NA BASHIR YAKUB -
Kuna mambo ambayo yafaa tujihadhari nayo sana hasa kipindi hiki. Wengi wamefutiwa umiliki wa ardhi. Takwimu za kufutiwa ni kubwa sana kipindi hiki kama ulikuwa hujui. Kwa watu wanaonunua ardhi na kwenda kuishi nje ya nchi hili lawahusu sana kabla hamjapoteza ardhi zenu.
Najua unachojua kuhusu kutelekeza ardhi ni pengine kutokujenga, au kutoitumia kama ilivyopangiwa matumizi, nk. Ni kweli lakini hiyo ni maana finyu ya kutelekeza ardhi.
Maana ni zaidi ya hiyo, na hapa tutaona ili ujihadhari na uwezekano wa kupoteza ardhi yako.
1.MAMBO AMBAYO UKIFANYA UTAHESABIKA KUTELEKEZA ARDHI.
Mambo haya yameelezwa na Sheria Namba 4 ya ardhi ya 1999 kifungu cha 51(1).
( a ) Kutokulipa kodi, tozo au ushuru wowote ambao upo kisheria kwa ajili ya ardhi ni kutelekeza ardhi kwa mujibu wa sheria hiyo. Mnazijua kodi za majengo, kodi za ardhi nk. Hizi ni muhimu sana na kimsingi ndizo zinazoeleza uhai wa ardhi yako.
Ikiwa hulipi hizi hata kama eneo hilo umejenga kiwanda kinachofanya kazi saa 24 siku 7 za wiki bado mbele ya macho ya sheria unahesabika kutelekeza ardhi. Dawa ya kuepuka hili ni ndogo. Lipa hizo kodi na tozo kwa mujibu wa sheria. Yamkini hizi huwa si pesa nyingi sana ya kumshinda mmiliki kulipa.
( b ) Jengo ndani ya ardhi kuwa gofu ni kutelekeza ardhi kwa mujibu wa sheria. Lakini pia katika eneo hilo sheria imetumia neno “disrepair”. Maana yake kutokufanya ukarabati. Kwa tafsiri hii ni kuwa kumbe hata kutokufanyia majengo yetu ukarabati nako ni kutelekeza ardhi.
Utaona katikati ya miji yetu majengo ya zamani machafu, yaliyopauka. Japo ndani mwake watu wanaishi na maofisi yamo bado kwa tafsiri ya neno “disrepair” ni kuwa jengo hilo limetelekezwa. Na sheria imeeleza zaidi kuwa itakuwa mbaya zaidi ikiwa jengo hilo linahatarisha afya au maisha ya watumiaji wake , majirani au hata wapita njia.
( c ) Sheria inasema ikiwa mmiliki ardhi ameondoka nchini na hakuacha mtu yeyote hapa nchini wa kuangalia ardhi ile kwa ajili ya kuilinda na kutekeleza masharti yote yanayohitajika kisheria kwa ardhi hiyo basi atakuwa ametelekeza ardhi hiyo. Sheria imetaja kabisa maneno mtu “aliyeondoka nchini”. Hii maana yake ni maalum kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Unayemuachia ardhi kazi yake kubwa si kukaa kama mlinzi kwenye ardhi hiyo. Laa hasha, bali kazi yake kubwa ni kuhakikisha anatekeleza masharti ya umiliki wa ardhi kwa mujibu wa sheria kwa niaba yako.
Na kama kuna mambo ambayo yatahitaji sahihi yako basi ni kuhakikisha yanakufikia na kuyatia sahihi kama inavyohitajika.
Wengi walio nje wamefutiwa umiliki wa ardhi kwa kukosa hili. Usimamizi wa ardhi zao. Hata hiyvo kifungu hicho kimeeleza utaratibu wa kumtaarifu Kamishna wa rdhi kuhusu ardhi yako kabla hujaondoka kwenda nje. Hii inaweza sana kukuweka salama.
( d ) Pia ardhi kuacha kutumika kwa manufaa, au ardhi kuwa imeharibiwa kwa maana ya uharibifu wa mazingira nako ni kutelekeza ardhi. Unaweza kuwa uharibifu uliosababisha wewe au wa asili.
2. IPI ADHABU YA KUTELEKEZA ARDHI.
Adhabu ya kutelekeza ardhi ni kufutiwa umiliki kwa mujibu wa kifungu cha 49 cha sheria hiyo. Ukifutiwa umiliki ardhi yako atapewa mtu mwingine au itaingia kwenye hifadhi ya ardhi ya serikali inayosubiri kugawiwa. Ni kitu kibaya sana.
Makala nyingine nitaeleza taratibu zinazotakiwa kufuatwa kabla hujafutiwa umiliki wa ardhi ili ujue kama umeonewa iwapo limekutokea hili au kama halijakutokea ujue kuwa kwa dalili hizi sasa naanza kufutiwa umiliki.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE. 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment