Saturday, April 28

SIO MIMI Mourinho ajivua lawama za kumuuza Salah


LONDON, ENGLAND
NANI alimuuza Mo Salah? Wameanza kutupiana mpira. Ni pale Stamford Bridge baada ya staa wa Liverpool, Mohamed Salah ambaye alikuwa ni mchezaji wao kuonyesha makali yasiyomithilika msimu huu katika michuano mbalimbali.
Kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho ambaye alikuwepo wakati Salah akinunuliwa Chelsea kisha kuuzwa, amejivua gamba rasmi baada ya kuendelea kutupiwa lawama na mashabiki mbalimbali ndani na nje ya Chelsea kwa kumruhusu Salah kuondoka Stamford Bridge.
Salah amefunga mabao 43 msimu huu akiwa anaongoza katika ligi kubwa tano za Ulaya, huku pia akiwa anatarajiwa kuchukua Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu ya England akiwa amefunga mabao 31 mpaka sasa huku zikiwa zimebakia mechi nne ligi kumalizika.
Staa huyo wa kimataifa wa Misri wiki iliyopita alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu huu mbele ya staa wa Manchester City, Kevin De Bruyne ambaye naye aliwahi kukipiga Chelsea kabla ya kuonyeshwa mlango wa kutokea na Mourinho.
Kelele za lawama zimekuwa nyingi zikielekeza kwa Mourinho kwa kumuuza Salah kwenda AS Roma katika dirisha kubwa la mwaka 2016 baada ya kwanza kumpeleka kwa mkopo Fiorentina kuanzia mwaka 2015.
Na sasa Mourinho amevunja ukimya na kurusha lawama zake kwa mabosi wengine wa Chelsea huku akidai yeye hausiki na kumuuza Salah badala yake apongezwe kwa kumleta Farao huyo England akitokea Basel ya Uswisi.
“Watu wanasema mimi ndiye niliyemuuza Salah lakini kumbe ni kinyume chake. Mimi ndiye niliyemleta. Mimi ndiye ambaye niliwaambia Chelsea wamnunue Salah. Ni wakati wa utawala wangu ndipo Salah alikuja Chelsea,” alijitetea Mourinho.
“Lakini alikuja akiwa kijana mdogo, kwa matumizi ya nguvu hakuwa tayari, kiakili hakuwa tayari, kwa suala la jamii na utamaduni alikuwa kama amepotea vile na kila kitu kilikuwa kigumu sana kwake,” aliongeza kocha huyo wa Manchester United.
“Tuliamua kumpeleka kwa mkopo na hata yeye mwenyewe aliomba hivyo hivyo. Alitaka kucheza dakika nyingi, kupata uzoefu, kiukweli alitaka kwenda na tulimpeleka Fiorentina, na alipofika kule alianza kukomaa,” alisema Mourinho.
Pamoja na sasa kuwa tishio huku baadhi ya wataalamu wakidai anastahili kuingizwa katika kundi la mastaa kama Cristino Ronaldo na Lionel Messi katika kugombea tuzo ya mwanasoka bora wa dunia mwakani bado Mourinho anaamini hakukuwa na kosa katika kumuruhusu Salah aondoke.
“Chelsea iliamua kumuuza. Sawa? Na wanaposema ni mimi ndiye niliyemuuza huo ni uongo. Mimi ndiye niliyemnunua. Nilikubali kumpeleka kwa mkopo kwa sababu niliona umuhimu. Chelsea ilikuwa na mawinga wengi wazuri. Wengine bado wapo pale kama vile Willian, Hazard na wachezaji wengine ambao walikuwa katika viwango vya juu.”
“Lakini kwa faida nilimnunua Salah na sikumuuza Salah. Hata hivyo haijalishi. Kitu cha msingi ni bonge la mchezaji na nina furaha kwa kila kinachomtokea kwa sasa na hasa ukizingatia hajatufunga katika mechi mbili ambazo amecheza na sisi msimu huu.”
Mourinho amekuwa akilaumiwa kwa kushindwa kuishi vizuri na wachezaji wenye vipaji huku kwa sasa akiwa katika matatizo na kiungo staa wa timu yake, Paul Pogba kwa kile kinachodaiwa staa huyo amekuwa hafuati maelekezo uwanjani.
Mourinho pia ana matatizo na beki wa kushoto wa timu hiyo, Luke Shaw ambaye naye kama ilivyo kwa Pogba wote wanahusishwa kuondoka katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto.

No comments:

Post a Comment