Saturday, April 28

Lema aachiwa huru, ashtakiwa upya

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (katikati) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha akiwa na Meya wa jiji hilo, Calist Lazaro baada ya kuachiwa kwa dhamana, jana. Picha Mussa Juma 

Arusha/Mikoani. Mahakama ya Wilaya Arusha jana ilimwachia huru mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema katika kesi ya uchochezi baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuwasilisha ushahidi, lakini alipandishwa tena kizimbani na kusomewa mashtaka mapya.
Hakimu Mkazi, Devotha Msofe alitoa uamuzi huo baada ya Wakili wa Serikali, Agness Hyera kuiomba Mahakama kuahirisha kesi kutokana na shahidi wa saba aliyetakiwa kutoa ushahidi jana kuwa mgonjwa.
Msofe alisema kesi ni ya muda mrefu, hivyo alimwachia Lema chini ya kifungu cha 225(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Lema aliyekuwapo mahakamani anawakilishwa na wakili Sheck Mfinanga. Katika kesi hiyo namba 440 ya mwaka 2016, mbunge huyo anadaiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 22, 2016 eneo la Kambi ya Fisi alitoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Kabla ya Januari 23, kesi hiyo ilisikilizwa kwa upande wa Jamhuri kuwasilisha mashahidi, lakini siku hiyo ushahidi wa video haukuwasilishwa kutokana na mawakili wa utetezi kuwasilisha pingamizi.
Baada ya Mahakama kumfutia mashtaka Lema, alipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi mkoani Arusha, George Katabazi akimtaka afike kituo kikuu cha polisi au Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na wadhamini wawili na mawakili wake.
Lema alikwenda mahakamani alikosomewa shitaka moja la kuamsha hisia kwa njia isiyo halali kinyume cha sheria mbele ya Hakimu Mkazi, Nestory Barro.
Wakili wa Serikali, Elianinenyi Njiro alidai Lema alitenda kosa hilo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 22, 2016 katika eneo la Kambi ya Fisi.
Anadaiwa kutamka, “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani iko siku Taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu,….
“Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya Katiba, Rais huyo ataliingiza Taifa katika majanga ya umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”
Wakili huyo alidai maneno hayo yalichochea hisia hasi kwa watu wa ngazi tofauti katika jamii. Alidai upelelezi haujakamilika.
Hakimu Barro aliahirisha kesi hadi Mei 30 na Lema alidhaminiwa na mdhamini mmoja aliyesaini hati ya Sh5 milioni.
Mbowe polisi
Mkoani Dar es Salaam, viongozi waandamizi wa Chadema waliripoti kituo kikuu cha polisi wakiongozwa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe. Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche hawakufika.
Mbali na Mbowe, wengine sita walioripoti ni Katibu Mkuu Dk Vincent Mashinji; Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika; Mhazini wa Bawacha, Esther Matiko; Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee; Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa.
Ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene alisema Mwalimu yuko Dodoma kwa majukumu ya kazi huku Heche akisema yupo msibani. Viongozi hao wanaripoti polisi kila Ijumaa kutekeleza amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyotolewa Machi 27 walipopatiwa dhamana katika kesi ya uchochezi inayowakabili.
Watatu washikiliwa Mbeya
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Mbeya, George Titho; Katibu wa Bavicha Wilaya ya Rungwe, Michael Kilaiti na Katibu wa Bavicha Kata ya Ibighi-Rundwe, Furaha Benson hadi jana mchana walikuwa wanaendelea kusota mahabusu ya kituo cha polisi Tukuyu baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia juzi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Mussa Taibu alipoulizwa alisema hawezi kuzungumzia suala hilo hadi timu ya upelelezi iliyotumwa kwenda Rungwe itakapomaliza kuwahoji.
Imeandikwa na Mussa Juma (Arusha), Pamela Chilongola na Fortune Francis (Dar) na Godfrey Kahango (Mbeya).

No comments:

Post a Comment