Thursday, November 2

Deni la Sh 250 milioni kumweka ndani meneja wa Diamond


Dar es Salaam. Meneja wa msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva), Abdul Nassib maarufu Diamond Platnum, Hamis Taletale na nduguye Idd Taletale sasa wanachungulia kifungo jela kwa kushindwa kulipa fidia ya Sh250 milioni, ambazo kampuni yao ya Tiptop Connection Limited inadaiwa.
Februari 18 mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliiamuru kampuni hiyo kumlipa fidia ya Sh250 milioni, Mhadhiri wa Dini ya Kiislam, Sheikh Mbonde kwa kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake, kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Hata hivyo meneja huyo wa Diamond, maarufu kama Babu Tale na nduguye wakiwa wakurugenzi na wanahisa pekee wa kampuni hawakuweza kulipa fidia hiyo wala kuweka wazi mali za kampuni hiyo, hivo Mbonde akalazimika kufungua maombi ya utekelezaji wa hukumu hiyo.
Mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Naibu Msajili Wilbard Mashauri Juni 9 mwaka huu iliwaamuru wakurugenzi hao wa kampuni hiyo kuweka wazi mali za zinazomilikiwa na kampuni yao hiyo.
Alisema kuwa iwapo watashindwa kutaja mali za kampuni hiyo basi wao wenyewe watalazimika kulipa kiasi hicho cha fedha au mali zao binafsi kukamatwa na kuuzwa na kwamba iwapo hawatakuwa na mali za kulipa fidia hiyo
“Kama hawana mali, basi watakamatwa na kufungwa gerezani kama wafungwa wa madai kwa mujibu wa masharti ya Amri ya 21 Kanuni ya 38(1) ya CPC (Kanuni za Mashauri ya Madai) Sura ya 33 marejeo ya mwaka 2002.”alisisitiza Naibu Msajili Mashauri.
Katika kutekeleza agizo la Mahakama kwa wakurugenzi hao, kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart & Co Ltd imewapa siku 14 Babu Tale na nduguye kutekeleza uamuzi na agizo hilo la Mahakama.
Taairifa hiyo ya Yono imekabidhiwa leo Alhamisi na Meneja Masoko wa Yono, Kene Mwankenja kwa mjumbe ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpakani, Kata ya Kwembe, wilayani Ubungo, Wilson John ili kuwafikishia kina Babu Tale
Iwapo hawataweka wazi mali za kampuni hiyo ili zipigwe mnada au walipe fidia hiyo ambayo kampuni yao inadaiwa ama kama hawatakuwa na mali zao binafsi ambazo zinaweza kupigwa mnada, basi wao wenyewe itabidi watupwe jela, kama Mahakama ilivyaomuru.
“Tumewapa notice (taarifa) hiyo ili kuwapa nafasi ya kumaliza suala hilo ndani ya muda huo. Wakilimaliza sawa, lakini wakipuuza basi wajibu wetu ni kutekeleza tulichoelekezwa.” amesema Mwankenja.
Katika hati ya madai ya kesi hiyo namba 185 ya mwaka 2013 na wakati wa usikilizwaji, Juni 6, 2013 Sheik Mbonde aliingia makubaliano na kampuni hiyo, kutumia kazi zake za mawaidha, kwa kuzalisha, kurekodi na kuzisambaza.
Pamoja na mambo mengine, walikubaliana kampuni kulipia gharama za kurekodi masomo na mafundisho ya mihadhara yake, kumnunulia gari, kumjengea nyumba na kugawana faida ya mauzo.
Hata hivyo, baada ya kukamilisha kurekodi masomo saba, maofisa wa kampuni hiyo walimkatia mawasiliano hadi alipobahatika kukutana na mmoja wao, Adam Waziri ambaye alimweleza kuwa wamesitisha mpango wa kuendelea na kazi hiyo.
Hata hivyo, Agosti 9, 2013, wakati mdai akiendesha mhadhara Bahi Dodoma, alibaini kuwa DVD za masomo yake zilikuwa zikiuzwa sokoni Dodoma na katika  mikoa mbalimbali kama vile Mbeya, Tanga na Dar es Salaam, bila ridhaa yake wala makubalino.
DVD hizo kwa mujibu wa hati hiyo zilikuwa ni za masomo mbalimbali aliyokuwa ameyatoa na kwamba makava ya DVD hizo yalikuwa na nembo na namba za simu za maofisa wa mdaiwa.

No comments:

Post a Comment