Monday, October 23

Myeshia Johnson: Mjane asema Trump hakukumbuka jina la mumewe

Myeshia Johnson Hollywood, Florida 21 OktobaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionMyeshia Johnson akitokwa na machozi akilibusu jeneza la marehemu Hollywood, Florida
Mjane wa mwanajeshi wa Marekani aliyeuawa nchini Niger amesema kuwa alikasiriswa na simu ya pole aliyopigiwa na Rais Donald Trump kwa sababu alionekana kutatizika kulikumbuka jina marehemu mumewe.
Bi Myeshia Johnson mjane wa Sajini La David Johnson ameambia shirika la habari la ABC kwamba kubabaika kwa Rais Trump "kulimuumiza zaidi."
Lakini Bw Trump amejitetea na kusema kwamba alikumbuka na kulitaja jina la Sajini Johnson "bila kusita" na akaeleza mazungumzo kati yake na mjane huyo kwa simu kama ya "heshima sana."
Sajini Johnson aliuawa na wanamgambo wa Kiislamu nchini Niger mwezi huu.
Simu hiyo ya pole ya Trump iligonga vichwa vya habari baada ya mbunge wa Democratic Frederica Wilson aliyeisikiliza pamoja na familia ya mwanajeshi huyo kusema haikuwa na utu.
Myeshia Johnson alionekana kukariri madai ya Bi WIlson kwamba Bw Trump alimwambia mumewe alijua hatari aliyokuwa akijiingiza kwake alipojiunga na jeshi.
Sgt La David JohnsonHaki miliki ya pichaUS ARMY
"Rais alisema alifahamu (Johnson) alikuwa anajiunga na nini, lakini inaumiza...Ilinifanya nilie na kukasirika sana kutokana na alivyoyasema hayo," alisema mjane huyo.
"Alikuwa na ripoti kumhusu mume wangu mbele yake, na hapo ndipo aliposoma La David. Nilimsikia akibabaika akijaribu kulikumbuka jina la mume wangu.
"Iwapo mume wangu alikuwa huko akipigania taifa letu na aliweka maisha yake hatarini kwa ajili ya taifa letu, ni kwa nini hukumbuki jina lake?" aliongeza.
Trump amesemaje?
Rais Trump alijitetea Jumatatu kwenye Twitter na kusema kwamba alitaja jina la mwanajehsi huyo mwanzoni mwa mazungumzo bila kusita.
Amepuuzilia mbali tuhuma za Bi Wilson akisema ni za uongo.
Trump alisema ana ushahidi kwamba madai hayo ni ya uongo lakini hajatoa ushahidi huo.
Ikulu ya White House ilisema mazungumzo ya Trump na jamaa za wanajeshi waliouawa ni ya faragha.
Donald TrumpHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionTrump amekosolewa sana kwa madai yake
Mzozo ulianza vipi?
Sajini Johnson alikuwa mmoja wa wanajeshi wanne wa Marekani waliouawa katika shambulio la kuvizia Niger 4 Oktoba.
Trump alikosolewa kwa kutowasiliana na jamaa za wanajeshi hao punde baada yao kuuawa.
Alijitetea akisema kwamba hata mtangulizi wake Barack Obama na marais wengine hawakuwa wanawasiliana na jamaa za marehemu, madai ambayo si ya kweli.
Mzozo uliziki Trump alipodai Obama hakupigia simu jamaa za mkuu wa utumishi wa Trump Jenerali John Kelly mwaa wao wa kiume alipouawa akiwa Afghanistan.
White House baadaye ilisema alizungumza na jamaa za waliouawa Niger lakini haikusema ni lini.

No comments:

Post a Comment