Thursday, November 2

Lusinde azungumzia kujiuzulu Nyalandu


Dar es Salaam. Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde amezungumzia kujiuzulu kwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu akieleza ni kutokana na kuwepo kwa mfumo ulioanzishwa na Serikali kwa ajili ya kuchunguza utendaji wa viongozi waliopo na waliomaliza muda wao.
Amesema lengo la mfumo huo ni kuchunguza kila kiongozi aliyehusika au kutenda makosa yaliyolisababishia Taifa hasara wakati wa uongozi wake kabla ya kuwachukuliwa hatua za kisheria.
“Sasa hivi Serikali imetengeneza mfumo wa kuchambua sisi viongozi, wale waliokuwa viongozi wa zamani na sisi tuliopo, kujua nani fisadi na alikosea wapi ili wachukue hatua za kuwapeleka mahakamani, sasa nina wasiwasi mheshimiwa Nyalandu alikuwa amepata taarifa,”amesema Lusinde.
“Pengine yupo katika orodha ya uchunguzi, kwa hiyo akaona atumie fursa hii kukimbia ili baadaye atakapokuja kukamatwa au kuanza kuhojiwa asingizie kaanza kuhojiwa kwa sababu ya kwenda upinzani, mimi nina wasiwasi mahali siri zimevuja lakini siyo kwamba ana hoja ya msingi ya kuondoka CCM.”
Lusinde anayezungumza kupitia video inayosambaa mtandaoni amesema tangu alipomfahamu Nyalandu hakuwahi kumsikia akitoa mawazo yake katika kikao chochote cha halmashauri Kuu akimfananisha na mwanasiasa togwa (aliyepoa na asiye na msisimuko) na mwenye bahati ya kushika nafasi za uwaziri pekee.  
“Na ndiyo maana ninasema ni lini tangu ametoka kwenye uwaziri aliwahi kusimama bungeni kutoa hisia zake Spika akamkata, akasema hisia zake Spika akamtoa nje na polisi ni lini? Kwa hiyo kuhama kwake na hoja alizozitoa, hoja sita lakini kubwa kuliko zote ni Serikali kukigandamiza chama na kinashindwa kuisimamia(serikali),”amesema.
Akifafanua hoja hiyo, Lusinde  amesema Serikali anayoituhumu Nyalandu ina toufaui na CCM ya mwaka 1975 ambayo kiutendaji, katibu kata alikuwa mtendaji wa kata, mkuu wa wilaya akiwa Katibu wa CCM wilaya na mkuu wa mkoa akiwa katibu wa CCM mkoa.
“Kwa hiyo hakukuwa na kimbilio, ukikosana naye kwenye chama , unamkuta serikalini, akikuweka ndani serikalini, anakuja kukumaliza kwenye chama, sasa haipo Serikali hiyo, Serikali ya sasa ambayo Nyalandu hakuielewa inajengwa kuondoa siasa za hovyo, majukwaa na kupeleka siasa za kazi, pengine Nyalandu hakuzoea siasa hizi,”amesema.
 Amesema katika hoja sita alizotoa Nyalandu, hakuna hata moja inayogusa mahitaji ya wananchi wa jimboni kwake, akituhumu kuwa ni hoja zake binafsi. 
“Hakuna hata moja, ni wapi aliposema anaondoka CCM kwa sababu haipeleki zahanati, haipeleki barabara, yote yanamuhusu yeye, kwa hiyo kuondoka kwa Nyalandu hakuna pengo isipokuwa kuna fursa,” amesema.

No comments:

Post a Comment