Ameieleza Mahakama Kuu kwamba, kama Kanumba asingefariki dunia, basi yeye ndiye angekufa kwa kuwa mpenzi wake huyo alikuwa amelewa na alimshambulia kwa kumpiga kwa ubapa wa panga, huku akimtishia kumuua kutokana na wivu wa mapenzi.
Lulu ameeleza hayo mahakamani leo Oktoba 23,2017 alipotoa utetezi katika kesi ya kumuua bila ya kukusudia inayomkabili. Anadaiwa Aprili 7,2012, nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam alimuua msanii huyo.
Msanii huyo alijitetea baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne na Jaji Samu Rumanyika kutoa uamuzi kwamba ana kesi ya kujibu.
Lulu akiongozwa na wakili Peter Kibatala kutoa ushahidi, amedai alifika nyumbani kwa msanii huyo saa sita au saa sita kasoro usiku baada ya Kanumba kumwita.
Alipofika nyumbani kwa Kanumba amedai alikuta mlango haujafungwa kwa kuwa awali aliwasiliana naye kwa simu na alimweleza anauacha wazi kwa kuwa alikuwa anakwenda kuoga.
Amesema alipofika chumbani kwa Kanumba alikuta akipata nywele mafuta na alikuwa amewekasuper black. Amedai kulikuwa na pombe kali aina ya Jack Danile’s na soda aina ya Sprite ambavyo mpenzi wake huyo alikuwa akinywa.
Lulu amedai akiwa amekaa kitandani, simu ya Kanumba iliita na kupitia mazungumzo alibaini aliyepiga alikuwa msanii wa muziki, Chalz Baba.
Amesema baadaye aliaga kwamba anaondoka kwa kuwa rafiki zake walikuwa wakimsubiri lakini Kanumba alimzuia akimweleza anataka watoke pamoja kwenda kwenye muziki wa dansi lakini alikataa kwa kuwa si mpenzi wa aina hiyo ya muziki aliosema anauona kuwa wa wazee.
Lulu amedai rafiki zake walimpigia simu lakini aliogopa kuipokea kwa kuwa alijua wangemuuliza kwa nini harudi, hivyo aliaga anakwenda kuchukua maji na alipotoka nje ya chumba aliipokea simu.
Amesema alipokuwa akimaliza mazungumzo kwenye korido, Kanumba alifungua mlango na kumuuliza alikuwa anazungumza na nani naye akamjibu kuwa ni rafiki zake.
Amedai alipomfuata alirudi nyuma akihofia kupigwa akidai alipokuwa amelewa Kanumba alikuwa mwenye kukasirika hata kwa vitu vya kawaida na kwa mara kadhaa alikuwa akimpiga kwa sababu hizo hata mbele za watu.
Lulu amedai alifungua mlango akatoka ndani na wakati huo Kanumba alikuwa amevaa taulo pekee, hivyo alijua asingeweza kumfuata.
Hata hivyo, amedai alimfuata na hata alipofungua geti na kukimbia kwenda kujificha kwenye baa ya Vatican bado alimfuata.
Lulu amedai baa hiyo haikuwa ikitumika na kwamba, licha ya giza Kanumba alimuona na alimpiga vibao na kumrudisha ndani nyumbani.
Amedai alikataa kuingia ndani akijua angepigwa zaidi lakini mpenzi wake huyo alimburuza na kumvuta hadi chumbani ambako alifunga mlango, akamtupa kitandani akaendelea kumpiga vibao.
Lulu amedai Kanumba alikuwa akilalamika kuwa alimsikia akizungumza kwa simu na mwanamume mwingine mbele yake na kwamba, alitoa panga uvunguni na kumpiga nalo mapajani kwa ubapa.
Amedai wakati Kanumba akimpiga aliziba uso kwa mikono yake na alisikia panga likianguka na sauti kama ya mtu aliyekabwa.
Lulu amedai alipoondoa mikono usoni alimwona Kanumba akiwa amejigonga ukutani na alijaribu kuinuka lakini akajigonga tena.
Amedai alikimbilia chooni ili kujiokoa, ambako alijifungia na akawa anapiga kelele kuomba msaada.
Akiwa chooni, amedai alisikia kishindo cha mtu aliyeanguka au aliyebamiza mlango na kisha kimya kikitawala.
Lulu amedai alidhani Kanumba alitoka ndani na kubamiza mlango kwa hasira, hivyo akaamua kutoka ili akimbie lakini alimuona Kanumba akiwa amelala chini kimya.
Amedai alidhani Kanumba alijifanya kazimia baada ya yeye kupiga kelele kuomba msaada. “Nilimwambia kuwa hata kama ukijifanya kuzimia akija mtu nitamwambia kuwa umenipiga na ulitaka kuniua,” amedai Lulu.
Amesema baada ya kuona kimya aliingia bafuni alikochukua maji na kumwagia Kanumba ambaye hakuamka, ndipo alipokwenda kumweleza Seth, ambaye ni mdogo wa Kanumba.
Lulu amedai Seth alipomuangalia Kanumba alimwita daktari wake ambaye alimwambia amfuate. Amedai Seth alimtaka abaki pale lakini alikataa kwa sababu alihisi akipata fahamu angeweza kumkata kwa panga, hivyo Seth alipoondoka naye akaondoka.
Lulu amesema alipokamatwa kwa msaada wa daktari wa Kanumba alipelekwa kituo cha polisi ambako alifanyiwa mahojiano katika vyumba vinne tofauti.
Amedai Aprili 8,2012 aliamka na kuhisi maumivu ya kipigo hivyo polisi walimpeleka katika Hospitali ya Mwananyama ambako alipatiwa matibabu.
Alipouliwa na wakili Kibatala kuhusu shtaka linalomkabili la kumuua Kanumba bila kukusudia au kusababisha kifo chake, Lulu alikana akisema hajawahi kusababisha kifo bali yeye ndiye alikuwa anashambuliwa kwa panga na asingeanguka basi huenda yeye ndiye angeuawa.
Lulu alipoulizwa na Wakili wa Serikali, Faraja George ni kwa nini hakuomba msaada kwa watu wengine katika nyumba hiyo na badala yake alikimbia nje, alijibu pamoja na kujiepusha pia alitaka kumfichia mpenzi wake aibu.
Baada ya Lulu kumaliza kutoa ushahidi, Jaji Rumanyia aliahirisha kesi hiyo hadi kesho Oktoba 24,2017 itakapoendelea kwa upande wa utetezi na kisha majumuisho ya hoja za mwisho za mawakili.
Lulu ambaye yupo nje kwa dhamana pia anatetewa na mawakili Fulgence Massawe na Omary Msemo.
No comments:
Post a Comment