuwajibika kulipa kodi watoa huduma wa picha jongevu za habari na burudani, na kutoa matangazo kwa njia ya mtandao (bloggers). “Zinamtaka kila mtumiaji wa mtandao awe na namba yake ya siri ili wajanja wasitumie kiurahisi chombo chake cha mawasiliano kutenda matendo hasi kinyume na sheria,” alisema.
“Zinazuia usambazaji wa kauli chafu, matusi, picha mgando na jongevu za utupu na zenye maudhui yasiyofaa kwa watoto.”
Alisema kanuni hizo pia zinataka redio na runinga kutoa kipaumbele kwa muziki wa Kitanzania kati ya saa 11:30 alfajiri hadi saa 3:00 usiku na kwamba, muziki wa Kitanzania uchukue asilimia 80 ya muda huo.
Kuhusu Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), alisema litakuwa na jukumu la kukitangaza, ikiwa ni pamoja na kuchapisha kamusi na kusajili wataalamu 500 wa lugha hiyo.
Mambo mengine yatakayofanywa na wizara hiyo ni kusimamia majukumu yanayofanywa na Bodi ya Filamu Tanzania, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Dk Mwakyembe aliliomba Bunge kuiidhinishia wizara hiyo bajeti ya Sh33.3 bilioni, kati ya fedha hizo Sh15.2 bilioni ni kwa ajili ya mishahara, Sh9.3 bilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh8.7 bilioni za miradi ya maendeleo.
Waziri huyo pia aligusia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 inayoishia Juni mwaka huu, kwamba mpaka kufikia Machi mwaka huu, wizara hiyo ilikuwa imepokea kiasi cha Sh18.1 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 64 ya bajeti yote ya Sh28.2 bilioni.
No comments:
Post a Comment