Kauli hiyo inaakisi utaratibu wake aliojiwekea katika utendaji wa Rais Magufuli katika awamu yake.
Ripoti hizo ziliwasilishwa na kamati mbili zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuangalia uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa almasi na tanzanite.
Baada ya ripoti hizo kuwasilishwa, Waziri katika Ofisi ya Rais Tamisemi George Simbachawene amelazimika kujiuzulu baada ya kutajwa kwamba akiwa Waziri wa Nishati na Madini, aliwahi kuridhia mabadiliko katika mauzo ya kampuni uchimbaji Tanzanite na utoaji wa leseni kinyume na utaratibu.
Mwingine ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Edwin Ngonyani naye aliandika barua ya kujiuzulu baada ya kamati ya almasi kusema aliwahi kuzuia Serikali kununua mgodi wa almasi kwa dola milioni 10 na kuikosesha Serikali zaidi ya dola milioni 300, fedha ambazo zilienda kwa kampuni iliyonunua hisa.
Mtikisiko huo umekuja wakati vumbi la Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo halijatua. Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Muhongo baada ya kudaiwa kusababishia taifa kukosa mapato yake kupitia biashara ya usafirishaji wa makinikia ya dhahabu.
Hawa wote wameondolewa katika nafasi hizo, kwa makosa waliyohusishwa nayo katika uongozi wa wizara hiyo.
Wahenga walisema ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji. Msemo huo unawagusa mawaziri wengine wanaoongoza wizara nyingine na hata wale waliowahi kuziongoza wizara hizo, kwamba wakati wowote kaburi litakapofukuliwa, hakuna atakayebaki salama.
Mzimu wa Nishati na Madini
Kumbukumbu zinaonyesha ni Simbachawene pekee ndiyo alikuwa ameshikilia rekodi ya kuondoka Wizara ya Nishati na Madini bila mawaa, lakini baada ya kujiuzulu siku nne zilizopita, wizara hiyo imefuta rekodi hiyo tangu uongozi wa awamu ya tatu, nne na tano madarakani.
Simbachawene aliyeongoza wizara hiyo kwa kipindi cha miezi 10 tu, tayari amejiuzulu baada ya kutajwa na ripoti ya Kamati maalum ya Bunge kuhusisha katika kashfa ya biashara ya Tanzanite. Simbachawene amefanya wizara hiyo kufikisha idadi ya mawaziri sita walioingia na kutoka kwa kashfa wizara hiyo.
Hii inatokana na ukweli kwamba kwa miaka ya karibuni mawaziri wote wa Nishati madini tangu uongozi wa awamu ya nne 2005, Dk Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, William Ngeleja, Profesa Sospeter Muhongo, George Simbachawene wote wameondoka kwa kashfa za umeme.
Pia yupo Daniel Yona aliyekuwapo wizarani hapo katika awamu ya mwisho ya uongozi wa Rais Benjamini Mkapa, kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuchaguliwa 2005.
Yona aliyedumu kwa miaka miwili baadaye aliishia jela kwa kashfa ya zilizohusu mikataba na Kampuni ya MS Alex Stuwart iliyopewa zabuni ya kuhakiki malipo tanzania iliyostahili kutokana na mauzo ya madini.
Waliofuata
Kwa mujibu wa kumbukumbu katika wizara hiyo, Januari hadi Oktoba 2006, Wizara hiyo iliongozwa na Dk Ibrahim Msabaha ambaye baadaye alihusishwa na kashfa ya Richmond na kulazimika kujiuzulu.
Oktoba mwaka 2006 hadi 2008, wizara hiyo ikawa chini ya Nazir Karamagi ambaye alikutana na joto la kashfa ya Richmond.
Kuanzia mwaka 2008 hadi 2012, kibarua cha wizara hiyo kikakabidhiwa kwa William Ngeleja lakini naye aliondolewa katika nafasi hiyo na sakata la mawaziri mizigo, na baadaye akiwa nje akakutwa na mgawo wa James Rugemalira kwenye sakata ya Tegeta Escrow.
Nafasi hiyo kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2014 ilijazwa na Profesa Sospeter Muhongo aliyeondolewa kwa mara ya kwanza kwa kuhusishwa kwenye mzimu wa Escrow.
Januari mwaka 2015, Rais Kikwete alimteua George Simbachawene kabla ya kurejeshwa Rais John Magufuli kumrejesha Profesa Muhongo, lakini akalazimika kumwondoa tena katika sakata la Makinikia.
Akizungumzia hali hiyo, Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti (Repoa), Dk Abel Kinyondo anasema tatizo linalojitokeza katika wizara hiyo ni unyeti wa rasilimali zake kuwa chini ya uamuzi wa kiongozi mmoja.
Anatoa mfano akisema mikataba inayoingiwa katika sekta ya madini, ni ya muda mrefu na hivyo kushawishi mwekezaji na waziri mwenye dhamana kutumia njia za kona.
