Saturday, April 28

Rais Magufuli akataa kuingilia mzozo



Rais John Magufuli
Rais John Magufuli 

Kondoa. Rais John Magufuli jana aliendelea kukataa maombi ya kumtaka afanye uamuzi wa papo kwa papo baada ya kuombwa amalize mgogoro wa eneo baina ya Halmashauri ya Mji wa Babati na CCM.
Rais pia aliepuka kutumia shughuli za kiserikali ya kufungua Barabara ya Dodoma-Babati, kuwapokea wanachama wa CCM baada ya kuombwa na uongozi wa chama hicho mjini Dodoma jana.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Rais kukataa kufanya uamuzi ya papo kwa papo kwenye mkutano wa hadhara baada ya kukaa ombi la kufuta hati ya balozi na wizara moja ya viwanja vilivyo karibu na jengo jipya la PSPF wakati akizindua tawi la benki ya NMB la Kambarage mjini Dodoma siku nne zilizopita.
Alitoa msimamo huo baada ya mwenyekiti wa bodi ya PSPF, Mussa Iyombe kumuomba afute hati ya kiwanja cha ubalozi wa Zimbabwe na Wizara ya Kazi na Ajira ili kitumiwe kama maegesho kwa mfuko huo, akisema hilo lingefanya eneo hilo kuwa na mandhari nzuri.
Jana, Rais alikataa ombi la kuingilia mgogoro huo baina ya Halmashauri ya Mji wa Babati, inayoongozwa na Chadema na CCM kuhusu eneo la stendi ambayo ilikuwa chanzo cha mapato cha halmashauri hiyo.
Mbunge wa Babati (Chadema), Paulina Gekul aliwasilisha ombi hilo kabla ya Rais kuzindua barabara hiyo ya urefu wa kilomita 251 katika eneo la Bicha wilayani Kondoa.
“Natumaini watu wako wamekufikishia. Maendeleo hayana vyama. Tungeomba Rais, ni ombi la wazee wa Babati bila kujali itikadi, stendi yetu ya Babati turudishiwe,” alisema Gekul.
“Sisi hatuna ugomvi na CCM, tutawapatia eneo jingine ili halmashauri yetu iendelee kukusanya ushuru pale. Kwa sababu ya muda, Rais ninajua hili lipo mezani kwako. Utusaidie ili wananchi wa Babati waweze kufanya maendeleo kupitia ushuru wa mabasi.”
Awali, kituo hicho cha mabasi kilikuwa chini ya halmashauri, lakini CCM walichukua na hivyo kuukosesha mapato mji huo.
Lakini jana, Rais Magufuli alisema hawezi kuhangaika kutafuta fedha za miradi ya maendeleo na kisha atatue migogoro ya kugombea stendi.
“Viongozi ni ninyi na wa kuamua ni ninyi. Nyie ndio mnajuana vizuri. Kwa hiyo kakaeni huko mkamalize migogoro yenu. Sio kila mgogoro kwa Rais, nitamaliza mingapi?” alihoji Magufuli.
“Viongozi waliopo washughulikie migogoro ya saizi yao, mimi nihangaike na kutafuta fedha, huku tena nihangaike na kutatua migogoro. Kama mna eneo la kuwapa CCM sasa, si mligeuze liwe stendi?”
Rais pia alikataa kutumia shughuli hiyo kisiasa baada ya kuombwa na mbunge wa Kondoa, Edwin Sanga.
Akizungumza kabla ya Rais kuhutubia, Sanga alisema kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, wanachama zaidi 800 kutoka vyama vya upinzani wamejiunga na chama hicho tawala.
Pia alisema jimbo lake lilikuwa na mitaa minne inayoongozwa na Chadema na CUF, lakini diwani mmoja wa Chadema alijiunga na CCM.
“Kama hutajali na kwa idhini yako ukiwapa mkono hapa itakuwa jambo jema sana, jamani karibu sana. Moja ya zawadi kubwa tunayokupa ni hawa viongozi, karibuni wale viongozi,” alisema Sanga.
Hata hivyo, Magufuli alikataa kufanya kazi hiyo kabla ya kuzindua barabara akisema ni kuchanganya shughuli za Serikali na siasa na kuahidi kufanya hivyo baada ya uzinduzi.
Akemea migogoro
Akihutubia katika hafla hiyo, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa Wilaya ya Kondoa kuacha ugomvi akisema umekuwa ukichelewesha baadhi ya shughuli za maendeleo.
“Nimeona niwape message (ujumbe) hii live hapahapa.mjirekebishe wote, niliowateua mimi nitawafukuza mimi. Haiwezekani Wilaya ya Kondoa kila siku ni migogoro, mara mbunge, mara nani,” alisema.
“Unakuta huyu anasema hivi, huyu anasema hivi. Acheni. Nafahamu viongozi huwa hampendi kuzungumzwa hadharani, lakini mimi huwa nazungumza tu, ndio tatizo langu. Naomba mniombee labda nibadilike lakini mimi ninapenda kuzungumza wazi ili tuelewane.”
Alisema kila mmoja amekuwa akitumia madaraka yake na kwamba wakishaelewana yeye atafahamu.
Ufisadi wa mradi wa maji
Rais Magufuli pia aliiagiza Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na vyombo vya dola kuwatafuta na kuwashughulikia watu wote waliohusika na ufisadi wa mradi wa maji wa Ntomoko.
“Hatuwezi tukawa tunaimba wakati wamechukua Sh2 bilioni na maji hakuna. Waziri Maji mkashughulikie, vyombo vya dola mpo hapa mkawashughulikie warudishe pesa zetu ama wahakikishe mradi wa maji umekamilika. Mkuu wa mkoa shughulikieni hawa,” alisema.
Kauli hiyo ilikuja baada ya mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge kusema kuwa mradi huo ulitengewa Sh2.8 bilioni mwaka 2014 na kwamba kazi hazikufanyika vizuri.
Alisema mradi huo umegubikwa na ubadhilifu wa zaidi ya Sh1.5 bilioni na Serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi imeanza kulifanyia kazi.
Rais Magufuli pia alisema Serikali haitatoa chakula kwa watu watakaolalamika njaa na kuwataka watumie vizuri mvua zinazoendelea kwa kulima.
“Mvua inanyesha halafu nije nikugawie chakula? Imenyesha miezi yote halafu itokee mwezi wa ngapi mseme hamna chakula tutakufa? Kufa,” alisema

No comments:

Post a Comment