Dar es Salaam. Neema zilizoachwa na ujio wa ndege kubwa aina ya Airbus A380-800 inayomilikiwa na Shirika la Ndege la Emirates jijini Dar es Salaam zimeendelea kutajwa.
Aprili 25, ndege hiyo ya abiria ambayo ni kubwa zaidi miongoni mwa zilizowahi kutua hapa nchini, ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa dharura na ghafla biashara katika uwanja huo na sekta ya hoteli ikaongekeza.
Imeelezwa kuwa, ujio wa ndege hiyo haukuacha neema kwa hoteli za kitalii ambazo abiria wake waliokuwa wakielekea Mauritius pekee walilala, bali hata Serikali kupitia baadhi ya taasisi zake zilinufaika.
Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 475 na wahudumu 27, ilishindwa kutua nchini Mauritius kutokana na hali mbaya ya hewa na kumlazimu rubani wake kuchagua uwanja wa Dar es Salaam kutua kwa dharura.
Ndege hiyo iliyotua Aprili 25 saa saba mchana, iliondoka siku iliyofuata saa 2:15 asubuhi kuendelea na safari yake.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari alisema jana kuwa, japokuwa ndege hiyo ilikuja wakati mgumu ambao ndege nyingine zilikuwa zimetua, ilihudumiwa sambamba na abiria wa ndege zingine.
Licha ya kuziingizia fedha hoteli walizolala wasafiri liliokuwa nao, Johari alisema pia Emirates iliingizia Serikali mapato kutokana na mafuta iliyowekewa ndege hiyo.
Alisema ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba lita 320,000 za mafuta, ilinunua lita 98,000 katika uwanja huo.
“Ilikuja kwenye peak time (muda mgumu) kwa sababu kulikuwa na ndege nyingine zinakuja kama Emirates (nyingine), Qatar, Ethiopia na nyinginezo ambazo kwa pamoja kulikuwa na abiria zaidi ya 2,000 lakini tuliwasimamia vizuri. Kwenye hilo tukawa tumefanya biashara,” alisema Johari. “Baada ya kuondoka asubuhi walitaka kujaza mafuta, ndege ile inakunywa lita 320,000 lakini pale ilikunywa lita 98,000.”
Hata hivyo, meneja wa operesheni wa kampuni ya Puma Energy, Raymond Tungaraza alikataa kutaja bei ya mafuta hayo akisema sera za ushindani wa biashara haziruhusu. Serikali ni mmiliki mwenza wa Puma Energy.
“Tuna taratibu zetu za ushindani wa kibiashara zinazotuzuia kutaja bei ya mafuta, lakini kwa kawaida bei yake inakuwa chini ya mafuta ya taa kwa sababu hayana kodi ya ongezeko la thamani. Lakini hayo ni mafuta mengi japo ni kama theluthi moja tu ya uwezo wa ndege hiyo,” alisema Tungaraza.
Johari alitaja huduma muhimu zilizotumiwa na ndege hiyo kuwa ni pamoja na mashine za ardhini za kusukuma ndege nyuma kabla haijaruka (push back) na ngazi za kushuka na kupandia abiria ambazo hutolewa kwa tozo maalumu, huku akitaja tozo ya kutua na kupaa kuwa ni Dola 620 (zaidi ya Sh1.53 milioni).
Kuhusu malazi ya abiria pamoja na wahudumu, alisema walitumia hoteli za nyota tano na nne ambazo ni Serena, Golden Tulip, Southern Sun na New Africa.
Baadhi ya wenye hoteli hizo walipoulizwa kwa simu jana hawakutaka kuzungumzia wateja wao, wala biashara hiyo ya ghafla.
Kaimu meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (Taa), Joseph Nyahade alisema japo bado hawajapiga hesabu kamili, lakini ni wazi ujio wa ndege hiyo uliongeza mapato yao. “Ile ni ndege kubwa na ilikuwa na abiria 475, kwa hiyo walikuwa wakihitaji huduma kubwa. Kama ni ngazi tuliwapatia, huduma ya usafi ilifanyika vizuri na zote hizo zinalipiwa. Sisi wenyewe kama mamlaka tulilipwa ada kubwa kulingana na ndege yenyewe, japo kwa sasa bado hatujapiga hesabu za mwisho,” alisema Nyahade.
Alisema mamlaka zote ikiwamo Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hoteli zilizopata wageni, ziliingiza mapato ya ghafla.
Kuhusu vigezo vilivyozingatiwa hadi ndege hiyo kutua Dar es Salaam, Johari alisema ni ubora wa uwanja kwani ndege hiyo inahitaji njia ya kutua yenye urefu wa kilomita tatu na upana wa mita kati ya 60 hadi 75.
“Kulingana na ndege aliyonayo, rubani ataangalia ‘running way capacity’, uwanja wa JNIA una urefu wa kilometa 3.1 umezidi kidogo na upana wa mita 60,” alisema.
Alitaja pia ubora wa mitambo ya uongozaji ndege inayomwezesha rubani kutua kwenye mistari maalumu bila kukosea na mifumo ya mawasiliano.
Vilevile, alisema huduma ya udhibiti wa moto ni kigezo kingine ambacho kwa JNIA ni ya kiwango kinachotakiwa ambacho ni namba tisa na ndicho kilichopo.
“Rubani pia anazingatia mitambo ya kutoa huduma za ardhini ikiwa pamoja na ngazi za kushukia abiria. Je, kuna mtambo wa kuwashia? (air starting unit) kwa sababu si muda wote ndege inakuwa ‘on’ (imewashwa). Wakati wa kuondoka kuna mtambo wa kuisukuma nyuma? Anataka kujiridhisha na mtoaji wa mafuta (fuel farm),” alisema.
Alitaja pia kiwango cha usalama (safety maturity level) akisema kwa sasa kimepanda kutoka asilimia 37.8 ya mwaka 2013 katika ukaguzi waliofanyiwa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani hadi asilimia 64.35 mwaka 2017.
“Aviation security level’ tulipokaguliwa tulipata asilimia 83, kwa hiyo tuko vizuri katika masuala ya usalama,” alisema Johari na kuongeza,“Hata kwenye operesheni wakiwamo marubani wa ziada pia wanapatikana.”
Hata hivyo, alitaja changamoto za kutokuwapo kwa mapokezi ya ghorofa katika uwanja huo, hivyo abiria waliokuwa ghorofani kushindwa kupokewa moja kwa moja kutoka kwenye ndege kuingia kwenye jengo la abiria.
“Somo kubwa tulilojifunza, tumepata kujiamini zaidi kwamba tunaweza kuhudumia ndege kubwa,” alisema.
Kutokana na kupanda hadhi hiyo, Johari alisema Rais wa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani, Dk Bernard Alio atakuja Tanzania kutoa tuzo kwa Rais John Magufuli atakapoalikwa.
Pia, Johari alithibitisha kuteuliwa kwake kuwa mwenyekiti wa Afrika wa Shirika la Kimataifa la Huduma za Anga na Uongozaji wa Ndege, (Cano).
No comments:
Post a Comment