Tuesday, November 14

Dk Shika asema nyumba za Lugumi bado zinahitajiwa na kampuni yake



Dar es Salaam. 'Bilionea' wa nyumba za Lugumi, Dk Louis Shika ameachiwa na kwenda kupanda daladala kuelekea nyumbani huku akisema mpango wake wa kununua nyumba za Lugumi uko palepale.
Baada ya kuachiwa na polisi leo Jumanne jioni amesema kwamba bado mpango wake wa kununua nyumba hizo uko palepale.
Amesema anachosubiri sasa ni fedha kuingizwa kwenye akaunti yake na kulipa asilimia 25 anayodaiwa.
"Siku nikipeleka fedha nataka Yono na TRA waite waandishi wa habari waone na wautangazie umma," amesema.
Amesema vyombo vya habari vimetoa taarifa zake lakini vitaumbuka siku akienda kupeleka fedha hizo.
Ameendelea kusisitiza kwamba nyumba hizo zinahitajiwa na kampuni yake ambayo hakuitaja.
Njiani wakati akielekea kwenye kituo cha daladala cha Mnazi Mmoja, Dk Shika alikuwa kivutio kwa watu aliokuwa akipishana nao.
Alipopanda daladala la Tabata Mawenzi, kondakta alimkaribisha kwa kumweleza karibu mzee Shika.
Kauli hiyo iliwaamsha abiria ambao walikuwa na hamu ya kumwona.
Dk Shika alipanda daladala na kusimama huku akionyesha tabasamu lisiloisha.

No comments:

Post a Comment