Wednesday, May 22

Maalim Seif: Nitaomba kuwania tena urais mwaka 2015

Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema ataomba tena kugombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV, Maalim Seif alisema kuwa anachoomba tu Mwenyezi Mungu ampe afya njema.
“Ni uamuzi wa wananchi na wanachama wenyewe wa CUF lakini kama Mwenyezi Mungu akinipa afya na uzima bado nia ipo,” alisema Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Alisema hivi sasa chama hicho kimekuwa kikijiimarisha visiwani huko kwa kufanya mikutano Pemba na Unguja ili kuhakikisha kinaendelea kukubalika kwa wananchi.
Kauli hiyo ya Maalim Seif ambaye amekuwa akiwania nafasi hiyo tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi, ilipokewa kwa hisia tofauti ambapo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bashiru Ali alisema vyama vya siasa ni lazima viwe vinatayarisha viongozi wa baadaye ambao watafahamu kwamba uongozi ni dhamana wanayopewa na wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema Maalim Seif kama mwanachama wa chama hicho anaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa dola.

No comments:

Post a Comment