Thursday, May 23

Umefika wakati wa kubadili muundo wa Tanesco


ahitaji ya umeme kwa wateja wake ni Megawati 906, lakini uwezo wake ni kuzalisha 705 tu. Megawati hizo zinazalishwa kupitia mabwawa ya Kidatu (204), Kihansi (180), Mtera (80), Pangani (68), Hale (21) na Nyumba ya Mungu (8).
Jana bungeni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka huu wa fedha na ndani ya hotuba yake alielezea hali mbaya ya Tanesco akisema inadaiwa zaidi ya Sh900 bilioni.
Haishangazi kusikia Tanesco ina hali mbaya kifedha, kwa sababu tangu shirika hilo lianzishwe mwaka 1964, limeshindwa kutoa huduma ya umeme kwa walau nusu ya Watanzania, hata hao waliounganishiwa, hawapati umeme wa uhakika.
Wizara inayoisimamia Tanesco imeshaongozwa na mawaziri 21 na makatibu wakuu 18. Hoja za baadhi yao ni shirika hilo kuzidiwa kimajukumu, ikiwamo mzigo wa madeni.
Katibu Mkuu aliyepita, David Jairo hakutafuna maneno aliposema hali ya Tanesco ni mbaya, mapato yake ya mwezi hayazidi Sh30 bilioni, wakati kwa siku inatumia Sh566 milioni kuwalipa Songas na IPTL.
Kwa mfano, mahitaji ya umeme kwa wateja wake ni Megawati 906, lakini uwezo wake ni kuzalisha 705 tu. Megawati hizo zinazalishwa kupitia mabwawa ya Kidatu (204), Kihansi (180), Mtera (80), Pangani (68), Hale (21) na Nyumba ya Mungu (8).
Umeme mwingine ni wa nguvu za mitambo iliyopo katika Vituo vya Tanesco vya Ubungo, Megawati 100 na Tegeta 45. Wakati uzalishaji wa umeme ni megawati 705, mahitaji ya Dar es Salaam pekee, ni Megawati 455. Profesa Muhongo ambaye ni waziri wa 21 katika wizara inayoongoza Tanesco, kwenye hotuba yake ya kwanza kwenye Bunge la Bajeti la mwaka jana, alizungumzia hoja ya kuinusuru Tanesco kwa kuipa ruzuku. Hata hivyo, msaada wa ruzuku ya Serikali kwa Tanesco umeonekana kutofua dafu.
Profesa Muhongo ameshawahi kukaririwa akitaka marekebisho makubwa katika shirika hilo, hoja ambayo inaungwa mkono na wananchi wengi. Kwa mfano, wananchi wa Wilaya ya Bunda, Mara wakizungumza kwenye mkutano wa wadau wa umeme walitamka bayana kuwa shirika hilo limezidiwa. Walisema limebeba mzigo mkubwa wa kuzalisha umeme, kuuza na kusambaza.
Ufanisi wa Tanesco umegubikwa na ‘umwinyi’ unaochangia kulidhoofisha, wateja wanaoomba kuunganishiwa umeme hawapewi huduma hiyo kwa wakati, kumekuwa na ulegevu wa ufuatiliaji madeni kwa wateja na hujuma nyingine zinafanywa na wafanyakazi wenyewe.
Kumekuwa na mianya mingi ya hujuma za mapato ya Tanesco, kumekuwa na tatizo la ‘vishoka’ wa kuunganisha umeme na wanaouza Luku na wote hao wana uhusiano na baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco.
Pamoja na kuiona Tanesco kwamba imekuwa mzigo, bado kuna waliolifikisha shirika hilo hapo, Serikali na taasisi zake ni mojawapo na kwa kiasi kikubwa hawawezi kukwepa lawama.
Siyo siri, Serikali imekuwa mdaiwa mkubwa wa Tanesco na kutolipa hayo kumechangia kulidhoofisha shirika hilo kimapato.
Tunadhani kwamba hakuna haja ya kuendelea kuibebesha Tanesco mzigo wa kuzalisha umeme, kuuza na kusambaza. Ni wakati sasa kwa Serikali kulivunja shirika hilo ili kulipunguzia mzigo wa majukumu lakini pia kuongeza ufanisi kwa kuleta ushindani katika sekta ya nishati.
Wakati mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ukiendelea bungeni, tungependa kuwashauri wabunge kuishauri Serikali kubadili muundo wa shirika hilo ili Watanzania wengi ambao ni zaidi ya milioni 40 waweze kunufaika na huduma ya umeme.

No comments:

Post a Comment