Saturday, December 2

Rushwa na ufisadi si ajenda pekee ya upinzani


Hivi karibuni mwanasiasa mmoja amehamia CCM kwa madai kuwa eti ajenda ya rushwa ya chama alichotoka sasa inashughulikiwa kikamilifu kabisa na CCM.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Tuki, Oxford, Toleo la 3 ukurasa 484 inaelezea neno rushwa kuwa ni fedha au kitu cha thamani kinachotolewa na kupewa mtu mwenye madaraka ya jambo fulani ili mtoaji apewe upendeleo. Yaani hongo, mrungura au kadhongo. Lakini neno linalovuma zaidi siku hizi ni ufisadi. Kamusi niliyoirejea hapo juu punde tu inaelezea neno hili kwa maana tatu. Kwanza ni tendo la kuleta maovu au uharibifu katika jamii, pili, upokeaji au utoaji wa hongo; na tatu, ni wizi wa mali ya umma au Serikali. Kenya walianza kulitumia neno ufisadi kwa nguvu zaidi katika kashfa ya Goldenberg iliyoikumba nchi hiyo takriban miongo miwili iliyopita.
Neno ufisadi linatokana na kitenzi fisidi, ambacho kinaelezwa na kamusi hiyo kuwa ni kufanya uharibifu au ubadhirifu, iba mali ya umma, tumia kwa njia mbaya, haribu, potoa na hujumu.
Kwa kifupi basi ufisadi unajumuisha rushwa ya juu kabisa, kwa kimombo, grand corruption.
Ibara ya 9(c) ya Katiba ya Tanzania inasema kuwa; mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vitawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mwingine.
Pili, mwanasiasa yule aliyehamia CCM yafaa amaizi kwamba hakuna chama cha siasa chenye ajenda moja tu duniani. Siku zote ajenda hubadilika kulingana na nyakati zilizopo. Mathalan sasa hivi ajenda kuu kabisa ya upinzani ni kudai Tume Huru ya Uchaguzi ili kupata demokrasia ya kweli nchini hususan katika chaguzi zote kuanzia udiwani, ubunge hadi urais.
Chaguzi zote za kweli duniani lazima zifanyike chini ya usimamizi wa Tume Huru za Uchaguzi. Sharti hili ni muhimu ili kuepuka upendeleo wa dhahiri au uliofichika kwa chama chochote kile kinachoshiriki uchaguzi husika.
Na hakika msingi wa sharti hili si utashi tu wa binadamu. Ni kutekeleza moja ya kanuni adhimu ya haki za msingi za binadamu ambayo inakataza mtu au mamlaka yoyote ile kuamua jambo ambalo mtu huyo au mamlaka hayo wana masilahi nalo.
Na mahakama zote Tanzania na duniani zinazingatia kanuni hii.
Ripoti ya Tume ya Jaji Nyalali ya mwaka 1991 ilisisitiza (katika ibara ya 591) kuwa muundo wa Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sharti ubadilike ili kukidhi haja ya demokrasia ya vyama vingi. Ili kuhakikisha kuwa Tume ya Uchaguzi inakuwa huru, katika ibara ya 592 Ripoti hiyo ilisema kuwa, “Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi sharti wachaguliwe na Bunge au Baraza la wawakilishi. Wakurugenzi wa uchaguzi ambao watakuwa ni Makatibu wa Tume ya Uchaguzi nao sharti wachaguliwe na Bunge au Baraza la Wawakilishi baada ya kupendekezwa na Tume Ajiri zinazohusika.”
Ni dhahiri mapendekezo hayo ya Tume ya Jaji Nyalali yalizingatia kuwa uchaguzi wa vyama vingi sharti uendeshwe kwa viwango vinavyokubalika kisheria na kiutaratibu duniani kote. Kwa mfano Tamko la Dunia kuhusu Haki za Binadamu la mwaka 1948 linasisitiza kufanyika kwa uchaguzi wa kweli ulio huru na haki. (Ibara ya 21(3).
Sharti hili lilisisitizwa baadaye na Sheria ya Kimataifa kuhusu Haki za Kisiasa na Kiraia ya 1966 (Ibara ya 25(b). Na msemo maarufu labda katika medani ya utoji haki duniani unasema, “Haitoshi kwamba haki imetendeka; sharti ionekane kuwa imetendeka.”
Katika mazingira ya Katiba na sheria za uchaguzi hapa nchini haki haiwezi kutendeka wala kuonekana imetendeka kwa sababu zifuatazo.
Kwa mujibu wa ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Uchaguzi ina wajumbe wafuatao wanaoteuliwa na Rais; Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wengine wanaotajwa na sheria iliyotungwa na Bunge.
