Monday, October 23

Mwigamba aeleza sababu za kutohudhuria kikao ACT -Wazalendo


Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa ACT -Wazalendo, Samson Mwigamba ametaja sababu mbili zilizomfanya kukataa wito wa kikao cha Kamati ya Uongozi ya chama hicho kwa ajili ya mahojiano.
Jumamosi Oktoba 21,2017 Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliwaeleza waandishi wa habari kwamba Kamati ya Uongozi ya chama hicho, ilimwita Mwigamba ili atoe maelezo baada ya kukituhumu chama hicho kukiuka misingi yake lakini hakufika.
Zitto alisema kamati hiyo baada ya kukutana na kujadiliana ilibaini hakuna misingi iliyokiukwa.
Mwigamba aliyekihama chama hicho na kujiunga na CCM, leo Jumatatu Oktoba 23,2017 amesema hakuona jambo jipya litakalojadiliwa dhidi yake katika kikao cha Kamati ya Uongozi kwa kuwa mengi aliyoyalalamikia alishayatolea ufafanuzi kwenye barua yake ya kujiuzulu.
Amesema jambo lingine lililomfanya kutohudhuria kikao hicho ni Kamati ya Uongozi kuwa na wajumbe 12 badala ya watano waliopo kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Ado Shaibu amesema hawana muda wa kulumbana na Mwigamba na wanaheshimu uamuzi wake wa kujiuzulu, hivyo wanamtakia kila la kheri kwenye safari yake ya kisiasa.

No comments:

Post a Comment