Pamoja na kwamba hali ni mbaya katika kundi hilo, lakini Tanzania kwa ujumla maambukizi yameshuka kwa asilimia 0.4 na kufikia asilimia 4.7 kutoka asilimia 5.1 ya utafiti uliofanyika 2011/2012.
Matokeo hayo yanatokana na utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS) ya mwaka 2016/2017 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambao umeonyesha kuwa jumla ya Watanzania 1.4 milioni (sawa na asilimia 2.9) wanaishi na virusi vya Ukimwi.
Utafiti huo uliofanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na kuhusisha kaya 14,811 zinaonyesha kuwa vijana walio kwenye umri huo (15-24) wengi wao wakiwa wasichana wanapata maambukizi mapya.
Takwimu hizo zimeonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15-19 ni asilimia 0.7 ambapo asilimia 1.0 ni watoto wa kike na asilimia 0.4 ni watoto wa kiume.
Kwa vijana wenye umri wa miaka 20-24 kiwango hicho kimeongezeka na kuwa asilimia 2.2 wasichana wakiwa ni asilimia 3.4 na wanaume ni asilimia 0.9.
Kiwango kimezidi kuongezeka na kufikia asilimia 4 kwa watu wenye umri wa miaka 25-29 wanawake wakiwa asilimia 5.6 na wanaume ni asilimia 2.3.
Akielezea sehemu ya utafiti huo Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa alisema ukubwa wa maambukizi ni wastani wa asilimia 4.7 wanawake wakiwa asilimia 6.5 na wanaume asilimia 3.5
Alisema ripoti hiyo inaonyesha maambukizi ya VVU kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 ni asilimia 1.4, wasichana wakiwa ni asilimia 2.1 huku wavulana wakiwa asilimia 0.6.
Maambukizi ya VVU kwa watu wazima wenye miaka 15 hadi 64 yako juu kwa wanawake kwa asilimia 6.5 ikilinganishwa na asilimia 3.5 ya wanaume.
Kiwango cha maambukizi kwa watoto walio chini ya miaka 15 ni asilimia 0.4
Takwimu hizo zinaonyesha Mkoa wa Njombe unaongoza kwa kuwa na asilimia 11.4 ya maambukizi ya Ukimwi ukifuatiwa na Iringa yenye asilimia 11.3 huku Lindi ikiwa ni mkoa wenye maambukizi machache zaidi kwa asilimia 0.3.
Kwa upande wa Dar es Salaam, Dk Chuwa alisema kiwango cha maambukizi ya Ukimwi katika ripoti hiyo mpya ni asilimia 4.7.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo kasi ya maambukizi ni kubwa zaidi kwa wanaoishi mijini kwa asilimia 6 ikilinganisha na asilimia 4.2 ya watu wanaoishi vijijini.
Kufuatia hali hiyo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaasa wanajamii kubadili mienendo wa maisha yao na kutambua kuwa Ukimwi ni tishio hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari kujiepusha na ugonjwa huo.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika Uwanja wa Mnazi Mmoja jana, Samia aliwataka wasichana kutokubali kurubuniwa kwa sababu ya njaa ya siku moja.
Mama Samia alisema, “naomba wasichana wabadilike Ukimwi ukikutesa hautakutesa peke yako bali Taifa zima, takwimu hizi zinaonyesha hali si nzuri kwa kundi hili ambalo ndilo nguvu kazi ya Taifa, mjitahidi muwe na mienendo inayoeleweka.”
Samia aliwageukia pia wanaume waharibifu na kuwasihi kuzingatia maadili na kuwaacha watoto wa kike wasome na kuja kulisaidia Taifa baadaye.
“Tunaona maambukizi kwa vijana hasa wa kike yanaongezeka, tunaweza kujiuliza wanapata wapi jibu ni kwamba wanapata kwa wanaume. Kuna wanaume watu wazima kabisa ambao wamezunguka huko na hatimaye wanatua kwa watoto na kuwapelekea maradhi yao, huo ni uuaji,” alisema.
Kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-19, maambukizi yapo chini kwa asilimia 0.7 na yako juu kwa wanawake wenye miaka 45-49 kwa asilimia 12.0.
Upande wa wanaume maambukizi hayo ni makubwa kwa wenye umri kati ya miaka 40 hadi 44 kwa asilimia 8.4 ikilinganishwa na miaka 55 hadi 59.
Takwimu hizo zilimsukuma Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Leonard Maboko kuanzisha kampeni maalumu kwa ajili ya wanaume kuwahamasisha kupima na kuanza kutumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi.
Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na janga hilo ikiwa ni pamoja na kutoa dawa kwa watu wote waliopimwa na kugundulika wana VVU.
Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi na endelevu ya kondomu na kuzisambaza bila malipo kupitia vituo vya huduma za afya.
Alisema, “katika kuendelea kudhibiti maambukizi kwa makundi maalumu, wizara inafanya majaribio ya namna ya kutumia ARV kujikinga na VVU kwa walio katika hatari zaidi ya kuambukizwa, ingawa hii sio mbadala wa njia nyingine za kujikinga.”
“Mafanikio katika mapambano dhidi ya Ukimwi yanaakisi mafanikio ya nchi katika kutekeleza lengo namba tatu la maendeleo endelevu hivyo tutahakikisha tunaendelea kutekeleza maendeleo hayo ili ifikapo 2020 malengo ya 909090 Tatu yanafikiwa na kuchangia malengo ya kutokomeza Ukimwi duniani ifikapo 2030,” alisema Dk Ndugulile.
No comments:
Post a Comment