Dk Mahenge amesema kutamka ukame ni kisingizio cha uvivu na ni sawa na watu wasiokuwa na maono.
Akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Chemba leo Jumanne katika mfululizo wa ziara zake, Dk Mahenge amesema haiingii akilini kutaja habari za ukame ilihali mkoa unafaa katika kilimo cha mazao mengi.
"Hata katika nchi ambazo ni jangwa lakini chini yake wana mafuta, hapa kwetu ukame tunauita sisi wenyewe," amesema Dk Mahenge.
Amewataka watumishi kubadilika kifikra ili wawape elimu wakulima wao watakaoweza kulima mazao yanayostahili katika maeneo ya mvua chache kama ilivyo mkoani humo.
Amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha wanashughulikia matatizo mengine lakini isiwe katika suala la njaa.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amesema wilaya yake imeweka mikakati ya kujitosheleza kwa chakula na kumaliza migogoro ambayo hupunguza muda wa uzalishaji.
Odunga amesema Chemba imejidhatiti kupambana na upungufu wa chakula na wanayo ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo.
"Hata hivyo tumeainisha mazao yanayotakiwa kulimwa kwa kila kata kutokana na mtawanyiko wa mvua za msimu," amesema Odunga.
Hata hivyo mkuu huyo amesema kuwa tofauti na maeneo mengine, Chemba wameendelea kukaribisha mifugo kwa kuwa ndiyo fursa kwao katika kuchangia maendeleo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge amesema mambo mengi yatafanikiwa ikiwa watumishi watafuata utaratibu na kutimiza wajibu wao.
Kwa mujibu wa Madenge bila ya kufuata utaratibu mzuri wa kiusimamizi hakuna kinachoweza kubadilika mkoani humo.
No comments:
Post a Comment