Saturday, December 2

Kenya ina majeraha, nani ataiponya?


Novemba 28, katika Jiji la Nairobi, Kenya taswira mbili zilitawala; Upande mmoja ulikuwa umejaa machafuko, milio ya bunduki, mabomu ya machozi, damu, majonzi na maombolezo. Pia, uharibifu wa mali ulikuwa mwingi mno.
Kwa upande mwingine, shangwe na vigelegele vilitawala huku wageni waalikwa na maelfu ya wafuasi wa Jubilee wakisherehekea hafla ya kuapishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta katika Uwanja wa Kasarani, Nairobi.
Jua lilipotua siku hiyo watu watatu walikuwa wameuawa miongoni mwao mtoto wa miaka saba katika makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa Muungano wa Nasa wanaokataa ushindi wa Kenyatta.
Muungano wa Nasa walikuwa wanajitayarisha kumkaribisha kiongozi wao, Raila Odinga kuwaongoza kwenye mkutano wa hadhara wa kuomboleza watu zaidi ya 57 waliopoteza maisha yao mikononi mwa polisi katika visa mbalimbali vya kisiasa kati ya Agosti 8 na Novemba 26.
Agosti 8 ndiyo tarehe ulipofanyika uchaguzi ambao ulikumbwa na kasoro nyingi na baadaye kubatilishwa na Mahakama ya Juu ya Kenya, wakati Novemba 26 ndipo ulifanyika uchaguzi wa marudio wa Rais na Uhuru kuibuka mshindi baada ya Odinga kuususia.
Baadhi ya watu waliuawa wakati Uhuru akiapishwa. Miongoni mwa waliouawa kwa kupigwa risasi ni mtoto Geoffrey Mutinda.
Wafuasi wengine upinzani wanadaiwa kuuawa katika kati ya polisi na wafuasi wa Nasa waliokuwa wanamlaki Raila aliporejea kutoka ziara ya siku 10 ughaibuni.
Wengine waliuawa katika mitaa ya mabanda na kuleta msisimko mkubwa wa vuguvugu la upinzani kuzidisha wito wao wa kutaka kuanza kile wanachokiita ukombozi wa tatu wa Kenya. Wafuasi na viongozi wa Nasa wanasema hawahisi kuwa ni Wakenya kwa jinsi wanavyohangaishwa na polisi na Serikali ya Jubilee.
Wanasema kuwa Katiba inakubali Wakenya wote kukutana mahala popote bora tu wamemwarifu mkuu wa polisi katika eneo wanapokutana, lakini licha ya Nasa kufuata sheria kwa kuwaarifu polisi kuhusu mikutano yao, hakuna siku wamekubaliwa kukutana.
Wiki jana, Raila aliongoza mchango wa kusaidia familia ya waliofiwa. Kiongozi huyo alipotoa machozi alipokumbuka maisha ya waliopotea kwa sababu ya siasa. Polisi wameendelea kuwa kizingiti kikubwa kwa juhudi za kuwaleta Wakenya pamoja na kudumisha amani na utangamano.
Popote wanapotumwa lazima wamwage damu. Mbaya zaidi ni kwamba hata watoto wameathiriwa kwa kuwa polisi hawachagui mtu mzima wala mtoto wanaporusha risasi. Visa hivi ni sawa na kunajisi Katiba.
Wengi wanasema polisi waliouwa na kujeruhi sharti wachukuliwe hatua za kisheria. Hatuwezi kuendelea kuishi na hofu katika nchi yetu ilhali tulipata uhuru 1963.
Baadhi ya Wakenya wamechoshwa na virumai za kila mara na wengine wao wanashangaa kwa nini walipigania huru kumfukuza mkoloni mweupe ilhali bado kuna watu weusi ambao ni wakatili kupita kisasi. Viongozi hawajali maisha—kile wanachokienzi ni uongozi. Lakini swali ni je, kukitokea vita vya kukata na shoka, viongozi hao watawaongoza nani? Wahenga walisema, vita havina macho na asiyeziba ufa atajenga ukuta.
Serikali ikiendelea kupuuza vifo hivi na hasara ya kila siku zinazosababishwa na malumbano, siku moja, na haitakuwa mbali, nchi inaweza kukumbwa na visa ambavyo vitakuwa vigumu kuvikomesha.
Kila mtu akijipiga kifua bila kujali matokeo ya matendo yake mwishowe itakuwa kulia na kusaga meno.
Wafuasi na viongozi wa Nasa wanasema hawahisi kuwa ni Wakenya kwa jinsi wanavyohangaishwa na polisi na Serikali ya Jubilee. Wanadai kuwa Katiba inakubali Wakenya wa tabaka zote kukutana mahala popote.
Kama ilivyofanyika kwa mikutano mingine ya hapo awali ya Nasa, Raila na viongozi wakuu wa upinzani walitimuliwa walipofika uwanja wa Jacaranda, Nairobi kuongoza maombolezo. Lakini, kwanza kiongozi huyo alitangaza uamuzi wa utata kuwa ataapishwa Desemba 12. Lakini je, ataapishwaje ilhali Katiba ina utaratibu wa jinsi Rais anafaa kuapishwa?
Wiki jana, kiongozi mwenza wa Nasa, Musalia Mudavadi alipohutubia wanahabari aligusia suala hilo la kuapishwa kwa Raila lakini muda mfupi baadaye, Raila alisema hakubaliani na matamshi hayo kwa sababu ni kinyume cha sheria.
