MENEJA wa Hoteli ya Kitalii ya Tree Top, iliyoko katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, wilayani Monduli ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na ngozi za chui nyumbani kwake, akiwa katika harakati za kuisafirisha kinyemela kwenda nje ya nchi.
Habari zilizothibitishwa na Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete, zilisema mtuhumiwa huyo anayeaminika kuwa ni raia wa Afrika Kusini alikotarajia kupeleka ngozi hiyo, alikamatwa saa 11 jioni ya Desemba 21, mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari hizo, kabla ya kutiwa mbaroni, Kikosikazi kinachoundwa na askari kutoka Tanapa, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), kilifanya upekuzi nyumbani kwa meneja huyo baada ya kupokea taarifa za siri kuwa anajihusisha na ujangili na kuuza isivyo halali, nyara za Serikali.
“Ni kweli mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kikosikazi chetu kupata taarifa kuwa anamiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria na kweli baada ya upekuzi alikutwa na ngozi ya chui,” alisema Shelutete kwa njia ya simu jana.
Alisema suala hilo tayari limefikishwa polisi katika Kituo cha Mto wa Mbu, wilayani Monduli kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi za kisheria kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Habari zaidi zilidai kuwa mtuhumiwa aliyepelekwa katika Kituo cha Polisi cha Karatu ambako ndiko yalipo makao makuu ya Kikosikazi cha kupambana na ujangili katika Hifadhi za NCAA, Manyara na Tarangire.
Inasemekana hata hivyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kudhaminiwa na mfanyakazi mmoja wa Hoteli za Sopa Lodges inayomiliki msururu wa hoteli kwenye mbuga za wanyama katika Mikoa ya Arusha na Mara.
Katika nyumba ilimokutwa nyara hizo za Serikali, inasemekana nyara zilikutwa zikiwa zimefungwa kwenye mfuko maalum tayari kusafirishwa huku jina na anwani ya mpokeaji ikiwa pia imeandikwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas aliyezungumza kwa njia ya simu akiwa njiani akitokea Moshi kwenda Arusha, aliahidi kulifualia suala hilo na kulitoa ufafanuzi suala hilo baada ya kufika ofisini.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la matukio yanayohusishwa na vitendo vya ujangili hatua ambayo inahatarisha usalama wa baadhi ya nyara za Serikali. Wiki iliyopita Serikali ilitangaza kutia mbaroni mtandao wa ujangali uliokuwa ukijihusisha na biashara haramu ikiwemo wa pembe za ndovu
No comments:
Post a Comment