Pia, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ambaye ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi naye huteuliwa na Rais kufanya kazi kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 (pamoja na mabadiliko yake). Ndiyo kusema, kimsingi Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 ilikuwa kwa ajili ya chaguzi za chama kimoja tu.
Mbali na Mkurugenzi wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi ni wakurugenzi wa majiji, Manispaa, Miji na wakurugenzi watendaji wa wilaya na watendaji wengine wote huteuliwa na Rais na hakika wote ni waajiriwa wa Serikali ya chama tawala.
Rais anaweza kumuondoa katika madaraka mjumbe yeyote wa Tume akipenda kufanya hivyo kwa mujibu wa Ibara ya 74(5) ya Katiba. Hakika basi, Rais ndiye mteuzi mkuu, mdhibiti na mnadhimu wa wajumbe, watendaji wakuu na hata wafanyakazi wote wa Tume ya Uchaguzi.
Hoja ya kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi pia ilijadiliwa na Kamati ya Kuratibu Maoni Kuhusu Katiba 1999 iliyoongozwa na Jaji Rufaa Mstaafu Robert Kissanga. Moja ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo yalidai kwamba, “Muundo wa Tume ya Uchaguzi hauzingatii uwakilishi wa vyama vya siasa na kwamba wajumbe wa Tume huteuliwa na Rais ambaye pia anaweza kuwa ni kiongozi wa chama cha siasa kinachotawala. Kwa sababu hiyo, wajumbe wa Tume katika utendaji wa kazi zao, ama watakuwa na upendeleo kwa Chama husika au watakuwa wanalipa fadhila kwake. Wanaotoa hoja hii wanapendekeza kwamba kuwe na chombo kitakachochuja majina ya wajumbe wa Tume kabla Rais hajawateua.” Wengi wanakumbuka kabisa kuwa Rais wa wakati huo Benjamin Mkapa hakupendezwa na mapendekezo ya Ripoti ya Kamati hiyo mpaka akaonyesha hisia zake hizo waziwazi dhidi ya Mwenyekiti wake Jaji Robert Kissanga.
Serikali ilipinga mapendekezo hayo kwa kudai kwamba, “... ili Tume ya Uchaguzi iweze kutekeleza majukumu yake bila woga wala upendeleo, inapaswa kuwa ya kitaalamu au yenye wajumbe wenye hadhi, wanaokubalika na ambao uteuzi wao hautazingatia mwelekeo wa siasa wa chama chochote. Muundo wa sasa wa Tume unazingatia sifa hizo na serikali inaona muundo huo uendelee.” Kisha serikali ilipigilia msumari kwa kudai, “Kwa upande wa wateuzi wa Tume ya Uchaguzi serikali inaona kwamba Rais ambaye ana dhamana kubwa kikatiba ya kuwateua hata majaji, aendelee kuwateua wajumbe wa Tume.” Waingereza husema, “ He who pays the piper chooses the tune.” Yaani, “Amlipaye mpiga nzumari huchagua mwimbo.” Na kisheria tunarejea pale pale kwamba, “Haitoshi kuwa haki imetendeka, sharti ionekane kuwa imetendeka.”
Na sasa, chombo shehena, jaliza nanga! Maana watendaji ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi kama tulivyoona hapo juu wana hofu ya kutumbuliwa pale watakapotangaza kuwa wagombea wa upinzani wameshinda kuanzia udiwani hadi urais. CCM wanataka kushinda nafasi zote, kwa vyovyote vile! Kama alivyosema Mzee Ngombale Mwiru, mwanasiasa nguli nchini aliyehama CCM mwaka 2015 kuwa,“Wapinzani hawawezi kuingia Ikulu bila ya kuwepo Tume Huru ya Uchaguzi.”
‘Ushindi wa kishindo’ wa CCM katika uchaguzi wa madiwani uliofanyika tarehe 25 Novemba 2017 ambapo upinzani unadaiwa kupata kiti kimoja tu cha udiwani kati ya viti arubaini na tatu, kwa kurejea msemo wa Waingereza ni “too good to be true.” Ni mbinu ya kuwakatisha tamaa wapinzani kuwa hawapendwi. Ni ithibati kamili ya kauli ya Mzee Ngombale Mwiru iliyorejewa punde.
Jumanne 28 Novemba 2006, Mwakilishi Mkazi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania, Oscar Fernandez Taranco “... alizitaka nchi za Kiafrika kuzingatia kanuni za demokrasia, utawala bora na kulinda haki za binadamu wakati wa chaguzi...” Akasisitiza kuwa, “Nia ni kuwa na mfumo wa uchaguzi ambao hautashawishi malalamiko kutoka kwa wale wanaoshindwa baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.”
Kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi ndiyo ajenda kuu kwa upinzani ili kupata demokrasia ya kweli Tanzania na kuepusha vurugu na uvunjifu wa amani ambao umetokea katika nchi nyingine Afrika na duniani kwa jumla.

No comments:

Post a Comment