Baadaye Raila na viongozi hao waliwakwepa maafisa wa polisi waliokuwa wanawafuata na kufika katika mtaa wa Mabanda wa Kibra ambako hali iliyojitokeza ni kwamba Kenya bado inaumia na suluhu ya tiba inahitajika haraka iwezekanavyo.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliongeza mafuta kwenye moto aliposema watu hawali siasa. Museveni angenyamaza na kuwaacha Wakenya watafute suluhisho la matatizo yao. Kiongozi huyo wa Uganda hana haki ya kuwashauri Wakenya ambao hawajasahau kwamba alishindwa kuipatia Kenya mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Uganda badala yake ukaenda Tanzania. Wanaona sasa anawapaka mafuta kwa mgongo wa chupa.
Museveni alikuwa anahutubia halaiki ya watu waliosafirishwa na Jubilee kutoka maeneo yaliyompigia kura Uhuru, kwenye uwanja Kasarani, Nairobi.
Yeye mwenyewe hula, huota na hulala akifikiria siasa. Tafadhali Museveni atuache na shida zetu kwa sababu wewe si mfano mzuri wa kuigwa na wengine.
Ulimwengu wote unajua kuwa amemhangaisha kiongozi wa upinzani Uganda, Dk Kizza Besigye kwa miaka mingi, lakini hiyo si stori yetu leo.
Siasa mbaya, maisha mabaya. Kenya huenda ikaendelea kuzama zaidi kwenye hili, lakini kusema ukweli, ushauri huu wa Museveni ni potofu kwa sababu twamjua; amekuwa akila siasa tangu 1986 alipochukua hatamu za uongozi baada ya kumtimua Milton Obote. Nitatofautiana na kiongozi huo wa Uganda kwa sababu Wakenya hawawezi kutambua ushauri wake.
Rais Uhuru aliapa kuwa atahakikisha Wakenya wote wanatimiza ndoto zao. Pia, aliahidi kuwa atafanya kila aliwezalo kuhakikisha kuwa amewaleta Wakenya wote pamoja. Watu watatu walifariki dunia kwenye visa vya polisi kukabiliana na wafuasi wa Nasa waliokuwa wamefika katika uwanja wa Jacaranda yapata kilomita 12 mashariki mwa jiji la Nairobi.
Si ajabu wafuasi wa Nasa waliona cha mtema kuni. Nasa ilikaidi amri ya polisi kwamba mkutano wao wa maombolezo uahirishwe hadi siku nyingine kwa sababu Rais Uhuru alikuwa anaapishwa.
Tayari, kitumbua kimeingia mchanga kwa sababu upinzani na serikali ya Jubilee hawapatani kwa lolote lile wanalogusia. Kila mmoja anataka kuonekana ana ujasiri kuliko mwenzake, lakini ameshika mpini Raila ameshika makali.
Bado upinzani umeapa kuwa kamwe hawatamtambua Rais Uhuru kama kiongozi wao. Wanasisitiza wataweka shinikizo hadi uchaguzi mwingine ufanywe ndani ya siku 90. Raila amesisitiza kuwa yeye haogopi lolote na ataapishwa Desemba 12.
Siku hii ni sikukuu kwa Kenya kwa sababu ni siku ambayo nchi inaadhimisha siku ya kujinyakulia madaraka kutoka kwa mikono ya wabeberu.
Raila amechagua siku hii kuashiria ukombozi wa Kenya ambao umekuwa pambio kwa Nasa tangu Agosti 8 ambapo ushindi wa Uhuru ulipingwa na majaji kuamua kwamba uchaguzi haukufanyika kwa njia inayofaa.
Hii itakuwa vigumu mno kwa sababu Rais Uhuru ameshakula kiapo cha muhula wa pili na wa mwisho. Je, Nasa itatetea vipi lengo lao la kutaka uchaguzi mwingine ufanywe? Rais Uhuru alipokuwa akiapishwa, Nasa ilikuwa inapanga jinsi ya kuvuruga utawala wake. Hii haitakuwa rahisi kwa Nasa na Wakenya zaidi watakufa kabla siku zao kufika.
Je, Wakenya wasio na hatia watauawa hadi lini? Mbona damu imwagwe usiku na mchana ilhali Katiba ya Kenya inawapa wananchi uhuru kuandamana ilimradi tu wawajulishe polisi wanapotaka kuwa na mkutano.
Wafuasi wa Nasa ndio sasa wanamwamuria Raila kutekeleza wanachotaka. Hii inadhihirika wakati Raila aliposema hataki kuapishwa na baadaye kutangazwa kuwa ataapishwa kuwa rais wa Kenya kulingana na matokeo ya kura ya Agosti 8 ambayo hata hivyo Kenyatta ndiye alitangazwa mshindi.
Wafuasi wa Raila wana kiu cha kufika nchi mpya yenye maziwa na asali. Kiongozi wao Raila amewaahidi watafika nchi hiyo inagawa kuna matatizo mengi safarini. Ni matumaini yao kwamba watafika nchi hiyo kwa vyovyote vile.
Uhuru anasema atakuwa Rais wa Wakenya wote bila kujali misingi ya kabila wala chama. Lakini, vitendo vilivyoonekana hata kabla sherehe ya kuapishwa kwake kumalizika ni tofauti kabisa.
Mazungumzo ya kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za kisiasa, yamepingwa mara kwa mara na upinzani lakini baadhi ya makanisa yanasema lazima kuwe na hali kama hii ili nchi isonge mbele. Muungano huo wa upinzani unasema hauwezi kukubali kugawana mamlaka kwa sababu ni washindi wa kura “iliyoibwa na Jubilee.”
Rais anawasihi viongozi wa Nasa waungane na kufanya kazi lakini wito wake ni kama mhubiri kuhubiria watu waliookoka. Ni kazi bure.

No comments:

Post a Comment