“Waziri anaingia wizarani akijua hataweza kukaa milele, na yeye ni binadamu anayeweza kuingiwa na tamaa, anajikuta ameshawishika kuingia mikataba itakayomnufaisha kwanza yeye,” anasema.
Dk Kinyondo anasema udhaifu katika wizara hiyo unachagizwa na Katiba na sheria zinazotoa mamlaka makubwa kwa waziri mwenye dhamana badala ya kuweka mfumo utakaokuwa na taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika upitishaji wa maamuzi ya mwisho.
“Norway hakuna kiongozi mmoja anayeweza kubadilisha au kupitisha maamuzi ya mwisho ndani ya kampuni ya usimamizi wa rasilimali. Ujerumani hakuna mwanasiasa anayeweza kuingia taasisi ya fedha na kufanya jambo fulani, hata sisi ilitakiwa waziri awe sehemu tu ya uamuzi wa mwisho, yaani tuwe na hatua mbalimbali za uhakiki wa mikataba, sheria zinazopitishwa na maamuzi ya mwisho,” anasema.
Dk Kinyondo anasema katika mazingira ya mfumo huo, hakuna waziri au kiongozi atakayeweza kuingiza udhaifu katika usimamizi, uthibiti na uendeshaji wa rasilimali za nchi.
Msingi anaoweka JPM
Mkurugenzi wa Taasisi ya Fordia, Bubelwa Kaiza anasema usafi anaouzungumzia Rais Magufuli hauishii kwa mawaziri waliopo madarakani, bali hata kwa mawaziri wastaafu na wabunge wa chama hicho atawajibishwa.
“Ndiyo maana akasema hata Bunge liangalie vizuri kanuni zake kwa wale wanaotajwa tajwa, ili Bunge litoe mapendekezo na chama chake kitaangalia namna ya kuwachuja.
Kaiza anasema ni jambo jema kujiwekea viwango na utaratibu wa viongozi anaofanya nao kazi. Mwanaharakati huyo katika sekta ya rasilimali za madini anasema kinachomsaidia ni mfumo alioanza kuweka kupitia sheria mpya ambazo zitalazimisha viongozi na mawaziri wapya wanaokuja wasiweze kumwangusha.
“Kwa mfano, Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 7 ya mwaka 2017 imeondoa mamlaka kwa waziri, katibu mkuu na kamishna wa madini katika usimamizi na udhibiti wa madini na badala yake mamlaka hayo imepewa Kamisheni ya madini itakayokuwa na wataalamu kutoka sekta mbalimbali. Hii ni hatua nzuri inayoondoa tamaa za kiongozi mmoja ndani ya wizara ya madini kuamua kwa maslahi yake,” anasema.
Hata hivyo, Kaiza anasema changamoto ilijitokeza katika mfumo uliokuwapo ambao ulikuwa wa kujinufaisha kwa viongozi wengi.
“Rais alijua wapya hawatamletea matatizo, ndiyo maana alitumia muda mrefu kuchuja wale wenye dosari na kuchukua wasiojulikana,” anasema.
Kuhusu hatma ya mawaziri wa zamani, mchambuzi huyo anasema itakuwa ni vigumu kupona endapo Rais atapita kila wizara kwa kipindi cha miaka mitatu aliyobakiza.
Kila wizara na kaburi lake
Kwa sasa ziko wizara 18 na kila moja tunaweza kusema ina kaburi lake ambalo likifukuliwa hatujui nani atakayepona.
Matatizo haya yamekuwa yakiibuliwa na mara nyingi na ripoti ya Ofisi Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na nyingine za kamati zinazoundwa na Bunge kuchunguza masuala mahususi.
Mathalan, licha ya kuondolewa kwa kashfa ya ulevi bungeni, wakati huohuo lilikuwa sakata la Lugumi lililoibua shinikizo la kung’olewa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga baada ya wizara yake kuhusishwa na zabuni tata ya mradi wa ufungaji wa vifaa vya mawasiliano kwenye vituo vua polisi.
Aidha, ripoti ya mwaka 2014/ 2015 iliyowasilishwa Aprili mwaka jana CAG Mussa Juma Assad iliibua uozo zaidi kwenye halmashauri, taasisi za Serikali na mashirika ya umma, ikibainisha kuwa nchi ina tatizo kubwa, zaidi ya watu wachache ambao wamekuwa wakishughulikiwa na Serikali ya Rais Magufuli.
Ripoti hiyo iligusa taasisi zilizowahi kuwa chini ya Wizara ya Elimu, Afya, Ardhi, Ujenzi, Mambo ya Nje na nyinginezo kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Pia ripoti hiyo inabainisha kuwa mapendekezo mengi ambayo CAG amekuwa akiyatoa kwa takribani miaka saba sasa, hayatekelezwi. Cha kujiuliza ni je, hivi yakitekelezwa nani atabaki salama?
No comments:
Post a Comment