Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekutana na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) huku uchaguzi wa marudio ambao umekumbwa na utata ukiendelea kukaribia.
Rais amekutana na Bw Wafula Chebukati katika afisi ya Bw Kenyatta katika jumba la Harambee, Nairobi.
Mwenyekiti huyo wa tume alikuwa amekutana na mgombea wa upinzani Bw Raila Odinga Ijumaa.
Bw Odinga alijiondoa kutoka kwenye uchaguzi huo wa Alhamisi akisema hana imani uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki.
Uchaguzi huo wa 26 Oktoba unaandaliwa baada ya Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi wa kwanza uliofanyika tarehe 8 Agosti ikisema kulikuwa na kasoro nyingi.
Bw Chebukati wiki iliyopita alikuwa ameitisha mkutano wa wagombea wote wa urais lakini baadaye akauahirisha na baadaye akakutana na Bw Odinga kivyake.
Alidokeza kwamba anapanga kuwakutanisha Bw Odinga na Bw Kenyatta baadaye baada kukutana na rais huyo.
Taarifa kutoka ikulu imesema Rais Kenyatta amemwambia mwenyekiti huyo kwamba yuko tayari kwa uchaguzi huo wa marudio na hana masharti yoyote kwa tume hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Naibu Rais William Ruto pia amehudhuria mkutano huo.
"Tumeweka wazi kwamba hatuna masharti wala matakwa yoyote kwa kuhusu suala hili. Tumetoa fedha za kutumiwa na IEBC kufanya kazi yake. Sasa wanafaa kfuanya kazi hiyo," amesema Rais Kenyatta.
"Tunasisitiza tu kwamba uchaguzi ufanyike tarehe 26 Oktoba, huo ndio wakati uliowekwa na IEBC kwa mujibu wa matakwa yaliyoambatana na kufutwa kwa uchaguzi wa tarehe 8 Agosti."
Mahakama ya Juu, kwenye uamuzi wake ilikuwa imeagiza uchaguzi mpya ufanyike kwa kufuata katiba na sheria kikamilifu katika muda wa siku 60.
IEBC awali ilikuwa imetangaza uchaguzi mpya ufanyike tarehe 17 Oktoba lakini baadaye ikaahirisha tarehe hiyo hadi 26 Oktoba baada ya moja ya kampuni zilizokuwa zikitoa huduma muhimu kwa ajili ya uchaguzi huo kusema hazingekuwa tayari wakati huo.
Bw Odinga amekuwa akiitaka IEBC kuahirisha uchaguzi huo na ametangaza kwamba tarehe hiyo "hakutakuwa na uchaguzi".
Kumekuwa na utata kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo hasa baada ya kujiuzulu kwa mmoja wa makamishna wa tume hiyo Dkt Roselyn Akombe wiki iliyopita.
Dkt Akombe alisema anaamini tume hiyo haina uwezo wa kuandaa uchaguzi huru na wa haki Alhamisi.
Lakini maandalizi ya uchaguzi huo yamekuwa yakiendelea.
Shehena ya kwanza ya karatasi za kupigia kura iliwasili Jumamosi na shehena nyingine inatarajiwa kufika Nairobi baadaye leo.
Wakuu wa IEBC
Mwenyekiti: Wafula Chebukati
Naibu Mwenyekiti: Consolata Nkatha Maina
Makamishna:
- Boya Molu
- Paul Kibiwott Kurgat
- Abdi Guliye
- Margaret Wanjala Mwachanya
Afisa Mkuu Mtendaji/Katibu: Ezra Chiloba
Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilimtangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, akiwa mbele ya mpinzani wake Raila Odinga wa muungano wa upinzani Nasa kwa zaidi ya kura 1.4 milioni.
Bw Odinga alipinga matokeo hayo mahakamani na Mahakama Kuu ikaamua ulijaa kasoro nyingi na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku sitini.
No comments:
Post a Comment