Thursday, November 2

Marais wa Afrika wammwagia sifa Uhuru Kenyatta


Nairobi, Kenya. Mataifa kadhaa barani Afrika yameelezea kuunga mkono matokeo ya uchaguzi wa marudio nchini Kenya yakisema  hayatarajii kuona Mahakama ya Juu nchini humo ikipinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi mitatu.
Wengi wa viongozi hao wamekuwa wakituma salama zao za pongezi kwa rais huyo mteule ambaye kuapishwa kwake kunasubiri kipindi cha siku kadhaa kupisha iwapo kama kuna raia anaweza kwenda mahakamani kupinga ushindi wake.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye hivi karibuni alichaguliwa kwa asilimia 98 ya kura, ilivyo kwa Rais Kenyatta alisema katika ujumbe wake kuwa ushindi wake (Rais Kenyatta) ni ushahidi tosha kuwa "Wakenya wana imani naye".
Naye Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wa Uganda ambaye amekuwa akikosolewa na wapinzani wake kwa kubana demokrasia amesema kuchaguliwa tena kwa Rais Kenyatta ni ishara tosha jinsi wananchi wa Kenya walivyokuwa na imani naye.
“Nakupa pongezi zangu za dhati na uanze kutekeleza uongozi sasa Wakenya wamekupa imani yao. Natumaini utaongoza Wakenya kwa njia ya kuwaunganisha pamoja na kuwatekelezea maendeleo ili uchumi wao ukue,” alisema.
Amesema kuwa anatazamia kuendeleza ushirikiano wa taifa lake na Kenya katika nyanja mbalimbali za kuleta manufaa kwa Wakenya na Waganda.
Rais wa Namibia, Hage Geingob amesema ushindi wa Rais Kenyatta ni mwafaka."Amenidhihirishia kuwa huweka maslahi ya taifa lake mbele,” alisema Geingob.
Nchini Somalia ambako Serikali ya Kenya imetuma vikosi vyake kwa ajili ya kusaidia kuleta amani, rais wake Mohammed Farmaajo ameonyesha kuridhishwa kwake na ushindi wa Rais Kenyatta na kuahidi kuendelea kushirikiana.
“Natumaini kuwa tutaendeleza ushirikiano wetu wa dhati kama mataifa jirani ili tupate ufanisi wa kuridhisha kwa watu wetu,” alisema.
Ushindi huo wa Kenyatta umepingwa na mpinzani wake, Raila Odinga ambaye anasisitiza kutaka kufanyika kwa uchaguzi mwingine.

No comments:

Post a Comment