Thursday, November 2

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZUNGUMZA NA BAADHI YA WATANZANIA WAISHIO NCHINI CANADA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waishio Canada wadumishe mshikamano wao na wawe na uzalendo kwa Taifa lao.

Ametoa wito huo jana (Jumanne, Oktoba 31, 2017) wakati akizungumza na Watanzania waishio Toronto, Canada.

Waziri Mkuu ambaye yuko Canada kwa ziara ya kikazi, alisema kila Mtanzania anapaswa ahubiri utaifa wake. “Tembea huku ukiringia nchi yako, wakati wote ringia nchi yako, unapotakiwa kuisemea nchi yako, isemee vizuri kama ambavyo wengine wanasemea vizuri nchi zao licha ya matatizo waliyonayo.”

Aliwataka wakumbuke kuweka akiba na wanapopata fursa watume fedha zao nyumbani ili zisaidie kuleta maendeleo. “Ukipata kitu kidogo, rusha nyumbani; ukipata mtu anayeweza kuleta tija, mlete nyumbani, nasi tutawapokea wewe na yeye,” alisisitiza. 

“Tunawasisitiza muitangaze nchi yetu kwa mataifa mengine ili nao waone Tanzania ni mahali pa fursa, na akitaka kuwekeza ajue kuwa anawekeza mahali ambapo ni salama,” alisema.

Alisema Serikali inasisitiza wananchi waishio nje ya nchi, wawe wazalendo na washirikiane kuhakikisha wanazitumia vizuri fursa za kimaendeleo kwa manufaa ya nchi yao.

Awali, Balozi wa Tanzania nchini Canada, Mhe. Jack Nzoka, alitumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania waishio nchini humo wazingatie sheria za nchi hiyo.“Wote sisi tunawatambua kama mabalozi katika nafasi zenu hapa Canada. Tunawashauri muwe raia wema, na muishi kwa kufuata sheria na taratibu za nchi hii na msisahau mlipotoka, kwani hakuna mahali pazuri kama nyumbani,” alisisitiza.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATANO, NOVEMBA MOSI, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya watanzania waishio nchini Canada, kwenye hoteli ya The Ritz-Carlton Toronto Oktoba 31, 2017
Watanzania waishio nchini Canada,wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipo kutana nao kwenye hoteli ya The Ritz-Carlton Toronto Oktoba 31, 2017.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment