Tuesday, November 14

Macho yote kwa Jaji Maraga


Nairobi, Kenya. Mahakama ya Juu inatarajiwa kufanya mkutano wa usikilizwaji wa awali leo wa kesi tatu za kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta zilizofunguliwa hivi karibuni kabla ya kuanza rasmi kibarua cha kusikiliza na kutoa hukumu.
Kesi zilizofunguliwa; ya kwanza ilipelekwa kortini na aliyekuwa Mbunge wa Kilome John Harun Mwau, ya pili iliwasilishwa na viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali Njonjo Mue na Khelef Khalifa ilhali ya tatu ilifunguliwa na Taasisi ya Demokrasia na Usimamizi (IDG) kupitia kwa wakili Kioko Kilukumi.
Katika kikao hicho kilichotarajiwa kuanza saa 5:00 asubuhi majaji na mawakali wa pande wote wanatarajia kukubaliana juu ya kanuni za kuongoza usikilizwaji wa kesi hadi hukumu. Jaji Mkuu David Maraga, mtu ambaye huzingatia sana matumizi ya muda ataupatia kila upande muda wa kuwasilisha hoja.
Walalamikaji watapewa muda mrefu zaidi wa kuwasilisha madai yao. Baada ya wajibu maombi kutoa hoja zao, walalamikaji watapewa tena fursa ya kuweka msisitizo katika hoja zao kwa mujibu wa sheria.
Katika usikilizwaji wa awali shughuli nyingine itakayofanywa na mahakama leo ni kusikiliza maombi ya wanaotaka kushirikishwa katika kesi hiyo dhidi ya Rais Kenyatta. Ombi la kwanza ni la mwanasheria mkuu, Profesa Githu Muigai kisha la aliyewania kiti hicho cha urais, Dk Ekuru Aukot.
Profesa Muigai ameeleza mahakama kuwa ni mshauri mkuu wa Serikali katika masuala yote ya sheria wakati Dk Aukot anasema katika ombi lake kwamba ana ushahidi utakaowezesha mahakama kufikia uamuzi wa haki.
Hii ni mara ya pili ushindi wa Rais Kenyatta unawekwa katika mikono ya Mahakama ya Juu baada ya kesi ya kwanza iliyofunguliwa na muungano wa vyama vya upinzani (Nasa) kupinga uchaguzi wa Agosti 8, 2017.
Septemba Mosi mahakama ilikubaliana na madai ya mlalamikaji kiongozi wa Nasa, Raila Odinga kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki hivyo ikaubatilisha ushindi wa Rais Kenyatta.

No comments:

Post a Comment